Mkutano Mkuu
Zaka: Kufungua Madirisha ya Mbinguni
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


14:12

Zaka: Kufungua Madirisha ya Mbinguni

Madirisha ya mbinguni yanafunguka kwa njia nyingi. Tumaini katika wakati wa Bwana; baraka daima zinakuja.

Nikiwa Amerika Kusini hivi majuzi, Ndugu Roger Parra kutoka Venezuela alishiriki nami tukio lifuatalo:

“Mnamo mwaka 2019 Venezuela ilitikiswa na matatizo ambayo yalisababisha kukatika kwa umeme kwa siku tano.

“Machafuko na vurugu vilitawala mitaani, na watu wengi waliokata tamaa hawakuwa na chakula cha kutosha.

“Wengine walianza kupora biashara za vyakula, na kuharibu kila kitu kilichokuwa katika njia walizopita.

“Kama mmiliki wa kiwanda kidogo cha kuoka mikate, nilikuwa na wasiwasi sana kuhusu biashara yetu. Kama familia, tuliamua kuwagawia watu wenye uhitaji chakula chote kilichokuwa katika kiwanda chetu cha mikate.

“Katika usiku mmoja wenye giza nene ghasia zilikuwa kila mahali. Wasiwasi wangu pekee ulikuwa juu ya usalama wa mke wangu mpendwa na watoto.

“Kulipopambazuka nilienda kwenye kiwanda chetu cha mikate. Kwa huzuni, kila biashara ya chakula iliyokuwa jirani ilikuwa imeharibiwa na waporaji, lakini kwa mshangao mkubwa, kiwanda chetu hakikuharibiwa. Hakuna kitu kilichokuwa kimeharibiwa. Nilimshukuru Baba yangu wa Mbinguni kwa unyenyekevu.

“Nilipofika nyumbani, niliiambia familia yangu kuhusu baraka na ulinzi wa Mungu.

“Walikuwa na shukrani sana.

“Mwanangu mkubwa, Rogelio, mwenye miaka 12 tu, alisema, ‘Baba! Ninajua kwa nini duka letu lililindwa. Wewe na Mama daima mnalipa zaka zenu.’”

Ndugu Parra alihitimisha: “Maneno ya Malaki yalikuja akilini mwangu. ‘Kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu’ [Malaki 3:11]. Tulipiga magoti na kwa shukrani kumshukuru Baba yetu wa Mbinguni kwa muujiza Wake.”1

Familia ya Parra.

Mkanijaribu kwa Njia Hiyo

Yote tuliyonayo na jinsi tulivyo vinatoka kwa Mungu. Kama wafuasi wa Kristo, tunashiriki kwa hiari na wale wanaotuzunguka.

Pamoja na yote Bwana anayotupatia, ametuomba tumrudishie Yeye na ufalme wake duniani asilimia 10 ya ongezeko letu. Ametuahidi kwamba tunapokuwa waaminifu katika zaka zetu, Yeye “atafungua … madirisha ya mbinguni, na kumwaga … baraka, kwamba hapatakuwa na nafasi ya kutosha kuhifadhi.”2 Ametuahidi kwamba atatulinda dhidi ya maovu.3 Ahadi hizi ni za uhakika,4 Bwana anatamka, “Mkanijaribu kwa njia hiyo,”5 kirai ambacho hakipatikani mahali pengine popote katika maandiko isipokuwa pale unapomnukuu Malaki.

Madirisha ya mbinguni yanafunguka kwa njia nyingi. Baadhi ni za kimwili, lakini nyingi ni za kiroho. Baadhi ni ndogo na rahisi kupuuzwa. Tumainia katika wakati wa Bwana; baraka daima zinakuja.

Tunahuzunika pamoja na wale wanaohangaika kupata mahitaji ya maisha. Kanisa hivi karibuni limetoa dola za Marekani milioni 54 kusaidia watoto na akina mama walio katika mazingira magumu kote ulimwenguni.6 Na kwa matoleo yanayotokana na mfungo wako wa kila mwezi, maaskofu wetu wazuri husaidia maelfu kila wiki ambao wanahitaji chakula kwa muda kwenye meza zao, nguo miilini mwao na makazi juu ya vichwa vyao. Suluhisho pekee la kudumu la umaskini wa ulimwengu huu ni injili ya Yesu Kristo.7

Jambo la Imani

Mtume Paulo alionya kwamba hekima ya wanadamu inaelewa mambo ya wanadamu lakini ina ugumu wa kuelewa mambo ya Mungu.8 Ulimwengu unazungumza juu ya zaka kulingana na pesa zetu, lakini sheria takatifu ya zaka kimsingi ni suala la imani yetu. Kuwa waaminifu katika zaka zetu ni njia mojawapo tunayoonesha nia yetu ya kumweka Bwana kwanza katika maisha yetu, kupita wasiwasi na maslahi yetu wenyewe. Ninakuahidi kwamba kadiri unavyomtumaini Bwana, baraka za mbinguni zitafuata.

