Mkutano Mkuu
Akina Kaka na Akina Dada katika Kristo
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Akina Kaka na Akina Dada katika Kristo

Na tufurahie zaidi uhusiano wetu wa kindugu wa kiroho ambao upo kati yetu na kuthamini sifa tofauti na vipaji tofauti sote tulivyonavyo.

Marafiki zangu wapendwa, tumekuwa na vikao vya mkutano wa kupendeza leo. Sote tumemsikia Roho wa Bwana na upendo Wake kupitia jumbe za kupendeza zilizotolewa na viongozi wetu. Ninahisi heshima kubwa kusema nanyi jioni hii kama msemaji wa mwisho wa kikao hiki. Ninaomba kwamba Roho wa Bwana aendelee kuwa nasi tunapofurahia kwa pamoja kama akina kaka na akina dada wa kweli katika Kristo.

Nabii wetu mpendwa, Russell M. Nelson, ametamka: “Ninawaomba waumini wetu kila mahali kuongoza katika kuachana na mitazamo na matendo ya kibaguzi. Ninawasihi kuhamasisha heshima kwa ajili ya watoto wote wa Mungu.”1 Kama Kanisa la ulimwenguni kote na linalokua, kufuata mwaliko huu kutoka kwa nabii wetu ni sharti la awali lililo muhimu kwa ajili ya ujenzi wa ufalme wa Mwokozi katika kila taifa la ulimwengu.

Injili ya Yesu Kristo inafundisha kwamba sisi sote tu wana na mabinti wa kiroho wa wazazi wa mbinguni ambao hakika wanatupenda2 na kwamba tuliishi kama familia katika uwepo wa Mungu kabla ya kuzaliwa katika dunia hii. Injili pia inafundisha kwamba sote tuliumbwa katika sura na mfano wa Mungu.3 Kwa hiyo, sisi sote ni sawa mbele Zake,4 kwani Yeye “ametufanya kwa damu moja mataifa yote ya wanaume [na wanawake].”5 Kwa hiyo, sisi sote tunayo asili ya kiungu, urithi, na uwezekano wa kuwa, kwani kuna “Mungu mmoja na Baba wa wote, aliye juu ya vyote, na kupitia vyote, na katika [sisi] sote.”6

Kama wafuasi wa Kristo, tunaalikwa kuongeza imani yetu na upendo kwa akina kaka- na dada zetu wa kiroho kwa dhati kuifuma mioyo yetu pamoja katika umoja na upendo, bila kujali tofauti zetu, hivyo kuongeza uwezo wetu wa kukuza heshima kwa ajili ya utu wa wana na mabinti wote wa Mungu.7

Je, hiyo haikuwa hali halisi ambayo watu wa Nefi waliipitia kwa takribani karne mbili baada ya Kristo kuwahudumia wao?

“Na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu. …

“Wala hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu.

“Na jinsi gani walibarikiwa!”8

Rais Nelson amezidi kuhimiza umuhimu wa kusambaza utu na heshima kwa wanadamu wenzetu alipoeleza: “Muumba wetu sisi sote anamwalika kila mmoja wetu kuachana na mitazamo ya kibaguzi dhidi ya kikundi chochote cha watoto wa Mungu. Yeyote kati yetu ambaye ana chuki dhidi ya mbari nyingine anahitaji kutubu! … Inampasa kila mmoja wetu kufanya lolote tuwezalo katika mazingira yetu ya ushawishi kulinda utu na heshima ambayo kila mwana na binti wa Mungu anaistahili.”9 Kwa hakika, utu wa mwanadamu unapaswa kutangulia heshima ya tofauti zetu.10

Kwa kuzingatia muunganiko wetu mtakatifu ambao unatuunganisha sisi na Mungu kama watoto Wake, maelekezo haya ya kinabii yaliyotolewa na Rais Nelson pasipo shaka ni hatua ya msingi kuelekea kujenga madaraja ya uelewa kuliko kutengeneza kuta za ubaguzi na mgawanyiko miongoni mwetu.11 Hata hivyo, kama Paulo alivyowaonya Waefeso, ni lazima tutambue kwamba ili kufikia dhumuni hili, tutahitajika kuonyesha bidii ya pamoja na binafsi ili tutende kwa unyenyekevu, upole na kwa kuvumiliana.12

Kuna hadithi ya mwalimu mmoja wa Kiyahudi ambaye alikuwa akifurahia kuchomoza kwa jua pamoja na rafiki zake wawili. Aliwauliza, “Je, mnajuaje kuwa usiku umekwisha, na siku mpya imeanza?”

Mmoja wao alijibu, “Unapokuwa unaweza kutazama upande wa mashariki na kuweza kumtofautisha kondoo na mbuzi.”

Yule mwingine kisha akajibu, “Unapoweza kutazama angani na kutofautisha mti wa mzeituni na mti wa mtini.”

