Mkutano Mkuu
Mpotevu na Njia Ambayo Inaongoza Nyumbani
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


14:32

Mpotevu na Njia Ambayo Inaongoza Nyumbani

Ingawa chaguzi zinaweza kukupeleka mbali kutoka kwa Mwokozi na Kanisa Lake, Bwana Mponyaji anasimama kwenye njia iongozayo nyumbani, kukukaribisha wewe.

Mtu Fulani Alikuwa na Wana Wawili.

Imeitwa na baadhi ya watu hadithi kuu fupi iliyowahi kusimuliwa.1 Kwa kuwa imetafsiriwa katika maelfu ya lugha kote ulimwenguni, inawezekana sana kwamba wakati wa milenia mbili zilizopita, jua halikutua bila hadithi hii kutajwa mahali fulani ulimwenguni.

Ilisimuliwa na Yesu Kristo, Mwokozi wetu na Mkombozi wetu, ambaye alikuja duniani “kuokoa kile kilichopotea.”2 Alianza kwa maneno haya rahisi: “Mtu fulani alikuwa na wana wawili.”3

Na mara moja, tunajifunza juu ya mgogoro wa kuvunja moyo. Mwana mmoja4 anamwambia baba yake hataki tena maisha ya pale nyumbani. Anataka uhuru wake. Anataka kuacha nyuma utamaduni na mafundisho ya wazazi wake. Anaomba mgao wa urithi wake—sasa hivi.5

Je, unaweza kufikiria kile baba huyu alichohisi aliposikia haya? Wakati alipotambua kwamba kile mwana wake alichotaka zaidi kuliko kitu chochote kingine ilikuwa ni kuiacha familia na labda asirudi kamwe?

Tukio Kuu

Mwana lazima alikuwa amehisi furaha ya safari na msisimko. Hatimaye, alikuwa peke yake. Huru kutokana na kanuni na sheria za utamaduni wa ujana wake, yeye angeweza sasa kufanya chaguzi zake mwenyewe bila ushawishi wa wazazi wake. Hakuna hatia tena. Angeweza kufurahia kukubalika na jamii yenye mawazo sawa na yake na kuishi maisha atakavyo yeye mwenyewe.

Alipowasili katika nchi ya mbali sana, mara moja alipata marafiki wapya na kuanza kuishi maisha aliyokuwa daima akiyatamani. Lazima alishabikiwa na wengi, kwani alitumia fedha bila kujali. Rafiki zake wapya—wafadhili wa upotovu wake—hawakumhukumu. Walisherehekea, wakasifia na hata kuunga mkono chaguzi zake.6

Kama kungekuwa na mitandao ya kijamii wakati huo, hakika, yeye angejaza kurasa zake mtandaoni kwa picha za marafiki wakicheka: #Kuishimaishayanguvizuri! #Mchangamfudaima! #Ningefanyahilikitambaosana!

Baa la Njaa

Lakini karamu haikudumu—ni nadra sana kudumu. Mambo mawili yalitokea: kwanza yeye aliishiwa fedha, na pili, baa la njaa lilisambaa kote nchini.7

Matatizo yalipokithiri, aliingiwa wasiwasi. Aliyekuwa haambiliki, mtu wa anasa sasa hangeweza kupata hata mlo mmoja, hata mahali pa kuishi. Je, angenusurika vipi?

Alikuwa mkarimu sana kwa marafiki zake—kwa nini hawangemsaidia sasa? Ninaweza kumuona akiomba msaada kidogo—kwa sasa tu—mpaka atapojiweza tena.

Maandiko yanatuambia, “Wala hapana mtu aliyempa kitu.”8

Akitapatapa kujaribu kubakia hai, alimpata mkulima mmoja ambaye alimwajiri kuwalisha nguruwe.9

Akiwa na njaa kali sana, aliyetengwa na mpweke, kijana huyu lazima alijiuliza jinsi ambavyo mambo yaliharibika na kwenda mrama kiasi hiki.