Yesu alisema tumpe “Kaisari yaliyo ya Kaisari; na kwa Mungu vitu vilivyo vyake.”9 Mwokozi aliyefufuka aliwaomba Wanefi waandike katika kumbukumbu zao ahadi Zake zinazopatikana katika Malaki.10 Katika siku zetu, Bwana alithibitisha tena sheria takatifu ya zaka, akitamka: “Huu utakuwa mwanzo wa zaka kwa watu wangu. Na [watalipa] sehemu ya kumi ya mapato yao yote kila mwaka; na hii itakuwa sheria ya kudumu kwao milele.”11

Bwana alielekeza kwa uwazi jinsi zaka inavyopaswa kutolewa, akisema, “Leteni zaka zote ghalani;”12 ikimaanisha kuleta zaka katika ufalme Wake uliorejeshwa, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.13 Aliagiza kwamba matumizi ya zaka hizi takatifu yangezingatiwa kwa sala na baraza la Urais wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, Uaskofu Simamizi, “na kwa sauti yangu kwao, asema Bwana.”14

Fedha Takatifu za Bwana

Fedha hizi takatifu si mali ya viongozi wa Kanisa. Ni mali ya Bwana. Watumishi wake wanajua kwa dhati asili takatifu ya usimamizi wao.

Rais Gordon B. Hinckley alisimulia tukio hili la utotoni: “Nilipokuwa mvulana nilimuuliza swali baba yangu … kuhusu matumizi ya fedha za Kanisa. Alinikumbusha kuwa wajibu wangu ni jukumu nililopewa na Mungu la kulipa zaka na matoleo yangu. Ninapofanya hivyo, [baba yangu alisema,] kile ninachotoa si changu tena. Ni mali ya Bwana ambayo ninaiweka wakfu kwake.” Baba yake aliongeza: “Kile ambacho mamlaka za Kanisa hukifanya na matoleo hayo hakihitaji kukusumbua [wewe, Gordon]. Wanawajibika kwa Bwana, ambaye atahitaji hesabu mikononi mwao.”15

Tunahisi uzito wa “kujibu kwa Bwana.”

Zaka na Matoleo Yako ya Ukarimu

Kutokana na zaka na matoleo ya ukarimu mliyoweka wakfu kwa Bwana, mwaka jana zaidi ya dola za Marekani bilioni moja zilitumika kuwabariki wale wenye shida.16

Katika jukumu letu kuu la kupeleka injili ya urejesho duniani kote, tuna zaidi ya wamisionari 71,000 wanaohudumu katika misheni 414.17 Kwa sababu ya zaka na matoleo yako, wamisionari, bila kujali hali za kifedha za familia zao, wanaweza kuhudumu.

Mahekalu yanajengwa kote ulimwenguni kwa idadi isiyo na kifani. Kwa sasa, mahekalu 177 yanafanya kazi, 59 kwa sasa yanajengwa au kukarabatiwa, na 79 zaidi yako katika mpango na usanifu.18 Zaka zako zinaruhusu baraka za hekalu kuwepo ambapo Bwana pekee angeweza kuona.

Kuna mikusanyiko zaidi ya 30,000 iliyo katika maelfu ya makanisa na majengo mengine katika nchi na himaya 195.19 Kwa sababu ya zaka zako za uaminifu, Kanisa linaanzishwa katika sehemu za mbali ambazo yamkini unaweza usizitembelee miongoni mwa Watakatifu waadilifu ambao pengine kamwe hutawajua.

Kwa sasa Kanisa linafadhili taasisi tano za elimu ya juu.20 Hizi zinahudumia zaidi ya wanafunzi 145,000. Madarasa laki moja na elfu kumi yanafundishwa kila wiki katika seminari na vyuo vyetu.21

Baraka hizi na nyingine nyingi huja kwa kiasi kikubwa kutokana na vijana na wazee wa kila hali ya kiuchumi ambao hulipa zaka ya uaminifu.