Wao kisha wakamgeukia yule mwalimu mwenye busara na wakamwuliza swali lile lile. Baada ya tafakuri ndefu, akajibu, “Unapoweza kutazama upande wa mashariki na kuona uso wa mwanamke au uso wa mwanamume na kuweza kusema, ‘huyu ni dada yangu; huyu ni kaka yangu.’”13

Wapendwa marafiki zangu, ninaweza kuwahakikishia kwamba nuru ya siku mpya inaangaza kwa uangavu zaidi katika maisha yetu tunapowaona na kuwatendea wanadamu wenzetu kwa heshima na utu na kama kaka na dada zetu katika Kristo.

Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu alionyesha mfano wa kanuni hii kwa ukamilifu pale “alipoenda huko na huko akitenda kazi njema”14 kwa watu wote, akiwaalika waje Kwake na kushiriki mema Yake, bila kujali asili yao, daraja lao kijamii au tabia za kitamaduni. Yeye alihudumu, aliponya na daima alikuwa msikivu kwa hitaji la kila mtu, hususani wale ambao wakati huo walifikiriwa kuwa tofauti, walipuuzwa au kutengwa. Yeye hakumkataa yeyote bali aliwatendea wote kwa usawa na kwa upendo, kwani Yeye aliwaona kama kaka na dada Zake, wana na mabinti wa Baba mmoja.15

Moja ya matukio yaliyoshangaza sana wakati hili lilipotokea ni wakati Mwokozi aliposafiri kwenda Galilaya, kwa makusudi akipita njia ambayo ilipitia Samaria.16 Yesu kisha akaamua kukaa pembeni ya kisima cha Yakobo ili kupumzika. Akiwa hapo, mwanamke Msamaria akaja ili kujaza mtungi wake kwa maji. Kwa kujua yote, Yesu alimwita, akisema,”Nipe maji ninywe.”17

Mwanamke huyu alishangazwa kwamba Myahudi amemwomba mwanamke Msamaria msaada na akaeleza mshangao wake, akisema, “Imekuwaje, wewe Myahudi, kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.”18

Lakini Yesu, akiweka pembeni desturi za muda mrefu za uadui kati ya Wasamaria na Wayahudi, kwa upendo alimhudumia mwanamke huyu, akimsaidia kuelewa Yeye hakika alikuwa nani—kwamba ni, Masiya, ambaye angemwambia mambo yote na ambaye alikuwa akingojea kuja kwake.19 Matokeo ya huduma ile ya upendo ilisababisha yule mwanamke kukimbia mjini kuwatangazia watu kile kilichomtokea, akisema, Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo?”20

Nina huruma zaidi kwa wale ambao wametendewa vibaya, wamepuuzwa au kuteswa na watu wenye ubaguzi na wasiojali, kwa sababu, katika safari ya maisha yangu, nimeona kwa macho yangu maumivu ambayo watu wema wameteseka kutokana na kuhukumiwa au kufukuzwa kwa sababu wamezungumza, wameonekana au kuishi tofauti. Ninahisi huzuni ya dhati moyoni mwangu kwa ajili ya wale ambao mawazo yao yamebakia gizani, na mioyo yao imebaki kuwa migumu kwa kuamini katika uduni wa wale ambao ni tofauti na wao. Mtazamo wao finyu juu ya wengine kwa hakika unazuia uwezo wao wa kuwaona wao ni kina nani kama watoto wa Mungu.

Kama ilivyotabiriwa na manabii, tunaishi katika siku za hatari zinazoelekea kwenye Ujio wa Pili wa Mwokozi.21 Ulimwengu kwa ujumla umepoa kwa migawanyiko mikubwa, ikizidishwa na ubaguzi wa rangi, siasa na maswala ya uchumi na jamii. Migawanyiko hiyo wakati mwingine huishia kushawishi njia za kufikiri za watu na kutenda kulingana na wanadamu wenzao. Kwa sababu hii, si jambo la kushangaza kuona watu wakizungumzia jinsi ya kufikiri, kutenda, na kuzungumza kwa tamaduni zingine, mbari na mila kama vitu duni, wakitumia mawazo na makosa ya kufikirika na mara nyingi ni mawazo ya kejeli, yakizalisha mitazamo ya dharau, ubaguzi, kutoheshimu na hata chuki dhidi yao. Mitazamo ya jinsi hii inayo mizizi yake katika kiburi, majivuno, husuda na wivu, tabia za mwili wa asili,22 ambazo ni kinyume kabisa na tabia kama za Kristo. Tabia hii si sahihi kwa wale wanaojitahidi kuwa wafuasi Wake wa kweli.23 Hakika, wapendwa akina kaka na dada zangu, hakuna nafasi kwa ajili ya mawazo au matendo ya kibaguzi katika jumuiya zetu za Watakatifu.