Sio tu tumbo tupu ambalo lilimsumbua. Ilikuwa ni nafsi tupu. Alikuwa na uhakika sana kwamba kujiingiza katika anasa za ulimwengu kungemfanya awe na furaha, kwamba sheria za maadili zilikuwa vikwazo kwa furaha hiyo. Na sasa alijua vyema zaidi. Na lo, ni gharama kiasi gani alilipia kupata maarifa hayo!10

Na njaa ya kimwili na kiroho zilipozidi, mawazo yake yalirudi kwa baba yake. Je, baba angemsaidia, baada ya yale yote yaliyotendeka? Hata walio masikini kati ya watumishi wa baba yake walikuwa na chakula na kimbilio kutokana na tufani.

Lakini kurudi kwa baba yake?

Hapana.

Kukiri kwa kijiji chake kwamba alikuwa ametapanya urithi wake?

Haiwezekani.

Kukutana na majirani ambao hakika walimuonya kwamba alikuwa anaidhalilisha familia yake na kuvunja mioyo ya wazazi wake? Kurudi kwa rafiki zake wa zamani baada ya kujigamba kwamba alikuwa huru?

Jambo zito hili.

Lakini njaa, upweke na majuto kweli hayangeweza kuisha—hadi “alipojirudi.”11

Alijua ni nini alihitajika kufanya.

Kurudi

Sasa turejee kwa baba, bwana wa nyumba aliyevunjika moyo. Ni mamia mangapi, labda maelfu, ya masaa aliyotumia kumhofia mwanaye?

Ni mara ngapi alikuwa ametazama njia ile ile ambayo mwanaye alikuwa ameichukua na upotevu mchungu aliouhisi wakati mwanaye akiondoka? Ni sala nyingi kiasi gani alizitoa usiku wa manane, akimsihi Mungu kwamba mwanaye angekuwa salama, kwamba angegundua ukweli, kwamba angerudi?

Na kisha siku moja, baba yule alitazama kwenye ile njia ya upweke—ile njia iongozayo nyumbani—akamuona mtu kwa mbali akitembea kumwelekea.

Je, inawezekana?

Ingawa yule mtu yuko mbali sana, baba yule anajua wakati ule ule kwamba alikuwa ni mwanaye.

Anamkimbilia, anamkumbatia na kumbusu.12

“Baba,” Mwana analia, kwa maneno ambayo huenda alikuwa ameyakariri mara elfu moja, “Nimekosa juu ya mbingu na mbele yako. Sistahili kuitwa mwana wako tena. Nifanye kama mmoja wa watumishi wako.”13

Lakini baba hakuacha amalize. Akiwa na machozi machoni mwake, anawaamuru watumishi wake: “Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike. Mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni. Nasi tule na kufurahi. Mwana wangu amerudi!”14

Sherehe

Katika ofisi yangu umetundikwa mchoro wa msanii Mjerumani Richard Burde. Mimi pamoja na Harriet tunaupenda mchoro huu. Unaonyesha mandhari ya upendo kutoka kwa mfano wa Mwokozi katika mtazamo wa kina.

Kurejea kwa Mwana Mpotevu, na Richard Burde.

Wakati kila mmoja akiwa amefurahia sana kurudi kwa yule mwana, mtu mmoja hakufurahia—kaka yake mkubwa.15

Anabeba mzigo fulani wa hisia.

Alikuwepo wakati kaka yake alidai urithi wake. Alishuhudia mwenyewe uzito mkubwa wa huzuni juu ya baba yake.

Tangu kaka yake aondoke, yeye amejaribu kumwondolea baba yake mzigo. Kila siku alifanya kazi kuponya moyo wa baba yake uliovunjika.

Na sasa yule mwana mbadhirifu alikuwa amerudi, na watu hawangejizuia kuwa pamoja na kaka yake huyo muasi.