Nguvu ya kiroho ya sheria ya kiungu ya kulipa zaka haipimwi kwa kiasi cha pesa kinachochangwa, kwa kuwa matajiri na maskini wanaamriwa na Bwana kuchangia asilimia 10 ya mapato yao.22 Nguvu huja kwa kuweka tumaini letu kwa Bwana.23

Nyongeza ya neema ya Bwana inayotolewa kupitia zaka zako za ukarimu imeimarisha akiba ya Kanisa, na kutoa fursa za kuendeleza kazi ya Bwana zaidi ya kitu chochote ambacho tumekipitia. Yote yanajulikana na Bwana, na baada ya muda, tutaona malengo Yake yote matakatifu yakitimizwa.24

Baraka Huja katika Njia Nyingi

Baraka za zaka huja katika njia nyingi. Mnamo 1998 niliandamana na Mzee Henry B. Eyring hadi kwenye mkutano mkubwa wa Kanisa katika eneo la Utah ambalo sasa linajulikana kama Silicon Slopes, jumuiya ya uvumbuzi mkubwa kiteknolojia. Ulikuwa ni wakati wa ukuaji kimafanikio, na Mzee Eyring aliwaonya Watakatifu kuhusu kulinganisha kile walichokuwa nacho na cha wengine na kutaka zaidi. Nitakumbuka daima ahadi yake, kwamba kadiri walivyotoa zaka ya uaminifu, tamaa yao ya mali nyingi zaidi ingepungua. Ndani ya miaka miwili, povu la teknolojia lilitapakaa. Wengi walipoteza kazi zao, na makampuni yalikuwa taabani wakati huu wa marekebisho ya kifedha. Wale waliofuata ushauri wa Rais Eyring walibarikiwa.

Ahadi yake ilinikumbusha tukio lingine. Nilikutana na Charlotte Hlimi mwenye umri wa miaka 12 karibu na Carcassonne, Ufaransa, mwaka 1990 nilipokuwa nikihudumu kama rais wa misheni. Akina Hlimi walikuwa familia yenye uaminifu iliyoishi katika nyumba moja na watoto wanane. Walikuwa na picha ya Mwokozi na ya nabii ukutani. Katika mahojiano ya baraka zake za patriaki, nilimuuliza Charlotte kama alilipa zaka ya uaminifu. Alijibu, “Ndiyo, Rais Andersen. Mama yangu amenifundisha kwamba kuna baraka za kimwili na baraka za kiroho ambazo huja kutokana na kulipa zaka zetu. Mama yangu alinifundisha kwamba ikiwa kila wakati tunalipa zaka yetu, hatutapungukiwa na chochote. Na Rais Andersen, hatupungukiwi na kitu.”

Familia ya Hlimi.

Katika kunipa mimi ruhusa ya kushiriki hadithi yake, Charlotte, ana umri wa miaka 45 na aliunganishwa hekaluni, alisema: “Ushuhuda wangu wa zaka ulikuwa halisi sana wakati huo, na hata ni thabiti sasa. Ninashukuru sana kwa ajili ya amri hii. Ninapoiishi ninaendelea kubarikiwa kwa wingi.”25

Siku moja kila mmoja wetu atamaliza safari yetu ya duniani. Miaka ishirini na tano iliyopita, siku chache tu kabla ya mama mkwe wangu, Martha Williams, kufariki kwa saratani, alipokea hundi ndogo katika barua. Mara moja alimwomba mke wangu, Kathy, kitabu chake cha hundi ili alipe zaka yake. Kwa kuwa mama yake alikuwa amedhoofika sana kiasi kwamba hakuweza kuandika, Kathy aliuliza ikiwa angeweza kumwandikia hundi hiyo. Mama yake akajibu, “Hapana, Kathy. Nataka kufanya mwenyewe.” Na kisha akaongeza kwa utulivu, “Nataka kuwa sahihi mbele za Bwana.” Mojawapo ya mambo ya mwisho ambayo Kathy alimfanyia mama yake ilikuwa kukabidhi bahasha yake ya zaka kwa askofu wake.

