Stahimili Siku katika Kristo
Yesu Kristo hufanya iwezekane kwa ajili yetu “kustahimilli siku.”
Ilikuwa ni siku iliyojaa mifano mahsusi na ya moja kwa moja, maswali magumu na mafundisho mazito. Baada ya kutoa karipio kali kwa wale ambao walikuwa kama “makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote,”1 Yesu alifundisha mifano mitatu zaidi kuhusu maandalizi ya kiroho na ufuasi. Mojawapo ya hii ilikuwa mfano wa wanawali kumi.
“Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofananishwa na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana harusi.
“Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara.
“Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao:
“Bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao.
“Hata bwana harusi alipokawia, wote wakalala usingizi.
“Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana harusi; tokeni mwende kumlaki.
“Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
“Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
“Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
“Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana harusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye harusini; mlango ukafungwa.
“Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.”2
“Akajibu akasema, Amin, nawaambia, hamkunijua ninyi.”3
Kesheni kwa sababu hamjui siku wala saa wakati Mwana wa Adamu atakapokuja.”4
Rais Dallin H. Oaks aliuliza maswali yafuatayo ya kuchochoea mawazo kuhusiana na kuja kwa Bwana harusi:5 “Ingekuwaje kama siku ya ujio Wake ni kesho? Kama tungejua kwamba tungekutana na Bwana kesho—kupitia kifo chetu katika umri mdogo au kupitia ujio Wake usiotarajiwa —je tungefanya nini leo?”6
Nimejifunza kutokana na uzoefu binafsi kwamba maandalizi ya kiroho kwa ajili ya ujio wa Bwana si tu muhimu bali ndiyo njia pekee ya kupata amani na furaha.
Ilikuwa siku ya majira ya kiangazi kikavu niliposikia kwa mara ya kwanza maneno “Wewe una saratani.” Mimi pamoja na mume wangu tulipigwa na butwaa! Tulipokuwa tukirudi nyumbani, kimya kimya tukifikiria habari hizo, moyo wangu uliwageukia wana wetu watatu.
Akilini mwangu nilimuuliza Baba wa Mbinguni, “Je, nitakufa?”
Roho Mtakatifu alininong’oneza, “Kila kitu kitakuwa SAWA.”
Kisha nikauliza, “Je, nitaishi?
Tena, jibu likaja: “Kila kitu kitakuwa SAWA.”
Nilikanganyikiwa. Kwa nini nilipokea jibu lile lile ikiwa ningeishi au ningekufa?
Kisha ghafla kila kiungo cha mwili wangu kilijawa na amani kamili pale nilipokumbushwa: Hatukuhitaji kuharakisha kwenda nyumbani na kuwafundisha watoto wetu jinsi ya kusali. Walijua jinsi ya kupokea majibu na faraja kutoka kwenye sala. Hatukuhitaji kuharakisha kwenda nyumbani na kuwafundisha wao kuhusu maandiko au maneno ya manabii walio hai. Maneno hayo tayari yalikuwa chanzo cha kawaida cha nguvu na uelewa. Hatukuhitaji kuharakisha kwenda nyumbani na kuwafundisaha wao kuhusu toba, Ufufuo, Urejesho, mpango wa wokovu, familia za milele au hata mafundisho ya Yesu Krisro.
Kwa wakati huo kila somo la jioni ya familia nyumbani, kikao cha kujifunza maandiko, sala ya imani iliyotolewa, baraka zilizotolewa, ushuhuda uliotolewa, agano lililofanywa na kutunzwa, nyumba ya Bwana iliyohudhuriwa na siku ya Sabato iliyotunzwa vilikuwa na maana—ee, ni jinsi gani kila kimoja kilikuwa na maana! Hatukuwa tena na muda wa kutia mafuta kwenye taa zetu. Tulihitaji kila tone moja, na tulilihitaji papo hapo!
Kwa sababu ya Yesu Kristo na injili Yake iliyorejeshwa, kama ningekufa, familia yangu ingefarijiwa, ingeimarishwa na siku moja kurejeshwa. Kama ningeishi, ningepata nguvu kuu sana hapa duniani ili kusaidia kunifariji, kunihimili na kuniponya. Mwisho, kwa sababu ya Yesu Kristo, kila kitu kinaweza kuwa SAWA.
Tunajifunza kutoka kwenye mafunzo makini ya Mafundisho na Maagano neno “SAWA” linachomaanisha:
“Na siku ile, wakati nitakapokuja katika utukufu wangu, ndipo mfano utakapotimia ambao nilisema juu ya wanawali kumi.
