Mkutano Mkuu
Mpende Jirani Yako
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Mpende Jirani Yako

Huruma ni sifa ya Kristo. Inazaliwa na upendo kwa wengine na haina mipaka.

Asubuhi hiii, ninawaalika kujiunga nami kwenye safari ya Kiafrika. Hamtaona simba wowote, pundamilia au tembo, isipokuwa mwisho wa safari, mtaona jinsi maelfu ya waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wanavyoitikia amri kuu ya pili ya Kristo ya “kupenda jirani yako” (Marko 12:31).

Fikiria kwa muda, udongo mwekundu, wa kijiji cha Afrika. Unaona kutoka kwenye ardhi iliyo kavu na isiyo na uoto kwamba mvua haijanyesha kwa kiwango cha kutosha kwa miaka mingi. Mifugo michache iliyokonda inayopita mbele yako ikiswagwa na mfugaji mwenye blanketi wa Karamojong akiwa amevalia ndala, akitembea kwa tumaini la kupata malisho na maji.

Wakati ukipita kwenye barabara ya vumbi na mawe, unaona makundi kadhaa ya watoto wa kupendeza na kushangaa kwa nini hawako shuleni. Watoto wanatabasamu na kukupungia mkono, nawe unawapungia mkono ukiwa na machozi na tabasamu. Asilimia tisini na mbili ya watoto wadogo unaowaona kwenye safari hii wanaishi kwenye ukata wa chakula na moyo wako unahuzunishwa kwa uchungu.

Mbele yako, unamuona mama amebeba kwa umakini chombo cha kutosha galoni tano (19 L) za maji kichwani mwake na kingine mkononi mwake. Anawakilisha moja kati ya kila kaya mbili kwenye eneo hili ambapo wanawake, wadogo kwa wakubwa, wanatembea zaidi ya dakika thelathini kwenda na kurudi, kila siku, kufuata maji kwa ajili ya familia zao. Unapatwa na wimbi la huzuni.

Picha
Mwanamke wa Kiafrika amebeba maji.

Saa mbili zinapita na unafika kwenye eneo lililotengwa, lenye kivuli. Sehemu ya kukutania si ukumbi wala hema bali chini ya miti mikubwa michache ikitoa kivuli dhidi ya jua kali. Kwenye sehemu hii, unagundua kwamba hakuna maji yatiririkayo, umeme wala vyoo vya kisasa. Unaangalia kuzunguka eneo zima na kujua kwamba u kati ya watu ambao wanampenda Mungu na mara moja unahisi upendo wa Mungu kwao. Wamekutana ili kupokea msaada na tumaini, na umefika kushiriki nao.

Hiyo ndivyo ilivyokuwa safari yangu na Dada Arden, tukiwasindikiza Dada Camille Johnson, Rais wetu Mkuu wa Muungano wa Usaidizi pamoja na Doug, mume wake na Dada Sharon Eubank, mkurugenzi wa Huduma za Kibinadamu za Kanisa, wakati tukisafiri huko Uganda, nchi yenye watu milioni 47 katika eneo la Kanisa la Afrika ya Kati. Siku hiyo, chini ya kivuli cha miti, tulitembelea mradi wa kijamii wa afya ambao unadhaminiwa kwa pamoja na Huduma za Kibinadamu za Kanisa, UNICEF na Wizara ya Afya ya Serikali ya Uganda. Hizi ni taasisi za kuaminika, zilizochaguliwa kiumakini kuhakikisha msaada wa kibinadamu uliotolewa na waumini wa Kanisa unatumika kwa busara.

Picha
Mtoto wa Kiafrika akipokea uangalizi.

Kadiri ilivyokuwa ya kuvunja moyo kuona watoto wenye utapia mlo na madhara ya kifua kikuu, malaria na kipindupindu, lilikuja kwa kila mmoja wetu ongezeko la tumaini la kesho iliyo nzuri zaidi kwa ajili ya wale tuliokutana nao.

Picha
Mama akimlisha mtoto wake.

Tumaini hilo lilikuja, kama sehemu, kupitia ukarimu wa waumini wa Kanisa kutoka kote ulimwenguni ambao wanachangia muda na fedha kwenye juhudi za Kanisa za Kibinadamu. Wakati nilipowaona wagonjwa na walioathiriwa wakisaidiwa na kuinuliwa, niliinamisha kichwa changu kwa shukrani. Wakati ule, nilielewa vyema kile ilichomaanishwa na Mfalme wa wafalme, ambaye alisema:

“Njooni, enyi mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme ulioandaliwa kwa ajili yenu … :

“Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula: nalikuwa na kiu, mkaninywesha: nalikuwa mgeni, mkanikaribisha” (Mathayo 25:34–35).

Mwaliko wa Mwokozi ni kuacha “Nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni” (Mathayo 5:16; ona pia mistari 14–15). Katika sehemu hiyo ya mbali ya dunia, matendo yenu mema yaliangaza maisha na kufanya mizigo ya watu wenye uhitaji mkubwa kuwa miepesi, na Mungu alitukuzwa.

Siku hiyo ya joto na vumbi sana, nilitamani mngeweza kusikia sala zao za dhati za shukrani kwa Mungu. Wangenitaka nisema kwenu kwa lugha yao ya Kikaramojong, “Alakara.” Asante.

Safari yetu ilinikumbusha fumbo la Msamaria Mwema, ambaye safari yake ilimpeleka kwenye njia ya vumbi, si kama ambayo nimeielezea, lakini ambayo ilitoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Msamaria huyu mhudumiaji anatufundisha kile inachomaanisha “kumpenda jirani yako.”