Kazi Muhimu ya Mungu

Kaka zangu na dada zangu, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho “limetokea kufahamika,”26 likileta baraka za kubwa kote duniani. Watakuwepo wanaotushangilia tuendelee mbele na wasiotushangilia. Nimefikiria maneno ya Gamalieli mwenye hekima, ambaye, aliposikia miujiza ya Mtume Petro na Yohana, alilionya baraza huko Yerusalemu:

“Waacheni [watu hawa]; kwa maana ikiwa … kazi hii ni ya wanadamu, itabatilika:

“Lakini ikiwa ya Mungu, hamwezi kuiangamiza; msije … mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”27

Wewe na mimi ni sehemu ya kazi muhimu ya Mungu duniani. Haitabatilika bali itaendelea kuzunguka ulimwenguni kote, ikitayarisha njia ya kurudi kwa Mwokozi. Ninashuhudia kwenye maneno ya Rais Russell M. Nelson: “Katika siku zijazo, tutaona madhihirisho makubwa zaidi ya uwezo wa Mwokozi ambayo ulimwengu haujawahi kuyaona. Kati ya sasa na wakati atakaporudi … Atatoa fursa zisizo na idadi, baraka na miujiza kwa walio waaminifu.”28

Huu ni ushahidi wangu. Yesu ndiye Kristo. Hii ni kazi Yake takatifu. Atakuja tena. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Barua binafsi kutoka kwa Roger Parra, Agosti 4, 2023.

  2. Malaki 3:10.

  3. Ona Malaki 3:11. Mzee Jeffrey R. Holland alisema: “Katika maisha yangu, kwa mfano, nimeona ahadi ya Mungu ikitimizwa kwamba ‘Atamkemea yeye alaye kwa ajili [yangu.]’ [Malaki 3:11]. Baraka hiyo ya ulinzi dhidi ya uovu imemiminwa juu yangu na juu ya wapendwa wangu zaidi ya uwezo wowote ninaopaswa kukiri vya kutosha. Lakini ninaamini kwamba usalama wa kiungu umekuja, angalau kwa kiasi, kwa sababu ya azimio letu, binafsi na kama familia, la kulipa zaka” (“Like a Watered Garden,” Liahona, Jan. 2002, 38).

  4. Bwana atafungua madirisha ya mbinguni kulingana na mahitaji yetu, na si kulingana na ulafi wetu. Ikiwa tunalipa zaka ili kupata utajiri, tunafanya kwa sababu mbaya. … Baraka kwa mtoaji … inaweza isiwe kila mara katika mfumo wa faida ya kifedha au mali” (Yeahings of Gordon B. Hinckley [1997], 657).

  5. Malaki 3:10; 3 Nefi 24:10.

  6. Ona “The Church of Jesus Christ Is Helping Alleviate Global Malnutrition,” Aug. 11, 2023, newsroom.ChurchofJesusChrist.org; ona pia “How the Church of Jesus Christ and UNICEF Are Keeping Mothers and Children Healthy and Safe,” Aug. 17, 2023, newsroom.ChurchofJesusChrist.org.

  7. “Bwana akawaita watu wake Sayuni, kwa sababu wao walikuwa wa moyo mmoja na wazo moja, na waliishi katika haki; na hapakuwa na maskini miongoni mwao” (Musa 7:18).

  8. Ona 1 Wakorintho 2:14. Mantiki ya mwanadamu sio kila wakati inalingana na hekima ya Mungu. Katika siku za Malaki, wengi walikuwa wamejitenga na Bwana. Bwana aliwasihi watu wake wa agano, “Nirudieni mimi, nami nitawarudia ninyi.” Kinachofuata mwaliko huu mwororo ni swali muhimu sana kwa kila mmoja wetu: “Lakini ninyi mwasema, Turudi kwa njia ipi?” (Malaki 3:7). Au kwa maneno mengine, “Nibadilishe kipi? Ninawezaje kukukaribia Wewe?” Bwana hujibu maswali kwa kufundisha umuhimu ya zaka, si tu kama sheria ya kifedha, lakini njia inayoonekana ya kugeuza matamanio ya mioyo yetu Kwake.

