Ukweli wa Milele
Hitaji la kutambua ukweli sasa ni la msingi sana!
Akina kaka na akina dada, tunawashukuru kwa kujitolea kwenu kwa Mungu Baba na kwa Mwanawe, Yesu Kristo, na tunashukuru kwa upendo wenu na huduma kwa kila mmoja. Ninyi ni watu bora sana!
Utangulizi
Baada ya mimi na mke wangu, Anne kupokea wito wa kutumikia kama viongozi wa misheni, familia yetu iliazimia kujua jina la kila mmisionari kabla ya kwenda eneo la misheni. Tulipata picha, tukatengeneza kadi zenye maelezo machache kuwahusu wao na kuanza kuchunguza nyuso na kukariri majina.
Tulipowasili, tuliitisha mikutano ya utambulisho pamoja na wamisionari. Tulipokuwa tukichangamana, nilimsikia mvulana wetu wa miaka tisa akisema:
“Nafurahi kukutana nawe, Sam!”
“Rachel, unatokea wapi?”
“Wow, David, wewe ni mrefu!”
Baada ya kujua hilo, nilimwendea mtoto wetu na kumnong’oneza, “Hujambo, kumbuka kuwaita wamisionari Mzee au Dada.”
Aliniangalia kwa mshangao na kusema, “Baba, nilidhani tulipaswa kukariri majina yao.” Mwana wetu alifanya kile alichodhani kilikuwa sahihi kulingana na uelewa wake.
Hivyo, ni upi uelewa wetu wa ukweli katika ulimwengu wa leo? Mara kwa mara tunalipuliwa na mitazamo mikali, ripoti za upendeleo na data zisizo kamili. Wakati huo huo, ukubwa na vyanzo vya taarifa hii vinakuwa kwa kasi. Hitaji la kutambua ukweli sasa ni la msingi sana!
Ukweli ni muhimu kwetu ili kujenga na kuimarisha uhusiano na Mungu, kupata amani na shangwe na kufikia hatma yetu ya kiungu. Leo, ngoja tuzingatie maswali yafuatayo:
-
Ukweli ni nini na kwa nini ni wa muhimu?
-
Je tunaupataje ukweli?
-
Tuupatapo ukweli, je, tunaushiriki vipi?
Ukweli ni wa Milele
Bwana alitufundisha katika maandiko kwamba, “ukweli ni maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa” (Mafundisho na Maagano 93:24). “Haukuumbwa au kutengenezwa” (Mafundisho na Maagano 93:29) na “hauna mwisho” (Mafundisho na Maagano 88:66).1 Ukweli ni kamili, usiobadilika na usiofichika. Kwa maneno mengine, ukweli ni wa milele.2
Ukweli hutusaidia kuepuka uongo,3 kutambua jema kutokana na baya,4 kupokea ulinzi,5 na kupata faraja na uponyaji.6 Ukweli pia unaweza kuongoza matendo yetu,7 kutuweka huru,8 kututakasa,9 na kutuongoza kwenye uzima wa milele.10
Mungu Hufunua Ukweli wa Milele
Mungu hufunua ukweli wa milele kwetu kupitia mtandao wa uhusiano wa kimafunuo ukimuhusisha Yeye mwenyewe, Yesu Kristo, Roho Mtakatifu, manabii na sisi. Acha tujadili majukumu tofauti lakini yanayoingiliana ambayo kila mshiriki huyafanya katika mchakato huu.
Kwanza, Mungu ni chanzo cha ukweli wote wa milele.11 Yeye na Mwanawe, Yesu Kristo,12 wana uelewa mkamilifu wa ukweli na daima hutenda kulingana na kanuni na sheria za kweli.13 Nguvu hizi huwaruhusu Wao kutengeneza na kutawala ulimwengu14 pamoja na kutupenda, na kutuongoza, kutulea kikamilifu.15 Wanatutaka sisi tuelewe na tutumie ukweli ili sisi tuweze kufurahia baraka ambazo Wao wanazo.16 Wao wanaweza kuutoa ukweli huo binafsi au kwa kawaida, kupitia wajumbe kama vile Roho Mtakatifu, malaika au manabii wanaoishi.
Pili, Roho Mtakatifu hushuhudia ukweli wote.17 Yeye hufunua kweli kwetu moja kwa moja na hushuhudia juu ya ukweli uliofundishwa na wengine. Misukumo kutoka kwa Roho kwa kawaida huja kama mawazo akilini mwetu na hisia mioyoni mwetu.18
Tatu, manabii hupokea ukweli kutoka kwa Mungu na kushiriki ukweli huo pamoja nasi.19 Tunajifunza ukweli kutoka kwa manabii waliopita katika maandiko20 na kutoka kwa manabii walio hai kwenye mkutano mkuu na kupitia njia zingine rasmi za mawasiliano.
