Mkutano Mkuu
Itakuwa Shangwe Kubwa Namna Gani Kwako
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


13:48

Itakuwa Shangwe Kubwa Namna Gani Kwako

Sasa ninawaalika mchukue ujuzi wenu pamoja na shuhuda zenu zinazoheshimika, na mwende misheni.

Kaka zangu na dada zangu wapendwa, mawazo yangu leo ni juu ya kuikusanya Israeli, kile ambacho Rais Russell M. Nelson anakiita “jambo muhimu zaidi linalotendeka duniani leo. Halilinganishwi na chochote katika ukubwa, halilinganishwi na chochote katika umuhimu, halilinganishwi na chochote katika utukufu.”1

Mkusanyiko huo ni utambuzi muhimu kabisa kwamba “thamani ya nafsi ni kuu mbele za Mungu.”2 Ni rahisi tu kama hivyo. Tunawakusanya watoto wa Mungu katika siku hizi za mwisho ili wapate “kumiminiwa baraka juu ya vichwa vyao”3 na ahadi ya “utajiri wa milele.”4 Kisha ni hivi kwamba ili kuikusanya Israeli tunahitaji wamisionari—wengi zaidi ya wale wanaoshiriki.5 Leo ninazungumza na wazee wengi wenye uzoefu katika Kanisa ambao wanaweza kutumika kama wamisionari. Bwana anawahitaji ninyi. Tunawahitaji huko New York na Chicago, Australia na Afrika, Thailand na Mexico, na kila mahali.

Ngoja niwarudishe nyuma mwaka wa 2015. Nilikuwa mshiriki mpya aliyeitwa wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili. Mojawapo ya majukumu mazuri tunayobeba kama Mitume ni kuwapangia wamisionari maeneo yao ya kazi. Nilishiriki kama Sabini katika mchakato huo,6 lakini sasa kama Mtume, nilihisi uzito kamili wa jukumu hilo. Nilianza kwa maombi kwa kuweka idadi kubwa ya akina kaka na akina dada vijana, mmoja baada ya mwingine, katika misheni kote ulimwenguni. Kisha niligeukia wanandoa wakubwa. Walikuwepo 10 kwenye orodha. Sio wengi sana. Kwa mshangao, nilimuuliza mshiriki wangu kutoka Idara ya Misheni, “Tunahitaji wangapi juma hili ili kujaza maombi?”

Akajibu, “300.”

Wakati huo wa tafakuri umebaki nami: Wenza wanandoa 10 kujaza maombi 300.

Rais Russell M. Nelson amewahimiza wanandoa “kupiga magoti na kumuuliza Baba wa Mbinguni kama wakati ni mwafaka kwao kutumikia misheni pamoja.”7 Kati ya sifa zote za kustahili, alisema, “hamu ya kutumikia inaweza kuwa jambo la maana zaidi.”8

Kama vile maandiko yanavyosema, “Ikiwa una hamu ya kumtumikia Mungu umeitwa kufanya kazi.”9 Kazi hiyo inahusu sheria ya mavuno. Tunasoma katika Yohana, “Apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja.”10

Nimeona sheria ya mavuno ikitimizwa katika familia yangu mwenyewe.

Miaka kadhaa iliyopita nilikuwa nikitembelea familia wakati askofu aliponiomba nihitimishe ibada ya sakramenti.11 Nilipokuwa nikishuka kutoka kwenye jukwaa, mwanamke mmoja alinijia akiwa na watoto wake saba na kujitambulisha kama Dada Rebecca Guzman.

Aliuliza, “Mzee Rasband, unawafahamu Rulon na Verda Rasband?”

Nilifurahi na kujibu, “Hao ni wazazi wangu.”

Unaweza kuona hii ilielekea wapi. Kwa ruhusa ya Rebecca, ambaye yuko hapa na familia katika Kituo cha Mikutano, ninashiriki hadithi ya familia yake.12

Dada Verda na Mzee Rulon Rasband.

