Mungu Anakujua na Anakupenda
Mpango wote wa Mungu wa furaha ni kuhusu ninyi. Wewe ni mtoto Wake wa thamani na ni mwenye thamani kuu.
Miaka sita iliyopita, familia yetu ilikuwa ikisafiri usiku nje tu ya jiji la Oxford. Kama ilivyo kawaida kwa watoto wadogo, tulihitaji kusimama, hivyo tukatafuta kituo cha kujaza mafuta chenye msururu wa maduka na migahawa. Kwa usahihi tulitoka ndani ya gari, tukaenda kwenye huduma, na kupanda tena garini, kuendelea tena na safari yetu.
Dakika kumi na tano baadaye, mwana wetu mkubwa akauliza swali la kipekee: “Jasper yuko wapi?” Jasper hukaa peke yake nyuma. Tulidhania kuwa amelala usingizi au amejificha au anatuchezea mchezo.
Kaka yake alipochunguza nyuma ya gari kwa makini, tuligundua kuwa mvulana wetu mwenye umri wa miaka mitano hakuwepo. Mioyo yetu ikajawa na hofu. Wakati tunageuza gari kurudi kule kituo cha kujazia mafuta, tulimwomba Baba wa Mbinguni kwamba Jasper angekuwa salama. Tulipiga simu polisi na kuwaarifu hali ilivyo.
Kwa shauku tulipowasili, baada ya zaidi ya dakika arobaini, tuliona magari mawili ya polisi katika eneo la kupaki magari, taa zikiwa zinawaka. Ndani ya gari moja alikuwepo Jasper akicheza na vitufe. Sitaweza kusahau shangwe tuliyohisi ya kuungana naye tena.
Mengi ya mafundisho ya Mwokozi ya mifano yanafokasi kwenye kukusanyika, kurejesha, au kujitahidi kutafuta kile ambacho kimetawanywa au kupotea. Miongoni mwa hayo ni mifano ya kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea na mwana mpotevu.1
Kama vile tukio la Jasper lilivyojirudia akilini mwangu kwa miaka mingi, nimetafakari juu ya utambulisho wa kiungu na umuhimu wa watoto wa Mungu, nguvu zenye kukomboa za Yesu Kristo, na ule upendo mkamilifu wa Baba wa Mbinguni, ambaye anakujua wewe na mimi. Ninatumaini kutoa ushahidi wa kweli hizi hivi leo.
I. Watoto wa Mungu
Maisha yana changamoto. Watu wengi wanahisi kulemewa, wapweke, waliotengwa au dhaifu. Mambo yanapokuwa magumu, tunaweza kuhisi kwamba tumepotea au tumechelewa. Kujua kwamba sisi sote tu watoto wa Mungu, na washiriki wa familia Yake ya milele kutarejesha hisia ya ushirika na ya dhumuni.2
Rais Ballard alishiriki: “Kuna utambulisho mmoja muhimu ambao sisi sote tunashiriki sasa na milele. … Hivyo ndivyo ulivyo na daima umekuwa hivyo mwana au binti wa Mungu. … Kuelewa ukweli huu—kuuelewa hasa na kuukumbatia—ni badiliko la maisha.”3
Tafadhali usielewe vibaya au kujishusha thamani kwa jinsi ulivyo wa muhimu kwa Baba yako wa Mbinguni. Wewe sio tunda la bidhaa ya asili lililotokana na ajali, au yatima wa badiliko la dunia, au jambo la matokeo ya maada jumlisha na muda jumlisha na nafasi. Palipo na usanifu, yupo msanifu.
