Mkutano Mkuu
Sisi ni watoto Wake
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


9:42

Sisi ni watoto Wake

Sote tuna asili ya kiungu na uwezekano ule ule usio na ukomo kupitia neema ya Yesu Kristo.

Je, unakumbuka uzoefu ambao nabii Samweli alikuwa nao wakati Bwana alipomtuma nyumbani kwa Yese kumpaka mafuta mfalme mpya wa Israeli? Samweli alimwona Eliabu, mzaliwa wa kwanza wa Yese. Eliabu, ilionekana, alikuwa mrefu na alikuwa na mwonekano wa kiongozi. Samweli aliliona hilo na kufikia hitimisho. Na kumbe hilo lilikuwa si hitimisho sahihi, na Bwana alimfunza Samweli: “Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; … maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”1

Je, unakumbuka uzoefu ambao mfuasi Anania alikuwa nao wakati Bwana alipomtuma ambariki Sauli? Sifa ya Sauli ilikuwa imevuma, na Anania alikuwa amesikia kuhusu Sauli na ukatili wake, mateso yasiyokoma ya Watakatifu. Anania alisikia na kuhitimisha kwamba pengine hakupaswa kumhudumia Sauli. Na kumbe hilo halikuwa hitimisho sahihi, na Bwana alimfunza Anania: “Huyu ni chombo kiteule kwangu, kulichukua Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli.”2

Nini ilikuwa shida kwa Samweli na Anania katika mifano hii miwili? Walitazama kwa macho yao na kusikia kwa masikio yao, na kama matokeo, walitoa hukumu kwa wengine kulingana na mwonekano na fununu.

Wakati waandishi na Mafarisayo walipomwona mwanamke aliyeshikwa kwenye uzinzi, je, waliona nini? Mwanamke mpotovu, mwenye dhambi aliyestahili kifo. Yesu alipomwona, je, aliona nini? Mwanamke ambaye kwa muda alishindwa na udhaifu wa mwili lakini angeweza kurejea kupitia toba na Upatanisho Wake. Watu walipomwona akida, ambaye mtumishi wake alikuwa na ugonjwa wa kupooza, je, waliona nini? Pengine waliona mgeni, mtu wa nchi nyingine, mtu wa kukataliwa. Yesu alipomwona, je, aliona nini? Mwanamume aliyejali ustawi wa mtu wa nyumba yake, aliyemtafuta Bwana katika ukweli na imani. Wakati watu walipomwona mwanamke mwenye tatizo la kutokwa damu, je, waliona nini? Pengine mwanamke mchafu, aliyetengwa ili kuepukwa. Yesu alipomwona, je, aliona nini? Mwanamke mgonjwa, mpweke na aliyetengwa kutokana na hali yake ambayo hakuweza kuidhibiti, ambaye alitumaini kuponywa na kujumuishwa tena.

Katika kila hali, Bwana aliwaona watu hawa kwa jinsi walivyokuwa na kwa ufasaha aliwahudumia kila mmoja. Kama vile Nefi na kaka yake Yakobo walivyotangaza:

“Anawakaribisha wote kuja kwake … , weusi kwa weupe, wafungwa na walio huru, wake kwa waume; na anawakumbuka kafiri; na wote ni sawa kwa Mungu.”3

“Na mwanadamu mmoja ni mwenye thamani machoni mwake kama mwingine.”4

Nasi vilevile tusiruhusu macho yetu, masikio au hofu zetu zitupotoshe, bali tuifungue mioyo na akili zetu na tuhudumu kwa uhuru kwa wale wanaotuzunguka kama Yeye alivyofanya.

Miaka kadhaa iliyopita, mke wangu Isabelle, alipokea jukumu lisilo la kawaida la kuhudumu. Aliombwa kumtembelea mjane mzee katika kata yetu, dada mwenye changamoto za kiafya na ambaye upweke wake ulileta hasira kwenye maisha yake. Pazia zake zilikuwa hazifunguliwi; nyumba yake ilikuwa imejaa vitu; hakutaka kutembelewa na aliweka wazi kwamba “hakuna chochote ninachoweza kufanya kwa yeyote.” Bila kukata tamaa, Isabelle alijibu, “Ndiyo, kipo! Unaweza kufanya kitu kwetu kwa kuturuhusu tuje tukutembelee.” Na hivyo Isabelle alikwenda, kwa uaminifu.

Muda fulani baadaye, dada huyu mzuri alifanyiwa upasuaji kwenye mguu wake, ambao ulihitaji bandeji yake ibadilishwe kila siku, jambo ambalo hakuweza kulifanya peke yake. Kwa siku nyingi, Isabelle alikwenda nyumbani kwake, akaiosha miguu yake, na kubadilisha bandeji zake. Isabelle kamwe hakuona ubaya; kamwe hakusikia harufu ya uvundo. Alimwona tu binti mrembo wa Mungu katika uhitaji wa upendo na uangalizi mzuri.

Kwa miaka mingi, mimi na wengine wengi wasio na idadi tumebarikiwa kwa kipawa cha Isabelle cha kuona kama Bwana anavyoona. Iwe wewe ni rais wa kigingi ama mkaribishaji kwenye kata, iwe wewe ni mfalme wa Uingereza au unaishi kwenye kijumba kidogo, iwe unazungumza lugha ya Isabelle au lugha tofauti, iwe unatii amri zote au unahangaika kwenye baadhi, atakuhudumia chakula chake bora zaidi katika sahani zake bora zaidi. Cheo cha kiuchumi, rangi ya ngozi, historia ya utamaduni, utaifa, kiwango cha uadilifu, nafasi ya kijamii, au utambulisho au jina lingine lolote havina madhara kwake. Anatazama kwa moyo wake; anamwona mtoto wa Mungu ndani ya kila mtu.

Rais RussellM. Nelson amefundisha:

“Mjaribu anafurahia kwenye majina ya utani kwa sababu yanatugawa na kuzuia jinsi tunavyofikiri kuhusu sisi wenyewe na kuhusu kila mmoja. Inahuzunisha kiasi gani tunapoheshimu zaidi majina ya utani kuliko tunavyoheshimiana.

Majina ya utani yanaweza kuongoza kwenye kuhukumu na chuki. Aina yoyote ya Unyanyasaji au chuki juu ya mwingine kwa sababu ya utaifa, rangi, mtazamo wa kijinsia, jinsi, shahada za elimu, utamaduni au utambulisho mwingine ni chukizo kwa Muumba wetu!”5

Ufaransa sivyo nilivyo mimi; ni mahala nilipozaliwa. Mweupe sivyo nilivyo mimi; ni rangi ya ngozi yangu, au ukosefu wa rangi. Profesa sivyo nilivyo mimi; ni kile nilichofanya kuisaidia familia yangu. Sabini Mkuu Mwenye Mamlaka sivyo nilivyo mimi; ni mahala ninapohudumu katika ufalme kwa sasa.

“La kwanza na muhimu,” kama Rais Nelson alivyotukumbusha, mimi ni “mtoto wa Mungu.”6 Nawe pia, na ndivyo ilivyo kwa watu wote wanaotuzunguka. Ninaomba kwamba tufikie kwenye kuuthamini sana ukweli huu wa kupendeza. Unabadilisha kila kitu!

Yaweza kuwa tumelelewa katika tamaduni tofauti; yaweza kuwa tunatoka kwenye hali tofauti za kijamii na kiuchumi; urithi tofauti wa duniani, ikiwa ni pamoja na utaifa wetu, rangi ya ngozi, mapendeleo ya vyakula, mtazamo wa kisiasa, n.k. vinaweza kutofautiana sana. Lakini sisi ni watoto Wake, sisi sote bila upendeleo. Sote tuna asili ya kiungu na uwezekano ule ule usio na ukomo kupitia neema ya Yesu Kristo.

C. S. Lewis aliliweka hivi: “Ni kitu muhimu kuishi kwenye jamii ya miungu wa kiume na miungu wa kike, ili kukumbuka kwamba mtu goigoi asiyevutiwa na lolote ambaye unaweza kuzungumza naye siku moja anaweza kuwa kiumbe ambacho, kama ungekiona sasa, kwa dhati ungeshawishika kukiabudu. … Hakuna watu wa ambao ni wa kawaida. Hujawahi kamwe kuzungumza na mtu wa kawaida tu. Mataifa, tamaduni, sanaa, ustaarabu—haya ni mambo ya muda, na uhai wake kwetu ni kama uhai wa mbu. Bali ni watu wasio kufa ambao tunataniana nao, tunafanya nao kazi, tunafunga nao ndoa, tunawachukia na kuwanyanyasa.”7