Wazazi wangu, Mzee Rulon na Dada Verda Rasband, walikuwa wakitumikia kama wanandoa wenza katika Misheni ya Fort Lauderdale Florida.13 Walikuwa wakitafuta watu wa kuwafundisha na kwa mwongozo wa kiungu wakabisha hodi kwenye mlango wa nyumba ya Rebecca. Alikuwa kijana tu na alipenda kusikiliza muziki wa akina Osmond, hasa rafiki yetu Donny—ambaye pia yuko hapa leo.14 Alikuwa amesikiliza mahojiano yao katika vyombo vya habari na kujua walikuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Alihisi kulikuwa na kitu tofauti kuhusu wao, na akifikiri inaweza kuwa dini yao, Rebecca alitumia miaka miwili kutafiti imani za Kanisa katika maktaba ya shule. Kwa hivyo, wakati wanandoa wenye sura nzuri walipobisha mlango wa familia yake na kujitambulisha wao wenyewe kama wamisionari Watakatifu wa Siku za Mwisho, alikumbuka.

“Mama yangu aliniambia niachane nao,” Rebecca aliandika baadaye, “lakini moyo wangu ukasema, ‘Hapana.’ Nilitazama katika nyuso zao na nikahisi ukarimu na upendo mwingi. Kumbukumbu bado inanitoa machozi na hisia nzito moyoni mwangu.”15

Rebecca aliwakaribisha ndani, na wazazi wangu wamisionari walishiriki ujumbe pamoja naye, dada zake wawili wadogo, na, mama yake licha ya upinzani wake.

Rebecca alinieleza hivi: “Wazazi wako wote wawili walikuwa wazuri katika kufafanua maswali yoyote tuliyokuwa nayo. Bado ninaziona nyuso zao kana kwamba kulikuwa na nuru iliyowazunguka. Mara zote tulimkumbatia mama yako wakati anaondoka na alisisitiza kila wakati kumsaidia mama yangu ili ajihisi vizuri na mwenye kuheshimiwa. Siku zote baba yako alikuwa anang’aa machoni pake alipokuwa akitufundisha kuhusu Yesu Kristo. Alijaribu kumjumuisha baba yangu kwenye majadiliano na hatimaye alifanikiwa. Baba yangu alikuwa mpishi katika klabu ya eneo letu na alianza kupika chakula cha jioni kwa wazazi wako, ikiwa ni pamoja na chakula pendwa cha baba yako cha pai ya ndimu.”16

Wakati Mzee na Dada Rasband walipomwomba Rebecca na familia yake wasome Kitabu cha Mormoni, Rebecca alifanya hivyo kwa siku tano. Alitaka kubatizwa mara moja, lakini wanafamilia wengine hawakuwa tayari. Baada ya miezi minne, Rebecca alisisitiza abatizwe na ajiunge na Kanisa la kweli. Alikumbuka, “Kila nyuzi za nafsi yangu zilijua ni kweli.”17 Mnamo Aprili 5, 1979, wamisionari walimbatiza Rebecca mwenye umri wa miaka 19, mama yake, na dada zake wawili. Baba yangu alikuwa shahidi wakati wa ubatizo.

Nilipokutana na Rebecca na familia yake kanisani, tulipiga picha ya familia yake pamoja nami. Niliipeleka nyumbani kwa mama yangu mzee, na akaishikilia karibu na moyo wake. Kisha akaniambia, “Ronnie, hii ni moja kati ya siku za furaha zaidi maishani mwangu.”

Akina Guzman, Rasband, na Osmond.

Jibu la mama yangu linawauliza wazee wetu swali: “Unafanya nini katika hatua hii ya maisha yako?” Kuna njia nyingi sana wamisionari wakubwa wanaweza kufanya kile ambacho hakuna mtu mwingine anaweza kufanya. Ninyi ni nguvu ya ajabu kwa ajili ya wema, mlioandaliwa katika Kanisa, na mko tayari kuwatia moyo na kuwaokoa watoto wa Mungu.

Huenda baadhi yenu mnafikiri, “Lakini vipi kuhusu kuwaacha wajukuu? Tungekosa matukio muhimu ya familia, siku za kuzaliwa, marafiki na hata wanyama wadogo wa kufugwa.” Kama ningemuuliza mama yangu kwa nini yeye na Baba walienda misheni, najua angesema hivi, “Nina wajukuu. Nataka wajue kwamba baba yako na mimi tulihudumu misheni, tulitaka kuweka mfano kwa vizazi vyetu, na tulibarikiwa, na kubarikiwa sana.”