“Miaka mingapi hii,” anamwambia baba yake, “Wala sijakosa amri yako wakati wowote. Lakini wakati wote huo, hukunifanyia sherehe.”16

Baba mwenye upendo anajibu, “Mwanangu mpendwa, vyote nilivyo navyo ni vyako! Hii si kuhusu kulinganisha thawabu au sherehe. Hii ni kuhushu uponyaji. Huu ndiyo ule wakati ambao tumekuwa tukiutumainia kwa miaka hii yote. Kaka yako alikuwa amekufa, na amefufuka tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa ameonekana!”17

Mfano wa Wakati Wetu

Wapendwa kaka na dada zangu, marafiki wapendwa, kama vile mifano yote ya Mwokozi, hili siyo tu kuhusu watu walioishi kitambo. Ni kuhusu wewe na mimi, leo.

Ni nani miongoni mwetu ambaye hajachepuka kutoka kwenye njia ya utakatifu, kwa upumbavu tukifikiria tungepata furaha zaidi kwa kufuata njia yetu wenyewe?

Ni nani miongoni mwetu ambaye hajahisi kunyenyekezwa, kuvunjika moyo na kutamani sana msamaha na rehema?

Pengine baadhi wanaweza kujiuliza, “Je, inawezekana kurejea? Nitakashifiwa milele, kukataliwa na kuepukwa na rafiki zangu wa zamani? Je, ni bora tu kubaki nimepotea? Je, Mungu atahisi vipi kama nikijaribu kurudi?”

Fumbo hili linatupatia jibu.

Baba yetu wa Mbinguni atatukimbilia sisi, moyo Wake ukifurikwa na upendo na huruma. Yeye atatukumbatia; kutuvika vazi kwenye mabega yetu, pete kidoleni na viatu kwenye miguu yetu, na kutangaza “Leo, tunasherehekea! Kwani mtoto wangu, ambaye alikuwa amekufa, amefufuka!”

Mbingu zitafurahia kurudi kwetu.

Shangwe Isiyoelezeka na Iliyojaa Utukufu

Je, naweza kuchukua dakika chache sasa na kuzungumza nanyi binafsi?

Bila kujali kile kinachoweza kuwa kilitendeka maishani mwako, ninapaza sauti na kutangaza maneno ya rafiki yangu mpendwa na Mtume mwenzangu Mzee Jeffrey R. Holland: “Haiwezekani kwako wewe kuzama chini zaidi kupita mng’aro wa ile nuru ya [dhabihu ya upatanisho] ya Kristo inavyong’ara.”18

Ingawa chaguzi zinaweza kukupeleka mbali kutoka kwa Mwokozi na Kanisa Lake, Bwana Mponyaji anasimama kwenye njia iongozayo nyumbani, kukukaribisha wewe. Na sisi kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo tunataka kufuata mfano Wake na kuwakumbatia ninyi kama akina kaka na akina dada zetu, kama marafiki zetu. Tunafurahia na kusherehekea pamoja nanyi.

Kurudi kwako hakutafifisha baraka za wengine. Kwani zawadi za Baba hazina kikomo, na kile kilichotolewa kwa mmoja kwa njia yoyote hakitafifisha hata kidogo haki ya kuzaliwa ya wengine.19

Sijifanyi kwamba kurudi ni kitu rahisi cha kufanya. Ninaweza kushuhudia juu ya hilo. Inaweza, kwa kweli, kuwa uchaguzi mgumu sana ambao utawahi kuufanya.

Lakini ninatoa ushahidi kwamba dakika ile unapoamua kurudi na kutembea katika njia ya Mwokozi na Mkombozi wetu, nguvu Zake zitaingia ndani ya maisha yako na kuyabadilisha.20

Malaika mbinguni watafurahia.

Na vivyo hivyo sisi, familia yako katika Kristo. Hata hivyo, sote tunajua jinsi kuwa mpotevu kulivyo. Sote tunategemea kila siku nguvu hizo hizo za upatanisho wa Kristo. Tunaijua njia hii, na tutatembea pamoja nawe.