Kwani wale walio na hekima na kupokea ukweli, na kumchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao, na hawajadanganyika—amini ninawaambia, hawatakatiliwa chini na kutupwa katika moto, bali watastahimili siku ile.”7
Yesu Kristo hufanya iwezekane kwa ajili yetu “kustahimilli siku.” Kustahimili siku haimaanishi kuongezea kwenye orodha inayoongezeka ya vitu vya kufanya. Fikiria kuhusu lenzi ya kukuzia. Dhumuni lake hasa si tu kufanya vitu vionekane kuwa vikubwa. Pia inaweza kukusanya mwanga na kuufanya kuwa na nguvu zaidi. Tunahitaji tu, kufokasi juhudi zetu na kuwa wakusanyaji wa Nuru ya Yesu Kristo. Tunahitaji uzoefu mtakatifu zaidi na wa ufunuo.
Huko kaskazini magharibi Ya Israeli, kuna safu ya mlima wa kupendeza na mara nyingi unajulikana kama “mlima wa kijani kibichi.” Mlima Carmel8 ni wa kijani mwaka mzima kutokana na matone madogo ya umande kwa sehemu kubwa. Kulishwa hufanyika kila siku. Kama vile “umande wa Carmel,9 tunapotafuta kulisha nafsi zetu “vitu vinavyohusu utakatifu,”10 “vitu vidogo na rahisi,”11 shuhuda zetu na shuhuda za watoto wetu zitakuwa hai!
Sasa, unaweza kuwa unafikiria, “Lakini Dada Wright, hauijui familia yangu. Sisi tunahangaika kweli na wala hatuko hivi.” Uko sahihi. Mimi siijui familia yako. Lakini Mungu kwa upendo usio na kikomo, rehema, nguvu, maarifa na utukufu anaijua.
Maswali unayoweza kuwa unauliza ni maswali ya moyo ambao unauma katika kina cha nafsi yako. Maswali kama hayo yanapatikana katika maandiko matakatifu:
“Mwalimu, si kitu kwako kuwa [familia yangu] tunaangamia?”12
“Tumaini langu li wapi?”13
“[Nifanye] nini, ili hili wingu la giza liweze kuondolewa kwamba lisinifunike [mimi]?”14
“Bali hekima itapatikana wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi?”15
“Inawezekanaje kwamba [mimi] nishikilie kila kitu kizuri?”16
“Bwana, ungetaka nifanye nini?”17
Na kisha kwa uzuri sana yaja majibu:
“Je, unaziamini nguvu za wokovu za Kristo?”18
“Je, Bwana amewaamuru wowote wasipokee wema wake?”19
“Mnaamini kwamba [Yeye] anaweza kufanya hili?”20
“Je! unawaamini manabii?”21
“Je, mnaweka imani yenu ya ukombozi kwa yule aliyewaumba?”22
“Je, mhukumu ulimwengu wote atakosa kutenda haki?”23
Rafiki zangu wapendwa, sisi hatuwezi kugawa mafuta yetu, lakini tunaweza kushiriki nuru Yake. Mafuta katika taa zetu hayatatusaidia tu “kustahimili siku” bali yanaweza pia kuwa njia ya kuangaza njia ambayo inawaongoza wale tunaowapenda hadi kwa Mwokozi, ambaye anasimama tayari “kwa mikono wazi kuwapokea” wao.24
“Bwana asema hivi; Zuia sauti yako, usilie, na macho yako yasitoke machozi; Maana kazi yako itapata thawabu, … nao watakuja tena kutoka nchi ya adui.
“Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema Bwana; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.”25
Yesu Kristo ndiye “tumaini kwa siku zako za mwisho.” Hakuna chochote tulichonacho, au tusichonacho, kilicho mbali na mfiko Wake usio na mwisho na dhabihu Yake ya milele. Yeye ndiye sababu ya kwa nini kamwe si mwisho wa hadithi yetu.26 Kwa hivyo sisi, “lazima tusonge mbele tukiwa na imani imara katika Kristo, tukiwa na mngʼaro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote. Kwa hivyo, kama [sisi] tutasonga mbele, tukila na kusherekea neno la Kristo, na tuvumilie hadi mwisho, tazama, hivi ndivyo asema Baba: [Sisi] tutapokea uzima wa milele.”27
Uzima wa milele ni shangwe ya milele. Shangwe katika maisha haya, sasa hivi—si kwa sababu ya changamoto za siku yetu bali kwa sababu ya msaada wa Bwana ili kujifunza kutoka kwazo na hatimaye kuzishinda—na shangwe isiyo na kifani katika maisha yajayo. Machozi yatakauka, mioyo iliyovunjika itaponywa, kile kilichopotea kitapatikana, wasiwasi utaondolewa, familia zitarejeshwa tena na vyote vile Baba aliavyonavyo vitakuwa vyetu.28
Mtegemee Yesu Kristo na uishi29 ndiyo ushuhuda wangu katika jina lililotukuzwa na takatifu la mpendwa “Mchungaji na Askofu wa nafsi [zetu],”30 Yesu Kristo, amina.