Mkutano Mkuu
Yesu Kristo ni Hazina
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


12:24

Yesu Kristo ni Hazina

Fokasi kwa Yesu Kristo. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu, “alama” ambayo kwake tunapaswa kuangalia, na ni hazina yetu kuu.

Mnamo1907 Mwingereza tajiri aliyeitwa George Herbert , Kabaila wa tano wa Carnarvon,1 alihamia Misri na kuvutiwa na mambo ya akiolojia. Alimfuata mtaalamu maarufu wa desturi za Kimisri, Howard Carter, na kupendekeza ubia. Carter angesimamia uchimbaji wa mabaki ya kale, na Carnarvon angetoa fedha.

Kwa pamoja, walifanikiwa kuchunguza maeneo mbalimbali. Kisha, walipokea kibali cha kuchimba katika Bonde la Wafalme, lililokuwa karibu na Luxor ya kisasa, ambapo makaburi mengi ya mafarao yalipatikana. Waliamua kulitafuta kaburi la Mfalme Tutankhamun. Tutankhamun alipanda juu ya kiti cha ufalme wa Misri zaidi ya miaka 3,000 iliyopita na kutawala kwa miaka 10 kabla ya kifo chake cha ghafla.2 Ilikuwa ikijulikana kwamba alikuwa amezikwa kwenye bonde la Wafalme,3 lakini lilipokuwa kaburi lake hapakujulikana.

Carter na Carnarvon walitumia miaka mitano bila mafanikio wakilitafuta kaburi la Tutankhamun. Hatimaye Carnarvon alimjulisha Carter kwamba alikuwa amechoshwa na juhudi zisizozaa matunda. Carter aliomba kupewa awamu moja zaidi ya kuchimba, na Carnarvon akalazimika kukubali na kuwa tayari kugharamia.

Carter aligundua kwamba ardhi yote ya bonde la Wafalme ilikuwa imechimbwa—isipokuwa lile eneo la kambi yao wenyewe Ndani ya siku chache za kuchimba pale, walipata vielelezo vya kwanza vyenye kuwaelekeza liliko kaburi.4

Hatimaye wakati Carter alipotazama kwenye chumba cha kaburi la Tutankhamun, aliona dhahabu kila mahali. Baada ya miezi mitatu ya kuweka katika makundi vitu vya kwenye kaburi, walifungua chumba kilichokuwa kimefungwa cha kaburi mnamo February 1923—miaka 100 iliyopita. Huu ulikuwa moja ya ugunduzi maarufu wa kiakiolojia wa karne ya 20.

Wakati wa ile miaka ya utafiti usiozaa matunda, Carter na Carnarvon hawakukitilia maanani kile ambacho kiuhalisia kilikuwa chini ya miguu yao. Takribani karne tano kabla ya kuzaliwa Mwokozi, Nabii Yakobo wa Kitabu cha Mormoni alirejelea kuhusu kuchukulia kwa urahisi au kutothamini kile ambacho kiko karibu kama “kuangalia kupita alama.” Yakobo aliona kwamba watu wa Yerusalemu hawangemtambua Masiya mwahidiwa wakati atakapokuja. Yakobo alitoa unabii kwamba wangekuwa “watu [ambao] wangeyadharau maneno yaliyo wazi … na [wangetafuta] mambo ambayo wao hawangeweza kuelewa. Kwa hivyo, kwa sababu ya upofu wao, upofu ambao [ungekuja] kutokana na kuangalia zaidi ya lengo, lazima waanguke.”5 Kwa maneno mengine, wangejikwaa.

Unabii wa Yakobo ulithibitisha hilo. Wakati wa huduma ya Yesu duniani, wengi waliangalia kupita alama zaidi ya kumwangalia Yeye. Waliangalia zaidi ya kumwona Mwokozi wa ulimwengu. Badala ya kutambua jukumu Lake katika kuukamilisha mpango wa Baba wa Mbinguni, walimshutumu na kumsulubisha. Walitafuta na kumsubiri mtu mwingine ili kuwaletea wokovu.