Alimuona “mtu … [ambaye] aliangukia mikononi mwa wanyang’anyi, waliomvua nguo, na wakamtia jeraha, wakaenda zao wakimwacha karibu ya kufa” (Luka 10:30). Msamaria mwema “alimhurumia” (Luka 10:33).

Huruma ni sifa ya Kristo. Inazaliwa na upendo kwa wengine na haina mipaka. Yesu, Mwokozi wa ulimwengu, ni mfano mkamilifu wa Huruma. Wakati tunaposoma kwamba “Yesu akalia machozi” (Yohana 11:35) tu mashahidi, kama Mariamu na Martha, kwa huruma Yake ambayo ilisababisha Yeye kuugua na kufadhaika roho (ona Yohana 11:33). Katika mfano wa Kristo wa huruma kwenye Kitabu cha Mormoni, Yesu aliwatokea umati na kusema:

“Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au vilema … au wale walio viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani ninayo huruma juu yenu. …

“… Na akawaponya kila mmoja” (3 Nefi 17:7, 9).

Bila kujali juhudi zetu zote, mimi na wewe hatutaweza kumponya kila mtu lakini kila mmoja wetu anaweza kuwa mwenye kuleta tofauti kupitia wema katika maisha ya mtu fulani. Ilikuwa ni kijana mmoja, mvulana tu, ambaye alitoa mikate mitano na samaki wawili ambapo watu elfu tano walilishwa. Tunaweza kuwa na maswali kwenye matoleo yetu, kama mwanafunzi Andrea alivyofanya juu ya mikate na samaki, “Hivi ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yohana 6:9). Ninakuhakikishieni: inatosha kutoa au kufanya kile ambacho unaweza, na kisha kuruhusu Kristo akuze juhudi zako.

Kwenye kipengele hiki, Mzee Jeffrey R. Holland alitualika “Tajiri au maskini, … tutende kile tumachoweza’ wakati wengine wanapokuwa katika shida.” Kisha alishuhudia, ninapofanya hivyo, kwamba Mungu “atakusaidia na kukuongoza katika matendo [yako] ya huruma ya ufuasi” (“Je, Sisi Sote Si Waombaji?,” Liahona, Nov. 2014, 41).

Katika nchi ile ya mbali, katika siku ile isiyosahaulika, nilisimama wakati huo na ninasimama sasa kama shahidi wa huruma inayochochea nafsi na inayobadili maisha ya waumini wa Kanisa, wote matajiri na maskini.

Mfano wa Msamaria Mwema unaendelea wakati “akifunga jeraha la [mtu yule] … na kumpeleka kwenye nyumba ya wageni” (Luka 10:34). Juhudi zetu za Msaada wa Kibinadamu za Kanisa hutufanya tuitikie kwa haraka kwenye majanga ya asili na kufunga majeraha makubwa ya ulimwengu ya magonjwa, njaa, utapia mlo, uhamiaji na majeraha yasiyoonekana ya kukatishwa tamaa, kuvunjika moyo na kukosa tumaini.

Msamaria kisha “akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu” (Luka 10:35). Kama Kanisa tuna shukrani kuungana na “wenyeji” wengine au taasisi kama ile ya Huduma ya Usaidizi ya Kikatoliki, UNICEF, na Msalaba Mwekundu/Mwezi Mwekundu, kusaidia kwenye juhudi zetu za kibinadamu. Vilevile tuna shukrani kwa “dinari zenu mbili” au yuro mbili, peso mbili au shilingi mbili, ambazo zinapunguza mzigo ambao wengi duniani wanaubeba. Inawezekana hamtapata kuwajua wapokeaji wa muda wenu, dola na mchango wenu mdogo, lakini huruma haituhitaji tuwajue, inatuhitaji tuwapende tu.

Asante, Rais Russell M. Nelson, kwa kutukumbusha kwamba “wakati tunapompenda Mungu kwa mioyo yetu yote, Yeye huigeuza mioyo yetu kuelekea kwenye ustawi wa wengine” (“Amri Kuu ya Pili,” Liahona, Nov. 2019, 97). Ninashuhudia kwamba kila mmoja wetu atakuwa na ongezeko la shangwe, amani, unyenyekevu na upendo wakati tunapoitikia wito wa Rais Nelson wa kuigeuza mioyo yetu kwa ajili ya ustawi wa wengine na wa Joseph Smith wa “kuwalisha wenye njaa, kuwavika walio uchi, kutoa kwa wajane, kufuta machozi ya yatima, [na] kuwafariji walioateswa, iwe kwenye Kanisa hili, au lingine lolote au kusiko na kanisa kabisa, kokote [tutakapowapata]” ( “Editor’s Reply to a Letter from Richard Savary,” Times and Seasons, Mar. 15, 1842, 732).

Picha
Mzee Ardern na Rais Camille N. Johnson pamoja na watoto wa Kiafrika.

Miezi hiyo yote iliyopita, tuliwapata wenye njaa na walioathiriwa kwenye ardhi kavu na yenye vumbi na tulikuwa mashahidi wa macho yao yaliyosihi kwa ajili ya msaada. Katika njia yetu sisi wenyewe, tunaugua na kufadhaika roho (ona Yohana 11:33) na bado hisia hizo zilibadilishwa wakati tulipoona huruma ya waumini wa Kanisa wakiwa kwenye kazi ambapo wenye njaa walilishwa, wajane walipewa msaada, na walioathirika walipewa faraja na machozi yao kufutwa.

Na daima tuangalie ustawi wa wengine na kuonyesha kwa maneno na vitendo kwamba sisi tu “tayari kubebeana mizigo” (Mosia 18:8), “kufunga mioyo iliyovunjika” (Mafundisho na Maagano 138:42), na kushika amri kuu ya pili ya Kristo ya “kumpenda jirani” (Marko 12:31). Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha