Mkutano Mkuu
Nguvu ya Yesu Kristo Katika Maisha Yetu Kila Siku
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


10:17

Nguvu ya Yesu Kristo Katika Maisha Yetu Kila Siku

Chanzo cha nguvu yetu ni imani katika Yesu Kristo tunapotafuta kwa kukusudia kuja Kwake kila siku.

Wapendwa akina kaka na akina dada, hili ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni shangwe iliyoje kukusanyika kama Kanisa Lake. Ninashukuru kwamba Rais Russell M. Nelson ametukumbusha kutumia jina sahihi la Kanisa la Bwana mara zote ili kwamba tukumbuke hili ni Kanisa la nani na ni mafundisho ya nani tunayafuata.

Rais Nelson amesema: “Katika siku zijazo, tutaona maonyesho makubwa zaidi ya nguvu za Mwokozi ambayo ulimwengu kamwe haujapata kuona. Atarejesha fursa zisizo na idadi, baraka na miujiza kwa walio waaminifu.”1

Mojawapo ya fursa kubwa kwangu mimi na mke wangu, Renee, ni kukutana na Watakatifu sehemu ambayo tunatumikia. Tunasikia hadithi zao, tunashuhudia hasara zao, tunashiriki majonzi yao na tunafurahia kwenye mafanikio yao. Tumeshuhudia nyingi ya baraka na miujiza ambayo Bwana alitoa kwa watakatifu. Tumekutana na watu ambao wamepitia yasiyowezekana, ambao wameteseka makubwa sana.

Rais José Batalla na mke wake, Dada Valeria Batalla.
Flavia Cruzado na baba yake.

Tumeona dhihirisho la nguvu ya Mwokozi kwa mjane ambaye alipoteza mume wakati walipokuwa kwenye kazi ya Bwana huko Bolivia.2 Tumeliona kwa msichana huko Ajentina ambaye alisukumwa na kudondokea uvunguni mwa treni na kupoteza mguu wake, kwa sababu tu mtu fulani alitaka kuiba simu yake.3 Na kwa baba yake mgane, ambaye sasa lazima aiboreshe hali na kumuimarisha binti yake baada ya tukio la kikatili lisiloelezeka. Tumeliona kwenye familia ambazo zilipoteza makazi yao na kila mali yao wakati wa moto huko Chile siku mbili baada ya Krismasi ya mwaka 2022.4 Tumeliona kwa wale ambao wanapata shida baada ya talaka iletayo mshituko na kwa wale ambao hawana hatia wanaoathiriwa na unyanyasaji.

Moto huko Chile.

Je, ni nini huwapa nguvu ya kuvuka mambo magumu? Je, ni nini huwapa tabaka la ziada la nguvu za kuendelea wakati kila kitu kinapoonekana kupotea?

Nimekuja kugundua kwamba chanzo cha nguvu hiyo ni imani katika Yesu Kristo tunapokuwa kwa makusudi tunatafuta kwenda Kwake kila siku.

Nabii Yakobo alifundisha, “Na anakuja ulimwenguni ili apate kuwaokoa wanadamu wote kama watakubali sauti yake; kwani tazama, anapokea maumivu ya wanadamu wote, ndiyo, maumivu ya kila kiumbe kinachoishi, waume kwa wake, na watoto, ambao ni wa familia ya Adamu.”5

Wakati mwingine, kuwa na imani katika Yesu Kristo kunaweza kuonekana kama jambo lisilowezekana, kama lisiloweza kupatikana. Tunaweza kudhani kwamba kuja kwa Kristo kunahitaji nguvu, uwezo na utimilifu ambao hatuna, na hatuwezi tu kupata nguvu ya kufanya haya yote. Lakini jambo ambalo nimejifunza kutoka kwa watu hawa wote ni kwamba imani katika Yesu Kristo ndicho kitu ambacho kinatupa nguvu ya kuanza safari. Wakati mwingine tunaweza kudhani, “Nahitaji kurekebisha maisha yangu kabla sijaenda kwa Yesu,” lakini ukweli ni kwamba tunaweza kwenda kwa Kristo ili kurekebisha maisha yetu kupitia Yeye.

Hatuendi kwa Yesu kwa sababu sisi tu wakamilifu. Tunaenda Kwake kwa sababu hatuna ukamilifu na kupitia Yeye tunaweza “kukamilishwa.”6

Je, tunaanzaje kutumia kiasi kidogo cha imani kila siku? Kwangu mimi huanzia asubuhi: Niamkapo, badala ya kuperuzi kwenye simu yangu, ninasema sala. Hata kama ni sala ya kawaida. Kisha ninasoma maandiko. Hii hunisadia kwenye maagano yangu ya kila wiki ambayo nayafanya wakati ninaposhiriki sakramenti ili “daima nimkumbuke Yeye.”7 Wakati ninapoianza siku yangu kwa sala na maandiko, “ninaweza kumkumbuka Yeye” wakati ninapoperuzi kwenye simu yangu. Ninaweza “kumkumbuka Yeye” ninapokumbana na matatizo na migogoro na najaribu kukabiliana nayo kama ambavyo Yesu angefanya.

Wakati “ninapomkumbuka Yeye.” ninahisi hamu ya kubadilika, kutubu. Ninapata chanzo cha nguvu ya kushika maagano yangu, na nahisi ushawishi wa Roho Mtakatifu maishani mwangu “na kutii amri zake ambazo [amenipa]; ili daima [niweze] kuwa na Roho wake.”8 Inanisadia kuvumilia mpaka mwisho.9 Au angalau mpaka mwisho wa siku! Na katika siku hizo ambazo ninashindwa kumkumbuka Yeye siku nzima, Yeye bado yupo, akinipenda na kuniambia Ni SAWA, unaweza kujaribu tena kesho.

Ingawa sisi si wakamilifu katika kumkumbuka Yeye, Baba yetu mpendwa wa Mbinguni kamwe haachi kutukumbuka.

Moja kati ya makosa ambayo mara nyingi tunafanya ni kudhani kwamba kushika maagano, au ahadi tulizoweka na Mungu, ni kama muamala ambao tunafanya Naye: Ninatii, na ananilinda dhidi ya kitu chochote kibaya kilichowahi kunitokea. Ninalipa zaka, na kamwe sitapoteza kazi yangu au moto hautaunguza nyumba yangu. Lakini pale vitu vinapoenda tusivyotarajia, tunalia kwa Bwana “Je hujali kwamba mimi ninaangamia?”10

Maagano yetu si ya kimuamala; ni ya kutubadilisha.11 Kupitia maagano ninapokea utakaswaji, nguvu na uwezo wa Yesu Kristo, ambao unaniruhusu niwe mtu mpya, kusamehe kile ambacho kinaonekana kutosameheka, kushinda kisichowezekana. Kwa kukusudia tukimkumkumbuka Yesu Kristo daima kunaleta nguvu; hunipa uwezo wa “kutii amri zake ambazo [amenipa].”12 Hunisaidia niwe bora zaidi, nitabasamu bila sababu yoyote, niwe mpatanishi,13 niepuke mabishano na nimwache Mungu ashinde maishani mwangu.14

Wakati maumivu yetu au ya mwingine ambaye tunampenda ni ya kina sana kwamba hatuwezi kuvumilia, kumkumbuka Yesu Kristo na kuja Kwake kunaweza kurahisisha mzigo, kulainisha mioyo na kupunguza maumivu. Hii ndiyo nguvu ambayo ilimwezesha baba kupita uwezo wake wa kawaida kumsaidia bintiye katika maumivu ya kimwili na kihisia ya kupoteza mguu wake.

Flavia Cruzado na Mzee Ulisses Soares.

Wakati Mzee Soares alipotembelea Ajentina Juni iliyopita na kumuuliza Flavia kuhusu ajali yake ya kushtua, kwa imani alijibu, “nilipitia hisia za mkanganyiko, uchungu, hasira na hata chuki wakati [hili lilipotokea]. Kitu ambacho kilinisaidia ilikuwa ni kutouliza, ‘kwa nini mimi?’ badala yake kuuliza ‘ni kwa ajili gani?’ Hiki kilikuwa kitu ambacho kilinisogeza karibu na wengine na kwa Bwana. … Badala ya kujiweka mbali Naye, ilinibidi Kumshikilia Yeye kwa nguvu.”15

Rais Nelson alifundisha: “Thawabu ya kushika maagano na Mungu ni nguvu ya kimbingu—nguvu ambayo inatuimarisha ili tuhimili majaribu, vishawishi na maumivu yetu ya moyo vyema zaidi. … Hivyo, washika maagano wanayo haki ya aina maalumu ya pumziko.”16 Hii ndiyo aina ya amani na pumziko niliyoiona kwenye macho ya mjane, licha ya maumivu ya moyo ya kumkosa mume wake kila siku.

Dhoruba kwenye Bahari ya Galilaya

Agano jipya linatuambia juu ya wakati ambapo Yesu na wanafunzi Wake walipokuwa kwenye meli:

“Punde palitokea dhoruba kuu na upepo, na mawimbi yakapiga chombo, hata kikaanza kujaa maji. …

“Naye alikuwa … amelala kwenye mto: wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu, si kitu kwako kwamba tunaangamia?

“Na yeye aliamka, na kuukemea upepo, na kuiambia bahari, Nyamaza, utulie. …

“Na akawaambia mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”17

Mara zote nimevutiwa na hadithi hii. Je, Bwana alitegemea watumie imani yao kutuliza upepo? Kukemea ule upepo? Imani katika Yesu Kristo ni hisia ya amani ya kuhimili dhoruba, tukijua kwamba hatutaangamia kwa sababu Yeye yuko chomboni pamoja nasi.

Hii ndiyo aina ya imani tuliyoiona wakati tulipozitembelea familia baada ya moto huko Chile. Nyumba zao zilikuwa zimeteketea kabisa kwa moto; walikuwa wamepoteza kila kitu. Hata hivyo tulikuwa tukitembea kwenye kile ambacho kilijulikana kama makazi yao na walikuwa wakituambia kuhusu uzoefu wao, tulihisi kuwa tulikuwa tukisimama kwenye ardhi takatifu. Mmoja wa akina dada alimwambia mke wangu, “Wakati nilipoona kwamba nyumba zilizo jirani zilikuwa zikiungua, nilipata msukumo kwamba nyumba yetu itaungua, kwamba tutapoteza kila kitu. Badala ya kukatishwa tamaa, nilihisi hali ya amani isiyoelezeka. Kwa kiasi fulani, nilihisi kila kitu kingekuwa SAWA.” Kumtumaini Mungu na kushika maagano yetu na Yeye huleta nguvu kwenye udhaifu wetu na faraja kwenye huzuni zetu.

Ninashukuru kwa fursa ambayo mimi na Renee tulikuwa nayo ya kukutana na baadhi ya Watakatifu hawa, kwa mifano yao mingi ya imani, nguvu na uvumilivu. Hadithi zenye kuumiza moyo na kukatisha tamaa ambazo pengine kamwe hayatawekwa kwenye kurasa za mbele za magazeti au kuwafikia wengi kwa muda mfupi. Kwa picha ambazo hazikupigwa machozi yakitiririka na sala zikitolewa baada ya hasara au talaka iliyosababisha mshituko, na kwa machapisho ambayo kamwe hayatengenezwi na hisia ya woga na huzuni na maumivu ambayo huvumilika kupitia imani yao katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake. Watu hawa wanaimarisha imani yangu, na kwa hilo nina shukrani za dhati.

Ninajua kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo. Ninajua kwamba Yeye anasimama tayari kutuzawadia nguvu Zake, kama tutakuja Kwake kila siku. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.