Kama vile watu wa Yerusalemu, na kama Carter na Carnarvon, nasi pia tunaweza kuwa waathirika wa kuangalia zaidi ya alama. Tunatakiwa kujilinda dhidi ya tabia hii tusije kumkosa Yesu Kristo katika maisha yetu na kushindwa kutambua baraka nyingi anazotupatia. Tunamuhitaji Yeye. Tunashauriwa kutegemea “kabisa kwenye ustahili wa yule aliye mkuu kuokoa.”6

Yeye ni alama yetu. Kama kimakosa tunafikiria kwamba kuna haja ya kitu fulani zaidi ya kile Yeyr anachokitoa, tunakana au kudharau uwezo na nguvu Yeye anazoweza kuwa nazo kwenye maisha yetu. Yeye amedai haki ya rehema na anaileta rehema hiyo kwetu.7 Yeye ni “chanzo [ambacho tunapaswa] kutegemea kwa ajili ya msamaha wa dhambi [zetu].”8 Yeye ni Mwombezi wetu kwa Baba na mshindi wa kile ambacho Baba amekitaka mara zote: kwa ajili yetu ili kurudi Kwake kama warithi katika ufalme Wake. Tunahitaji, katika maneno ya nabii Alma, “kuzungusha macho [yetu] na kuanza kuamini katika Mwana wa Mungu, kwamba atakuja kukomboa watu wake, na kwamba atateseka na kufa ili alipie dhambi zetu; na kwamba atafufuka tena kutoka kwa wafu, na kuleta ufufuko.”9 Yesu Kristo ni hazina yetu.

Mwokozi ametupa njia nyingi za kuweza kwa dhati kufokasi Kwake, ikijumuisha fursa ya kila siku ya kutubu. Wakati mwingine, hatuthamini jinsi gani baraka hii iliyotolewa ilivyo kuu. Nilipokuwa na miaka minane, nilibatizwa na baba yangu. Baadaye, nilishika mkono wake wakati tulipokuwa tukivuka barabara ya mtaa wenye shughuli nyingi. Nilikuwa siko makini na nilitembea kuvuka ukingo wakati lori kubwa lilipopita likitoa sauti kubwa. Baba yangu alinivuta kwa haraka na kunirudisha kwenye ukingo. Kama asingefanya hivyo ningegogwa na lori. Nikiijua hali yangu ya utundu, nilifikiria “Pengine ingekuwa bora zaidi kwangu kufa kwa kugongwa na gari kwa sababu kamwe sitakuwa msafi kama nilivyo sasa baada ya ubatizo wangu.”

Kama mwenye miaka minane, kimakosa nilidhania kwamba maji ya ubatizo yaliondoa dhambi. Si hivyo. Kwa miaka mingi tangu ubatizo wangu, nimejifunza kwamba dhambi huondolewa kwa nguvu ya Yesu Kristo kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi wakati tunapofanya na kushika agano la ubatizo.10 Kisha, kupitia zawadi ya toba, tunaweza kubakia wasafi. Pia nimejifunza kwamba sakramenti huleta mzunguko mtakatifu wenye nguvu katika maisha yetu, ukituwezesha kuendelea kubakia na msamaha wa dhambi zetu.11

Kama vile hazina iliyokuwa chini ya miguu ya Carter na Carnarvon, hazina za baraka ya sakramenti zinapatikana kwetu kila mara tunapohudhuria mkutano wa sakramenti. Tunaahidiwa kwamba Roho Mtakatifu atakuwa mwenza wetu wa daima ikiwa tutaiendea sakramenti kwa njia sawa na ile ambayo mwongofu mpya anauendea ubatizo na uthibitisho, kwa moyo uliovunjika na roho iliyopondeka, na ari ya kuishi agano la ubatizo. Roho Mtakatifu hutubariki kupitia nguvu Yake ya utakaso ili kwamba daima tubakie na msamaha wa dhambi zetu, mwanzoni hadi mwishoni mwa wiki.12

Msingi wetu wa kiroho huimarishwa kupitia toba, na kwa nia ya dhati kujiandaa kwa ajili ya na kwa ustahiki kushiriki sakramenti. Ni kupitia tu msingi wetu imara wa kiroho tunaweza kustahimili mvua, upepo na mafuriko ya kisitiari ambayo hutukabili maishani mwetu.13 Kinyume chake, msingi wetu wa kiroho hudhoofishwa wakati kwa hiari tupoacha kuhudhuria mkutano wa sakramenti au wakati tunapokuwa hatufokasi kwa Mwokozi wakati wa sakramenti. Tunaweza bila kukusudia “kujiondoa [wenyewe] kutoka kwa Roho wa Bwana, kwamba asiwe na nafasi ndani [yetu] ili [kutuongoza] katika njia za hekima ili [tuweze] kubarikiwa, kustawi na kulindwa.”14

Wakati Roho Mtakatifu anapokuwa pamoja nasi, tutapata msukumo na kuongozwa kufanya na kushika maagano mengine kama yale ya hekaluni. Kwa kufanya hivyo uhusiano wetu na Mungu huwa wa kina.15 Unaweza kuona kwamba mahekalu mengi mapya yametangazwa miaka ya hivi karibuni, ili kuleta mahekalu karibu zaidi na waumini.16 Kwa njia ya fumbo, kadiri mahekalu yanavyoweza kufikika zaidi, inaweza kuwa rahisi kwetu kutotilia maanani sana kuhudhuria hekaluni. Wakati mahekalu yanapokuwa mbali, tunapanga muda na rasilimali zetu ili kusafiri kwenda hekaluni kuabudu. Tunazipa kipaumbele safari hizi.