Mwishowe, wewe na mimi tuna jukumu muhimu katika mchakato huu. Mungu anategemea tutafute, tutambue na tutende juu ya ukweli. Uwezo wetu wa kupokea na kuutumia ukweli hutegemea uimara wa uhusiano wetu na Baba na Mwana, uitikiaji wetu kwenye ushawishi wa Roho Mtakatifu, na unyoofu wetu kwa manabii wa siku za mwisho.
Tunahitaji kukumbuka kwamba Shetani anafanya kazi kutuweka sisi mbali na ukweli. Anajua kwamba bila ukweli, hatuwezi kupata uzima wa milele. Anasuka nyuzi za ukweli kwa filosofia za ulimwengu ili kutukanganya na kutuvuruga sisi kutoka kwenye kile kinachowasilishwa na Mungu.21
Kutafuta, Kutambua na Kutumia Ukweli wa Milele
Tunapotafuta ukweli wa milele,22 maswali mawili yafuatayo yanaweza kutusaidia tutambue kama wazo hutoka kwa Mungu au kutoka chanzo kingine:
-
Je, jambo linafundishwa mara kwa mara katika maandiko na manabii walio hai?
-
Je, jambo hilo limethibitishwa kwa ushahidi wa Roho Mtakatifu?
Mungu hufunua kweli za kimaandiko kupitia manabii na Roho Mtakatifu huthibitisha kweli hizo na hutusaidia kuzitumia.23 Sisi lazima tutafute na tujiandae kupokea misukumo hii ya kiroho pale inapokuja.24 Tunapokea vyema ushuhuda wa Roho pale tuwapo wanyenyekevu,25 kuomba kwa dhati na kujifunza maneno ya Mungu,26 na kushika amri Zake.27
Pale Roho Mtakatifu anapothibitisha kuhusu ukweli mahususi kwetu, uelewa wetu huongezeka kwa kadiri tunapoiweka kanuni hiyo kwenye matendo. Baada ya muda, tunapoendelea kuishi kanuni hiyo, tunapata maarifa ya uhakika ya ukweli huo.28
Kwa mfano, nimefanya makosa na kuhisi hatia kwa chaguzi mbaya. Lakini kupitia sala, kujifunza na imani katika Yesu Kristo, nilipokea ushahidi wa kanuni ya toba.29 Nilipoendelea kutubu, uelewa wangu kuhusu toba ulikuwa imara. Nilihisi kuwa karibu na Mungu na Mwana Wake. Sasa najua kwamba dhambi inaweza kusamehewa kupitia kwa Yesu Kristo, kwa sababu nimepata baraka za toba kila siku.30
Mtumaini Mungu Wakati Ukweli Bado Haujafunuliwa
Je, tunapaswa kufanya nini tunapotafuta kwa dhati ukweli ambao bado haujafuniliwa? Ninawahurumia sana wale miongoni mwetu wanaotamani majibu ambayo hayaonekani kuja.
Kwa Joseph Smith, Bwana alishauri, “Nyamaza mpaka nitakapoona inafaa kuyafanya mambo yote yajulikane … kuhusu jambo hili” (Mafundisho na Maagano10:37).
Na kwa Emma Smith, Bwana alielezea “Usinungʼunike kwa sababu ya vitu ambavyo wewe hujaviona, kwani vimezuiliwa kwako na kwa ulimwengu, ambayo ni hekima kwangu katika wakati ujao” (Mafundisho na Maagano 25:4).
Mimi pia nimetafuta majibu kwa maswali ya nafsi. Majibu mengi yamekuja, na baadhi hayajaja.31 Tunapoendelea kusubiri—tukiamini hekima na upendo wa Bwana, tukishika amri zake na kutegemea kile ambacho tunajua—Yeye anatusaidia kupata amani mpaka afunue ukweli wa vitu vyote.32
Kuelewa Mafundisho na Sera
Tutafutapo ukweli, ukweli huo hutusaidia kuelewa tofauti kati ya mafundisho na sera. Mafundisho hurejelea kweli za milele, kama vile asili ya Uungu, mpango wa wokovu, na dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo. Sera ni matumizi ya mafundisho kulingana na hali ya sasa. Sera hutusaidia tulisimamie Kanisa kwa mpangilio.