Maisha yako yana maana na dhumuni. Urejesho unaoendelea wa injili ya Yesu Kristo unaleta nuru na uelewa kuhusu utambulisho wako wa kiungu. Wewe ni mtoto mpendwa wa Baba wa Mbinguni. Wewe ndiye mada ya mifano na mafundisho yote. Mungu anakupenda sana kwamba alimtuma Mwanawe ili akuponye, akuokoe na kukukomboa.4
Yesu Kristo alitambua asili takatifu na ustahili wa milele wa kila mtu.5 Alielezea jinsi gani amri kuu mbili za kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu ndio msingi wa amri zote za Mungu.6 Moja ya wajibu wa kiungu ni kuwajali wale walio katika shida.7 Hii ndio sababu wafuasi wa Yesu Kristo, “tunabebeana mizigo, … tunaomboleza na wale wanaoomboleza … , na kuwafariji wale wanaohitaji faraja.”8
Dini sio tu kuhusu uhusiano wetu na Mungu; pia ni juu ya uhusiano wetu sisi kwa sisi. Mzee Holland alielezea kwamba neno la Kiingereza dini linatokana na Kilatino religare, likimaanisha “kufunga” au maana ya wazi zaidi “kufunga tena.” Hivyo, “dini ya kweli [ni] kamba ambayo inatufunga sisi kwa Mungu na kwa kila mmoja.”9
Jinsi gani tunatendeana hakika ni jambo la muhimu. Rais Nelson anafundisha, “Ujumbe wa Mwokozi u wazi: wafuasi Wake wa kweli hujenga, huinua, huimiza, hushawishi na kuvutia.”10 Hii ni muhimu wakati wasafiri wenzetu wanapohisi wamepote, wapweke, wamesahauliwa au wameondolewa.
Hatuhitaji kutazama mbali ili kupata watu wanaotaabika. Tunaweza kuanza kwa kumsaidia mtu mmoja katika familia yetu wenyewe, au kusanyiko, au jumuiya yetu. Tunaweza pia kutafuta kupunguza makali ya mateso ya watu milioni 700 wanaoishi na ufukara mkali11 au wale watu milioni 100 waliolazimishwa kwa nguvu kuhama makazi yao kutokana na mateso, migogoro na machafuko yenye msingi wa utambulisho.12 Yesu Kristo ni mfano mkamilifu wa kuwajali walio katika shida—wenye njaa, walio ugenini, wagonjwa, masikini, walio kifungoni. Kazi yake ni Kazi yetu.
Mzee Gerrit W. Gong anafundisha kwamba “safari yetu kuelekea kwa Mungu mara kwa mara huwa ya pamoja.”13 Kwa jinsi hiyo, kata zetu zinapaswa kuwa kimbilio kwa watoto wote wa Mungu. Je, tunahudhuria Kanisani kwa nia isiyo ya dhati au kwa dhati tunajenga jumuiya ambazo dhumuni lao ni kuabudu, kumkumbuka Kristo na kuhudumiana?14 Tunaweza kutii ushauri wa Rais Nelson kuacha kuhukumu, kupenda zaidi na kueneza upendo wa Yesu Kristo kupitia maneno na matendo yetu.15
II. Nguvu ya Uponyaji ya Yesu Kristo
Upatanisho wa Yesu Kristo ndio kielelezo cha upendo wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake.16 Neno upatanisho linafafanua kuwaweka pamoja wale waliofarakana au kutengana.
Huduma ya Mwokozi wetu ilikuwa kutoa njia ya kurudi kwa Baba wa Mbinguni na msaada safarini. Mwokozi anajua kupitia uzoefu Wake jinsi gani ya kutusaidia sisi kwenye changamoto za maisha.17 Usifanye makosa: Kristo ni mwokoaji wetu na mponyaji wa nafsi zetu.