    Tuliona hili katika familia yetu wenyewe. Mama yake Kathy alijiunga na Kanisa akiwa na umri wa miaka 22. Martha na Bernard Williams walihudhuria kanisani kwa muda mfupi, lakini baada ya kuhamia jimbo lingine hawakuhudhuria kikamilifu. Bernard alitumwa na jeshi ng’ambo, na Martha akahamia nyumbani Tampa, Florida, ambako alikubali mwaliko wa ukarimu wa kuishi na shangazi yake na mjomba wake, ambao walikuwa wakipinga Kanisa. Huku akiishi katika hali duni sana, akimtarajia mtoto wake wa kwanza na kutohudhuria kanisani, Martha Williams alifanya uamuzi wa kuanza kutuma hundi yake ya fungu la kumi kwa askofu. Baadaye katika maisha yake, alipoulizwa kwa nini, alisema kwamba alikumbuka kitu ambacho wamisionari walikuwa wamemfundisha kuhusu zaka na baraka za Mungu: “Tulihitaji sana baraka za Mungu katika maisha yetu, na hivyo nikaanza kutuma hundi yetu ya zaka kwa askofu.” Martha na Bernard Williams walirudi Kanisani. Baraka yao kuu—vizazi sita vimebarikiwa kwa sababu ya uamuzi wake wa kulipa zaka yake wakati hakuwa na chochote ila imani katika Mungu na tumaini katika ahadi Zake.

  9. Mathayo 22:21.

  10. Ona 3 Nefi 24.

  11. Mafundisho na Maagano 119:3–4. “Zaka ni mchango wa asilimia kumi ya mapato ya mtu kwa Kanisa la Mungu (ona Mafundisho na Maagano 119:3–4.); faida inaeleweka kumaanisha mapato). Waumini wote ambao wana mapato wanapaswa kilipa zaka,” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 34.3.1, Maktaba ya Injili).

  12. Malaki 3:10.

  13. “Tunalipa zaka, kama Mwokozi alivyofundisha, kwa kuleta zaka ‘ghalani’ [Malaki 3:10; 3 Nefi 24:10]. Tunafanya hivi kwa kulipa zaka zetu kwa askofu wetu au rais wa tawi. Hatutoi fungu la kumi kwa kuchangia misaada tunayopenda. Michango tunayopaswa kutoa kama misaada inatoka kwenye fedha zetu wenyewe, si kutoka kwenye zaka tunazoamriwa kulipa kwenye ghala la Bwana” ( Dallin H. Oaks, “Tithing,” Ensign, Mei 1994, 35).

  14. Mafundisho na Maagano 120:1.

  15. Gordon B. Hinckley, “Rise to a Larger Vision of the Work,” Ensign, May 1990, 96.

  16. Ona “The 2022 Report on How the Church of Jesus Christ Cared for Those in Need,” Mar. 22, 2023, newsroom.ChurchofJesusChrist.org.

  17. Imepokelewa kupitia barua pepe kutoka Idara ya Wamisionari, Julai 14, 2023.

  18. Ona “Orodha ya Hekalu,” ChurchofJesusChrist.org/temples/list.

  19. Imepokelewa kupitia barua pepe kutoka Rekodi za Uumini na Takwimu, tarehe 28 Julai 2023.

  20. Hii inajumuisha Chuo Kikuu cha Brigham Young, Chuo Kikuu cha Brigham Young–Idaho, Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii, Chuo cha Ensign, na BYU Pathway Worldwide

  21. Ilipokelewa kupitia barua pepe kutoka Seminari na Chuo mnamo Julai 28, 2023.

  22. Ona Kitabu cha Maelezo Jumla, 34.3.1.

  23. Rais Dallin H. Oaks alishiriki hadithi hii kuhusu kumwamini Bwana: “Mama yangu mjane aliwasaidia watoto wake watatu kwa mshahara [mdogo]. … Nilimuuliza mama kwa nini alilipa kiasi kikubwa cha mshahara wake kama zaka. Sijasahau kamwe maelezo yake: ‘Dallin, huenda kukawa na watu fulani ambao wanaweza kukidhi maisha bila kulipa zaka, lakini sisi hatuwezi. Bwana amechagua kumchukua baba yako na kuniacha niwalee ninyi watoto. Mimi siwezi kufanya hivi bila ya baraka za Bwana, na ninapokea hizo baraka kwa kulipa zaka kwa uaminifu’” (“Zaka,” 33).

  24. “Ili kwa majaliwa yangu, licha ya taabu itakayoshuka juu yenu, kwamba kanisa liweze kusimama huru juu ya viumbe wengine chini ya ulimwengu wa selestia” (Mafundisho na Maagano 78:14).

  25. Barua binafsi kutoka kwa Charlotte Martin, Agosti 30, 2023.

  26. Mafundisho na Maagano 1:30.

  27. Matendo ya Mitume 5:38–39.

  28. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 95.