Kama wana na mabinti wa agano tunaweza kusaidia kumaliza aina hii ya tabia kwa kutazama tofauti zinazoonekana ambazo ziko kati yetu kwa macho ya Mwokozi24 na kulingana na kile tulichonacho sisi sote—utambulisho wetu wa kiungu na uhusiano wa kindugu. Zaidi ya hayo, tunaweza kujitahidi kujiona sisi wenyewe katika ndoto, matumaini, huzuni na maumivu ya majirani zetu. Sisi sote tu wasafiri kama watoto wa Mungu, tukiwa sawa katika hali yetu isiyo kamilifu na katika uwezo wetu wa kukua. Tunaalikwa kutembea pamoja, kwa amani, mioyo yetu ikijawa upendo kwa Mungu na wanadamu wote—au, kama vile Abraham Lincoln alivyosema, “bila kinyongo kwa yeyote;na hisani kwa wote.”25

Je, umewahi kutafakari jinsi gani kanuni ya kuheshimu utu wa mtu na usawa inavyoonyeshwa kupitia njia rahisi ya jinsi tunavyovaa katika nyumba ya Bwana? Sisi sote tunakuja hekaluni tukiwa wamoja katika dhumuni moja na tuliojawa na hamu ya kuwa safi na watakatifu katika uwepo Wake mtakatifu. Tukivalia mavazi meupe, sisi sote tunapokelewa na Bwana Mwenyewe kama watoto Wake wapendwa, wanaume na wanawake wa Mungu, watoto wa Kristo.26 Tuna haki ya kufanya ibada zile zile, kufanya maagano yale yale, tunaahidi kuishi maisha ya juu zaidi na matakatifu zaidi na kupokea ahadi zile zile za milele. Wamoja katika madhumuni, tunaonana kwa macho mapya, na katika umoja wetu, tunasherehekea tofauti zetu kama watoto wa kiungu wa Mungu.

Hivi karibuni nilisaidia kuwaongoza watu maarufu na maofisa wa serikali kuzuru Hekalu la Brasilia Brazil. Nilisimama kidogo katika eneo la kubadilisha nguo na makamu wa rais wa Brazil, na tukajadiliana juu ya nguo nyeupe ambazo kila mtu anavaa ndani ya hekalu. Nilimwelezea kwamba matumizi haya ya ulimwenguni kote ya nguo nyeupe ni ishara ya kwamba sisi sote tu sawa kwa Mungu na kwamba hekaluni utambulisho wetu sio makamu wa rais wa nchi au kiongozi wa kanisa bali utambulisho wetu wa milele kama wana wa Baba mpendwa wa Mbinguni.

Picha
Maporomoko ya Iguaçú.

Mto Iguaçú unatiririka kupitia Brazil ya kusini na kumwaga maji yake kwenye nyanda ambazo zinatengeneza mfumo wa maporomoko ya maji ujulikanao ulimwenguni kote kama Maporomoko ya Iguaçú—moja ya uumbaji wa Mungu ulio mzuri na wenye kupendeza zaidi duniani, ikichukuliwa kama moja ya maajabu saba ya ulimwengu. Kiasi hiki kikubwa sana cha maji kinatiririkia kwenye mto mmoja tu na kisha yanagawanyika, yakitengeneza mamia ya maporomoko ya kipekee. Nikiongea kiistiari, mfumo huu wa ajabu wa maporomoko ya maji ni mfano wa familia ya Mungu duniani, kwani tunashiriki kiini na asili ya kiroho ile ile, inayotokana na urithi wetu wa kiungu na uhusiano wetu wa kindugu. Hata hivyo, kila mmoja wetu anatiririka katika utamaduni, kabila na mataifa tofauti kwa maoni, uzoefu na hisia tofauti. Licha ya hili, tunasonga mbele kama watoto wa Mungu na kama akina kaka na akina dada katika Kristo, bila kupoteza muunganiko wetu wa kiungu, ambao hutufanya tuwe watu wa kipekee na jumuiya ya wapendwa.27

Wapendwa akina kaka na dada zangu, na tuiweke mioyo na mawazo yetu sambamba na ufahamu na ushuhuda kwamba sisi sote ni sawa mbele za Mungu, kwamba sisi sote tumepewa endaumenti kamili pamoja na uwezekano na urithi wa milele. Na tufurahie zaidi uhusiano wetu wa kindugu wa kiroho ambao upo kati yetu na kuthamini sifa tofauti na vipaji tofauti sote tulivyonavyo. Kama tutafanya hivyo, ninaahidi kwamba tutatiririka katika njia zetu wenyewe, kama vile maji ya Maporomoko ya Iguaçú, bila kupoteza muunganiko wa kiungu ambao unatutambulisha kama watu wa kipekee, “watoto wa Kristo na warithi wa ufalme wa Mungu.”28

Ninawashuhudia kwamba tunapoendelea kutiririka kwa njia hii wakati wa maisha yetu duniani, siku mpya itaanza ambayo itayaangaza maisha yetu na kumulika fursa za kipekee za kuthamini zaidi, na kubarikiwa kwa ukamilifu zaidi kwa tofauti hizi zilizoumbwa na Mungu miongoni mwa watoto Wake.29 Hakika tutakuwa vyombo mikononi Mwake ili kuhamasisha heshima na utu miongoni mwa wana na mabinti Zake. Mungu yu hai. Yesu Kristo ni Mwokozi wa ulimwengu. Rais Nelson ni nabii wa Mungu katika siku yetu. Ninatoa ushahidi wa kweli hizi katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Chapisha