Tutumiapo imani, Yeye hutusaidia kusonga mbele kupita magumu. Yeye anaendelea kutoa mwaliko Wake wenye upendo na wenye rehema:
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
“Jitieni nira yangu, na mkajifunze kwangu; … nanyi mtapata pumziko la nafsi zenu.”18
Mfano wa nira ni wa muhimu sana. Kama Rais Howard W. Hunter alivyoelezea: “Nira ni kifaa … ambacho kiliruhusu nguvu za mnyama wa pili kuunganishwa na kuzidishwa kwenye jitihada za mnyama mmoja, wakishirikiana na kupunguza kazi nzito ya jukumu lililo [mkononi]. Mzigo uliokuwa ukimzidia au pengine kutowezekana kwa mtu mmoja kubebwa unaweza na kwa faraja kubebwa na wawili waliofungwa kwa pamoja na nira ya pamoja.”19
Rais Nelson alifundisha: “Unakuja kwa Kristo ili ufungwe nira pamoja Naye na pamoja na nguvu Zake, ili kwamba usivute mzigo wa maisha peke yako. Unavuta uzito wa maisha ukiwa umefungwa nira pamoja na Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu.”20
Je, sisi tunafungaje nira, au kujifunga wenyewe kwa Mwokozi? Mzee David A. Bednar alifundisha:
“Kufanya na kushika maagano matakatifu hutuunganisha na Bwana Yesu Kristo. Kimsingi, Mwokozi anatuita tumtegemee na tuvute pamoja Naye. …
“Sisi hatuwezi na kamwe hatuhitaji kuwa peke yetu.”21
Kwa yeyote alemewaye na mzigo, aliyepotea, aliyekanganywa: huna haja ya kuwa peke yako.22 Kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo na ibada Zake, unaweza kufungwa nira au kuunganishwa Naye. Kwa upendo atatoa nguvu na uponyaji unaohitaji ili kuikabili safari iliyo mbele yako. Yeye ni kimbilio dhidi ya dhoruba.23
III. Upendo wa Baba wa Mbinguni
Kwa kumbukumbu, Jasper ni mjanja, mwenye upendo,\ mwenye akili na mtundu. Lakini kitu muhimu katika hadithi hii ni kwamba yeye ni wangu. Yeye ni mwanangu ninampenda zaidi kuliko yeye atakavyojua. Kama mtu asiye mkamilifu, baba wa duniani anajihisi hivyo, unaweza kufikiria jinsi gani Baba wa Mbinguni aliyemkamilifu, mtukufu, mwenye upendo anavyojihisi kuhusu wewe?
Kwa marafiki zangu wapendwa wa kizazi kinachoinukia, Kizazi Z na Kizazi Alpha: Tafadhali jueni kwamba imani inahitaji vitendo.24 Tunaishi katika wakati ambao, kwa wengi “kuona ndio kuamini.” Imani inaweza kuwa changamoto na inahitaji chaguzi. Lakini sala zinajibiwa.25 Na majibu yanaweza kuhisika.26 Baadhi ya vitu ambavyo ni halisi sana katika maisha havionekani; vinahisiwa, vinajulikana na vinapatikana kwa uzoefu. Navyo pia ni halisi.
Yesu Kristo anataka wewe ujue na uwe na uhusiano na Baba yako wa Mbinguni.27 Yeye alifundisha, “Nani miongoni mwenu, mwenye mwana, akiwa amesimama nje, na aseme, Baba, fungua nyumba yako ili niweze kuingia na kula pamoja nawe, ambaye hatasema, Karibu, mwanangu; kilicho changu ni chako, na chako changu?”28 Unaweza kufikiria juu ya mtu binafsi zaidi mwenye upendo, zaidi ya Mungu Baba wa Milele?
Wewe ni mtoto Wake. Kama unahisi umepotea, kama una maswali au kupungukiwa hekima, kama unapambana na hali zako au unasumbuka na mfarakano wa kiroho, mgeukie Yeye. Omba faraja, upendo, majibu na mwelekeo. Hitaji lako lolote na mahali popote ulipo, mimina moyo wako kwa Baba yako wa Mbinguni. Kwa baadhi yenu, mnaweza kutaka kufuata mwaliko wa Rais Nelson na kuuliza “kama Yeye kweli yupo—Kama Yeye anakujua wewe. Muulize Yeye jinsi Anavyohisi kuhusu wewe. Na kisha sikiliza.”29
Wapendwa akina Kaka na akina Dada:
-
Mjueni Baba yenu aliye Mbinguni. Yeye ni mkamilifu na mwenye upendo.
-
Mjueni Yesu Kristo ni nani.30 Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Jiunganisheni wenyewe na wale uwapendao Kwake.
-
Na jueni ninyi ni nani. Jueni utambulisho wenu wa kweli wa kiungu. Mpango wote wa Mungu wa upendo ni kuhusu ninyi. Wewe ni mtoto Wake mwema na una thamani kuu. Yeye anakujua na anakupenda.
Juu ya kweli hizi rahisi lakini kweli za kimsingi, nashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.