Kwa hekalu kuwa karibu zaidi, inaweza kuwa rahisi kuacha vitu vidogo vidogo kuingilia uhudhuriaji, tukijiambia, “Sawa, nitaenda siku nyingine.” Kuishi karibu na hekalu kunafanya iwe rahisi kwenye kupanga muda wa kuwa hekaluni, lakini urahisi huo unaweza kufanya iwe rahisi kutolitilia maanani hekalu. Tufanyapo hivyo “tunaikosa ile alama,” tunashusha hadhi ya fursa ya kusonga karibu na Mwokozi kwenye nyumba Yake takatifu. Ari yetu ya kuhudhuria lazima angalau iwe ya nguvu wakati hekalu likiwa karibu au wakati likiwa mbali.

Baada ya Carter na Carnarvon kuchimba pengine katika bonde la Wafalme wakilitafuta kaburi la Tutankhamun, waligundua kwamba walikuwa wamekosea. Hatuhitaji kufanya kazi bila mafanikio, kama ilivyokuwa kwao kwa muda, ili kupata hazina. Na hata hatuhitaji kutafuta ushauri kutoka vyanzo vya nchi za mbali, tukitafuta kwa bidii uthamani wa chanzo tukidhania kwamba ushauri huo utakuwa elekezi zaidi kuliko ule ambao tunaweza kuupokea kutoka kwa nabii wa Mungu aliye mnyenyekevu.

Kama ilivyoandikwa kwenye Agano la Kale, wakati Naamani alipotafuta uponyaji wa ukoma wake, alikasirika alipoambiwa kujichovya mara saba kwenye mto wa kawaida uliyo karibu. Lakini alishawishiwa kufuata ushauri wa nabii Elisha, kuliko kutegemea dhana zake mwenyewe za jinsi miujiza inavyotakiwa kufanyika. Kama matokeo, Naamani aliponywa.17 Wakati tunapomuamini nabii wa Mungu hapa duniani leo na kutenda kulingana na ushauri wake, tutapata furaha, nasi pia tutaponywa. Hatuhitaji kuangalia mbali zaidi.

Akina kaka na akina dada, ninawahimiza mkumbuke na daima kufokasi katika injili ya Yesu Kristo. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu, “alama” ambayo kwake tunapaswa kuangalia, na ni hazina yetu kuu. Wakati unapokuja Kwake, utatunukiwa nguvu ili kukabiliana na changamoto za maisha, ujasiri wa kutenda mema na uwezo wa kutimiza misheni yako kwenye maisha haya. Thamini fursa ya kutubu, fursa ya kushiriki sakramenti, baraka za kufanya na kushika maagano ya hekaluni, shangwe ya kuabudu hekaluni na shangwe ya kuwa na nabii aliye hai.

Mimi natoa ushahidi wangu wa dhati na hakika kwamba Mungu, Baba wa Milele, ndiye Baba yetu wa Mbinguni na kwamba Yeye yu hai; Yesu ndiye Kristo; Yeye ni rafiki yetu wa mbinguni mkarimu, mwenye hekima,18 na hili ni Kanisa Lake lililorejeshwa. Asanteni kwa imani na uaminifu wenu. Ninaomba kwamba mbarikiwe, mstawi na mlindwe, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Jina kamili la Kabaila wa tano wa Carnarvon ni George Edward Stanhope Molyneux Herbert.

  2. Kipimo cha CT scan kilichofanyika mnamo 2005 kinaonyesha kwamba Mfalme Tutankhamun yaweza kuwa alipatwa na mivunjiko kadhaa ya moja ya mifupa ya miguu yake, huenda hicho kilichosababisha maambukizo na kifo.

  3. Wengi wa mafarao wa Ufalme Mpya wa Misri walizikwa katika Bonde la Wafalme. Mengi ya makaburi hayo yalipatikana na vidani vyake kuibiwa.

  4. Simulizi hii ya ugunduzi wa kaburi la Tutankhamun kimsingi unatokana na Eric H. Cline, “King Tut’s Tomb,” Archaeology: An Introduction to the World’s Greatest Sites (2016), 60–66.

    Sababu kadhaa zilichangia kwenye chaguzi za Carter na Carnarvon za wapi kuchimba—na wapi pasichimbwe—katika Bonde la Wafalme. Eneo karibu na kambi halikuwa likishawishi kuchimbwa moja kwa moja. Eneo la pembe tatu liliruhusu wageni kuelekea kaburi la Ramses wa VI, hivyo uchimbaji wa eneo hilo ungevuruga mambo. Eneo lilifunikwa na, kwa maneno ya Carter, “nyumba za nyasi zilizojengwa hovyo, huenda zilitumiwa na wafanyakazi katika kaburi la Rameses [,] … [na] udongo wa futi tatu ambao uliwekwa chini yao.” Haikuonekana kama nyumba hizo za nyasi zingejengwa juu ya njia ya kuingia kwenye kaburi (ona Howard Carter and A. C. Mace, The Tomb of Tut-ankh-Amen: Discovered by the Late Earl of Carnarvon and Howard Carter, vol. 1 [1923], 124–28, 132).

    Kwa ajili ya maelezo mengine ya ugunduzi wa kaburi la Tutankhamun, ona Zahi Hawass, Tutankhamun and the Golden Age of the Pharaohs (2005); Nicholas Reeves, The Complete Tutankhamun: The King, the Tomb, the Royal Treasure (1990), 80–83; and Nicholas Reeves and Richard H. Wilkinson, The Complete Valley of the Kings: Tombs and Treasures of Ancient Egypt’s Royal Burial Site (1996), 81–82.

  5. Yakobo 4:14.

  6. 2 Nefi 31:19.

  7. Ona Moroni 7:27–28.

  8. 2 Nefi 25:26.

  9. Alma 33:22.

  10. Ona Mafundisho na Maagano 76:52.

  11. Ona David A. Bednar, “Fundisha Kujenga Imani katika Yesu Kristo” (hotuba iliyotolewa kwenye mafunzo ya viongozi wapya wa misheni, Juni 23, 2023); Rachel Sterzer Gibson, “Teach to Build Faith in Jesus Christ, Elder Bednar Instructs,” Church News, June 23, 2023, thechurchnews.com.

  12. Sakramenti ilikuwa, hata hivyo, sio kutolewa kama maana fulani ya kulinda ondoleo la dhambi zetu (see James E. Talmage, The Articles of Faith, 12th ed. [1924], 175). Mtu hawezi kutenda dhambi kwa makusudi Jumamosi jioni na kutarajia kwamba yote anayopaswa kufanya ni kula kipande cha mkate na kunywa kikombe cha maji Jumapili na kutakaswa kimiujiza. Lakini matokeo ya utakaso ya Roho Mtakatifu yanaweza kuwatakasa wote wanaotubu kwa moyo wa dhati na kusudi halisi.

  13. Ona 3 Nefi 18:12–13.

  14. Mosiah 2:36.

  15. Rais Nelson alisema: “Mungu anao upendo maalumu kwa kila mtu anayefanya Naye maagano katika maji ya ubatizo. Na upendo huo wa kiungu huongezeka kadiri maagano ya ziada yanapofanywa na kushikwa kwa uaminifu” (“Choices for Eternity” [worldwide devotional for young adults, May 15, 2022], Gospel Library). Maagano mengi katika njia ya agano sio tu yako katika mpangilio lakini ni ya nyongeza na jumuishi. Yanachochea muungano wa karibu na imara pamoja na Mungu. Muungano huo huturuhusu kubadilishwa kwa kiwango kwamba taswira Yake inakuwa kwenye nyuso zetu na mioyo yetu kwa dhati na daima hubadilishwa (ona Alma 5:14).

  16. Rais Nelson alifafanua kwamba Bwana “anafanya mahekalu Yake yafikike kwa karibu zaidi. Anaongeza kasi ya sisi kujenga mahekalu. Anaongeza uwezo wetu wa kusaidia kukusanya Israeli. Anafanya iwe rahisi pia kwa kila mmoja wetu kutakaswa kiroho.” (“Fokasi kwenye Hekalu,” Liahona, Nov. 2022, 121).

  17. Ona 2 Wafalme 5:9–14.

  18. Ona “Najua Yesu Yu Hai,” Nyimbo za Kanisa, na. 136.