Nilivyotembelea misheni kote ulimwenguni, nimeona huduma ya kustaajabisha ya kikosi chetu cha wamisionari wazee. Ni wazi wanafurahia kufanya “mapenzi ya Bwana” na kuwa katika “kazi ya Bwana.”18

Kwa wengine, na tunatumaini maelfu yenu, huduma ya muda wote ya umisionari katika kona nyingine ya dunia itakuwa mahali sahihi.19 Kwa wengine, kuhudumu misheni ya huduma ya Kanisa kwenye nchi zenu inaweza kuwa vyema. Kwa sababu ya masuala ya afya na hali nyinginezo, kuna wale ambao hawawezi kuhudumu. Tunaelewa hali hizo, na ni matumaini yangu mnaweza kupata njia za kuwasaidia wale wanaohudumu. Fuata ushauri wa nabii na uombe kujua ni nini Bwana angetaka ufanye.

Maeneo ya misheni kote ulimwenguni yanaomba usaidizi wako. Rais Nelson amesema kuhusu wamisionari wetu wazee, “Ni vijana kiroho, wenye hekima, na wako tayari kufanya kazi.”20

Mkiwa kwenye maeneo yenu, mna fursa nyingi: mnaweza kuhudumu katika ofisi za misheni au kwenye mahekalu, kuwaimarisha wamisionari vijana, kuimarisha matawi madogo, kufanya kazi katika vituo vya historia ya familia au katika maeneo ya kihistoria, kufundisha chuo cha Kanisa, kutoa huduma ya kibinadamu, kufanya kazi na vijana, kusaidia katika vituo vya ajira au kwenye mashamba ya Kanisa. Maelezo ya njia za kutumikia, yale yanayokufaa zaidi, mahali unapohitajika, na jinsi unavyoweza kujiandaa kwenda yanajibiwa kwenye tovuti ya “Senior Missionary.”21 Unaweza pia kuzungumza na askofu wako au rais wako wa tawi.

Nimewaita wanandoa wengi kutumikia na kutazama jinsi Nuru ya Kristo inavyojaza nyuso zao.22 Wakati wa kurejea kwao, wameelezea kuwa karibu na Bwana na karibu zaidi na mmoja na mwingine, wakimhisi Roho wa Bwana akishuka juu yao, na kujua kwamba wanaleta tofauti.23 Nani hatataka hilo?

Misheni inaweza kuwa sura kuu katika maisha ya wanandoa. Jina zuri linaweza kuwa “Bwana Wangu Atanihitaji.”24 Unaweza kuwa kwenye ardhi usiyoijua; hata hivyo, nguvu za Roho zitakufanya uhisi uko nyumbani.

Wazazi wangu, na makumi ya maelfu ya wanandoa wamisionari waliorejea wametoa ushuhuda wa furaha waliopata katika kazi ya umisionari. Bwana amesema katika maandiko ya Siku za Mwisho, “Na kama itakuwa kwamba utafanya kazi siku zako zote katika kutangaza toba kwa watu hawa, na kuleta, japo iwe nafsi moja kwangu, shangwe yako itakuwa kubwa jinsi gani pamoja naye katika ufalme wa Baba yangu!”25

Isaya alitupatia maelezo ya kishairi ya maana ya kuhudumu katika “eneo” la misheni. Maandiko yanatuambia “eneo ni ulimwengu.”26 Nabii huyu mkuu wa kale aliandika, “Kwa maana mtatoka kwa furaha, na kuongozwa kwa amani: mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi.”27 Milima, vilima, mashamba, na miti vinaweza kulinganishwa na marais wa misheni, maaskofu, viongozi wa wilaya, waumini, na wale wanaotafuta ukweli lakini “hawajui ni wapi pa kuupata.”28 Watashuhudia kwamba wamisionari wazee wanabadili eneo la misheni kwa shuhuda zao za Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo.

Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninakuomba utumikie kama mmisionari katika kuikusanya Israeli na pengine utumikie tena. Tunakuhitaji—tunawahitaji. Tunawashukuru ninyi wazee, kwa maisha ambayo mmeishi na mifano ambayo mmekuwa katika nyumba zenu, kata na vigingi. Sasa ninawaalika mchukue ujuzi wenu pamoja na shuhuda zenu zinazoheshimika, na mwende misheni. Ninaomba kwamba wakati mwingine nitakapokaa kuwapangia wanandoa wakubwa kutakuwa na mamia yenu mkingojea kwa hamu wito wenu.

Pia ninaahidi kwamba mnapotumikia, mtahisi upendo wa Bwana maishani mwenu, mtamjua Yeye, Naye atawajua ninyi, na “jinsi gani shangwe yenu itakuwa kuu.”29 Huduma yenu ya kujitolea kwa Yesu Kristo itatia moyo na kubariki familia yako, wajukuu zako na vitukuu. “Amani na upendo vitaongezeka”30 katika maisha yao kwa miaka mingi ijayo. Ninaahidi Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (mkutano wa ibada ya vijana ulimwenguni kote, Juni 3, 2018), Maktaba ya Injili.

  2. Mafundisho na Maagano 18:10.

  3. 3 Nefi 10:18.

  4. Mafundisho na Maagano 78:18.

  5. Kanisa lina wamisionari 71,000 katika misheni 414 ulimwenguni kote, kutoka Amerika ya Kaskazini na Kusini hadi Ulaya na Afrika, Asia, na Australia/Oceania. Kuna wamisionari wazee wa huduma ya Kanisa 34,000. (Data ya Idara ya Umisionari, Sept. 2023.)

  6. Ona Ronald A. Rasband, “Wito Mtakatifu wa Mmisionari,” Liahona, Mei 2010, 52–53.

  7. Russell M. Nelson, “Nyakati za Wamisionari Wazee,” Liahona, Nov. 2016, 27.

  8. Russell M. Nelson, “Senior Missionaries and the Gospel,” Liahona, Nov. 2004, 81.

  9. Mafundisho na Maagano 4:3.

  10. Yohana 4:36.

  11. Nilikuwa New York, Marekani, nikihudhuria ubatizo wa mjukuu wa kike Brooklyn na baraka ya mjukuu wa kike Ella, Aprili 2006.

  12. Barua kutoka kwa Rebecca Guzman kwenda kwa Mzee Ronald A. Rasband, Septemba 8, 2009.

  13. Wazazi wangu walitumikia katika Misheni ya Fort Lauderdale Florida mwaka 1979.

  14. Familia ya Osmond ilikuwa kikundi maarufu cha muziki cha Amerika kinachojulikana kwa nyimbo zao za pop. Kikundi kilifikia kilele cha umaarufu katikati ya miaka ya 1970, kikitumbuiza kwenye vipindi vya televisheni. Donny na Marie waliendelea na televisheni na kazi za jukwaani huku akina kaka wakitumbuiza kwa miongo kadhaa kama wasanii wa nchi huko Branson, Missouri.

  15. Barua kutoka kwa Rebecca Guzman, Sept. 8, 2009.

  16. Barua kutoka kwa Rebecca Guzman, Sept. 8, 2009.

  17. Barua kutoka kwa Rebecca Guzman, Sept. 8, 2009.

  18. Mafundisho na Maagano 64:29.

  19. Nafasi za wamisionari wazee huwa za aina nyingi, na wanandoa au akina dada wazee wanaweza kuorodhesha mapendeleo na vile vile muda wote au huduma ya Kanisa. Hatimaye, nabii wa Kanisa anatoa wito wa huduma ya muda wote. Marais wa vigingi hutoa majukumu ya huduma ya Kanisa. Huduma inaweza kuanzia miezi 6 hadi 23, na wamisionari watu wazee wana uhuru zaidi, na shughuli zisizo na ratiba kama wamisionari vijana. Ona seniormissionary.ChurchofJesusChrist.org.

  20. Russell M. Nelson, “Wamisionari Wazee na Injili,” Liahona, Nov. 2004.

  21. Ona seniormissionary.ChurchofJesusChrist.org.

  22. Ona Alma 5:14. “Mwonekano” unaweza kuelezwa kuwa unaonesha mtazamo wa kiroho wa mtu binafsi na hali yake ya akili.

  23. Ona Yuda 1:22; Mosia 4:20.

  24. Ona “Nitakwenda Utakako,” Nyimbo za Dini, no. 154.

  25. Mafundisho na Maagano 18:15.

  26. Bwana alieleza, “Shamba ni ulimwengu; … mavuno ni mwisho wa dunia” (Mathayo 13:38–39).

  27. Isaya 55:12.

  28. Mafundisho na Maagano 123:12.

  29. Mafundisho na Maagano 18:15.

  30. Yuda 1:2.