Familia yetu imebahatika kuishi katika nchi na tamaduni mbalimbali; watoto wetu wamebarikiwa kuoa makabila mbalimbali. Nimekuja kutambua kwamba injili ya Yesu Kristo ni mletaji mkuu wa usawa. Tunapokumbatia injili, “Roho mwenyewe anashuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu.”8 Ukweli huu wa kustaajabisha hutuweka huru, na majina yote ya utani na matabaka ambayo kwa namna nyingine yangetutesa sisi na mahusiano yetu na kila mmoja “yamezwe kwenye shangwe ya Kristo.”9 Punde inakuwa wazi kwamba sisi, na wengine vilevile, “si wageni wala wapitaji, bali wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.”10

Hivi karibuni nilimsikia rais wa tawi wa moja ya kitengo chetu cha lugha za tamaduni mbalimbali akirejelea hili, jinsi ambavyo Mzee Gerrit W. Gong amelirejelea, kama kuwa wa agano.11 Dhana ya kupendeza iliyoje! Tunajumuishwa kwenye kundi la watu ambao wanajitahidi kumweka Mwokozi na maagano yao kwenye kiini cha maisha yao na kuishi injili kwa shangwe. Hivyo basi, badala ya kumwangalia kila mmoja kupitia lenzi iliyoharibiwa ya maisha ya duniani, injili inainua uoni wetu na kuturuhusu tumwone kila mmoja kupitia lenzi isiyo na dosari, isiyobadilika ya maagano yetu matakatifu. Kwa kufanya hivyo, tunaanza kuondoa chuki na ubaguzi wetu asilia dhidi ya wengine, jambo ambalo huwasaidia wao wapunguze chuki na ubaguzi wao dhidi yetu,12 katika mduara wa kupendeza wa wema. Hakika, tunafuata mwaliko wa nabii wetu mpendwa: “Akina kaka na dada zangu wapendwa, jinsi tunavyotendeana ndicho cha muhimu! Jinsi tunavyozungumza na wengine na kuwahusu wengine iwe nyumbani, kanisani, kazini na mtandaoni ndiyo muhimu hasa. Leo, ninawaomba tuchangamane na wengine katika njia ya juu na takatifu zaidi.”13

Mchana huu, katika roho ya mwaliko, ninataka niongeze hakikisho langu kwenye lile la watoto wetu wa kupendeza wa Msingi:

Ikiwa huenendi kama watu wengi wanavyoenenda,

Baadhi ya watu watakuacha,

Lakini mimi sitakuacha! Sitakuacha!

Ikiwa hutazungumza kama watu wengi wanavyozungumza,

Baadhi ya watu wanakuzungumzia na kukucheka,

Lakini mimi sitafanya hilo! Sitafanya!

Nitatembea nawe. Nitazungumza nawe.

Hivyo ndivyo nitakavyoonesha upendo wangu kwako.

Yesu hakumwacha yeyote.

Aliutoa upendo wake kwa kila mmoja.

Nami nitafanya hivyo! Nitafanya hivyo!14

Ninashuhudia kwamba Yeye tunayemwita kama Baba yetu wa Mbinguni hakika ni Baba yetu, kwamba anatupenda, kwamba anamfahamu kwa undani kila mtoto Wake, kwamba anajali kwa dhati kuhusu kila mmoja, na kwamba sisi sote ni sawa Kwake. Ninashuhudia kwamba jinsi tunavyotendeana ni dhihirisho la moja kwa moja la uelewa wetu na heshima yetu kwa dhabihu ya juu na Upatanisho wa Mwana Wake, Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Ninaomba kwamba, kama Yeye, tuwapende wengine kwa sababu hilo ndilo jambo sahihi kufanya, na si kwa sababu wanafanya yaliyo sahihi au kufanya “yanayonafaa”. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. 1 Samweli 16:7.

  2. Matendo ya Mitume 9:15.

  3. 2 Nefi 26:33.

  4. Yakobo 2:21.

  5. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, May 15, 2022), Gospel Library.

  6. Russell M. Nelson, “Choices for Eternity.”

  7. C. S. Lewis, The Weight of Glory and Other Addresses (1949), 14–15.

  8. Warumi 8:16

  9. Alma 31:38.

  10. Waefeso 2:19.

  11. Ona Gerrit W. Gong, “Kuwa wa Agano,” Liahona,, Mei 2019, 80–83.

  12. Dale G. Renlund na Ruth Lybbert Renlund, Ukuhani wa Melkizedeki: Kuelewa Mafundisho, Kuishi Kanuni (2018), 112.

  13. Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,“ Liahona, Mei 2023, 99.

  14. I’ll Walk with You,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 140–41