La, njia yetu haitakosa majonzi, huzuni au uchungu. Lakini hatujafika hapa ila tu “kwa neno la Kristo na kwa imani isiyotingishika ndani yake, tukitegemea kabisa ustahili wa yule aliye mkuu kuokoa.” Na pamoja “tutasonga mbele kwa bidii katika Kristo, tukiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na [watu] wote.”21 Pamoja, “tutafurahia kwa shangwe isiyoelezeka na tukijaa utukufu,”22 kwani Yesu Kristo ni nguvu yetu!23

Ni maombi yangu kwamba kila mmoja wetu aweze kusikia, katika huu mfano mkuu, sauti ya Baba ikituita sisi tuingie katika njia iongozayo nyumbani—kwamba tuweze kuwa na ujasiri wa kutubu, kupokea msamaha, na kufuata njia iongozayo kurudi kwa Mungu wetu mwenye huruma na rehema. Kwa haya ninatoa ushuhuda na kuwaachieni baraka yangu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Inapatikana katika Luka 15, mfano ni moja ya mifano mitatu (kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea, na mwana aliyepotea) ambayo huonesha thamani ya vitu vilivyopotea na sherehe ambazo hufanyika wakati kile kilichopotea kinapopatikana.

  2. Luka 19:10.

  3. Luka 15:11.

  4. Mwana huyu labda alikuwa mdogo. Alikuwa hajaoa, ambayo ni ishara ya ujana wake, lakini si mdogo kiasi kwamba asingeweza kudai urithi wake na kuondoka nyumbani mara alipoupata.

  5. Kwa sheria na utamaduni wa Kiyahudi, mkubwa kati ya wana wawili alikuwa na haki ya mbili ya tatu ya urithi wa baba yake. Mwana mdogo, kwa hiyo, alikuwa na haki ya sehemu ya moja ya tatu. (Ona Kumbukumbu la Torati 21:17.)

  6. Ona Luka 15:13.

  7. Ona Luka 15:14.

  8. Luka 15:16.

  9. Kwa Wayahudi, nguruwe walichukuliwa kuwa “najisi” (ona Kumbukumbu la Torati 14:8) na walikuwa chukizo. Wanaofuata mila za Kiyahudi hawangeweza kufuga nguruwe, hii inaonesha kwamba msimamizi alikuwa myunani. Pia ingeweza kupendekeza umbali gani mwana huyu mdogo alikuwa amesafiri ili kuwa mbali na Wayahudi wacha Mungu.

  10. Mzee Neal A. Maxwell alifundisha: “Bila shaka, ni bora kama tunanyenyekezwa ‘kwa sababu ya neno’ badala ya kunyenyekezwa na mazingira, ingawa mazingira yanaweza kufanya hivyo! (ona Alma 32:13–14). Baa la njaa linaweza kuleta njaa ya kiroho” (“The Tugs and Pulls of the World,” Liahona, Jan. 2001, 45).

  11. Luka 15:17.

  12. Ona Luka 15:20.

  13. Ona Luka 15:18–19, 21.

  14. Ona Luka 15:22–24.

  15. Kumbuka, mwana mdogo alikuwa tayari amekwishapokea urithi wake. Kwa mwana mkubwa, hiyo ilimaanisha kwamba kila kitu chote kilikuwa chake. Kumpa chochote mwana mdogo kungemaanisha kukitwaa kutoka kwa mwana ambaye alibakia.

  16. Ona Luka 15:29.

  17. Ona Luka 15:31–32.

  18. Jeffrey R. Holland, “The Laborers in the Vineyard,” Liahona, Mei 2012, 33.

  19. Kile anachopatiwa mmoja hakififishi hata kidogo haki ya kuzaliwa ya wengine. Mwokozi alifunza hili fundisho wakati alipotoa mfano wa wafanyakazi katika Mathayo 20:1–16.

  20. Ona Alma 34:31.

  21. 2 Nefi 31:19–20.

  22. 1 Petro 1:8

  23. Ona Zaburi 28:7.