Wakati mafundisho kamwe hayabadiliki, sera hubadilika mara kwa mara. Bwana hutenda kazi kupitia manabii Wake ili kuimarisha mafundisho Yake na kuboresha sera za Kanisa kulingana na mahitaji ya watoto Wake.
Kwa bahati mbaya, wakati mwingine tunachanganya sera na mafundisho. Kama hatuelewi tofauti, tunajihatarisha kukata tamaa pale sera zinapobadilika na kusababisha kuhoji hekima ya Mungu au jukumu la ufunuo la manabii.33
Kufundisha Ukweli wa Milele
Tunapopokea ukweli kutoka kwa Mungu, anatuhimiza kushiriki maarifa hayo na wengine.34 Tunafanya hili tunapofundisha darasa, kumwongoza mtoto au kujadili kweli za injili pamoja na rafiki.
Lengo letu ni kufundisha ukweli katika njia ambayo hualika nguvu ya uongofu ya Roho Mtakatifu..35 Acha nishiriki baadhi ya mialiko rahisi kutoka kwa Bwana na manabii Wake ambayo inaweza kusaidia.36
-
Fokasi kwa Baba wa Mbinguni, Yesu Kristo na mafundisho Yao ya msingi.37
-
Bakia imara kwenye maandiko na katika mafundisho ya manabii wa siku za mwisho.38
-
Tegemea mafundisho yaliyodhibitishwa kupitia mashahidi kadhaa wenye mamlaka.39
-
Epuka kubahatisha, maoni binafsi au mawazo ya kilimwengu.40
-
Fundisha kipengele cha mafundisho ndani ya mazingira yahusianayo na kweli za injili.41
-
Tumia mbinu za kufundisha ambazo hualika ushawishi wa Roho.42
-
Wasiliana wazi wazi ili kuepuka kutoelewana.43
Ongea Ukweli kwa Upendo
Jinsi tunavyofundisha ukweli ni jambo la msingi sana. Paulo anatuhimiza kuzungumza “ukweli katika upendo” (ona Waefeso 4:14–15). Ukweli huwa na nafasi nzuri ya kumbariki mtu mwingine wakati unapofikishwa kwa upendo kama wa Kristo.44
Ukweli ufundishwao bila upendo unaweza kusababisha hisia za hukumu, kukata tamaa na upweke. Daima hupelekea kwenye kinyongo na mgawanyiko—hata ugomvi. Kwa upande mwingine, upendo bila ukweli ni bure na hukosa ahadi ya ukuaji.
Vyote ukweli na upendo ni vya msingi katika ukuaji wetu wa kiroho.45 Ukweli hutoa mafundisho, kanuni na sheria zilizo muhimu kupata uzima wa milele, wakati upendo hukuza ari inayohitajika kukumbatia na kutenda juu ya kile kilicho kweli.
Daima nina shukrani kwa wengine ambao kwa subira walinifundisha kanuni za milele kwa upendo.
Hitimisho
Katika kuhitimisha, acha nishiriki kweli za milele ambazo zimekuwa nanga kwa nafsi yangu. Nimepata kujua kweli hizi kwa kufuata kanuni zilizojadiliwa leo.
Najua kwamba Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni.46 Yeye anajua yote,47 ana nguvu zote,48 na anapenda kwa ukamilifu.49 Alitengeneza mpango kwa ajili yetu ili tupate uzima wa milele na kuwa kama Yeye.50
Kama sehemu ya mpango huo, Yeye alimtuma Mwana Wake, Yesu kristo, atusaidie.51 Yesu alitufundisha tufanye mapenzi ya Baba52 na tupendane.53 Alilipia dhambi zetu54 na kuyatoa maisha Yake msalabani.55 Alifufuka kutoka wafu baada ya siku tatu.56 Kupitia Kristo na neema Yake, tutafufuka,57 tunaweza kusamehewa,58 na tunaweza kupata nguvu katika mateso.59
Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu alianzisha Kanisa Lake.60 Baada ya muda, Kanisa hilo lilibadilishwa na kweli zikapotea.61 Yesu Kristo alirejesha Kanisa Lake na kweli za injili kupitia Nabii Joseph Smith.62 Na leo, Kristo anaendelea kuongoza Kanisa Lake kupitia manabii na mitume walio hai.63
Ninajua kwamba tunaposonga kwa Kristo, hatimaye “tutakamilishwa ndani yake” (Moroni 10:32), kupata “shangwe kamili” (Mafundisho na Maagano 93:33), na kupokea “vyote ambayo Baba anavyo” (Mafundisho na Maagano 84:38). Juu ya kweli hizi za milele ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.