Kutembea katika Uhusiano wa Agano na Kristo
Yule aliyejeruhiwa na kuvunjwa kwa ajili yetu ataruhusu maisha haya yafanye kazi ndani yetu, lakini Yeye hatuachi tukabiliane na changamoto hizo peke yetu.
Nilitambulishwa kwenye njia huko Israeli na rafiki yangu mwema Ilan. “Inaitwa Njia ya Yesu,” alisema, “kwa sababu ni njia inayotoka Nazareti mpaka Kapernaumu ambayo watu wengi wanaamini Yesu aliipita. Niliamua wakati huo na palepale kwamba nilitaka kuipita njia hiyo, hivyo nilianza kupanga safari kwenda Israeli.
Wiki sita kabla ya safari, nilivunjika kiwiko cha mguu. Mume wangu alihofu kuhusu jeraha; wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa ni jinsi gani ningetembea Njia ya Yesu mwezi mmoja baadaye. Nina asili ya ushupavu, hivyo sikufuta tiketi yangu ya ndege.
Nakumbuka kukutana na kiongozi wetu Mwisraeli asubuhi ile nzuri ya mwezi Juni. Nilichechemea kutoka garini na kisha kutoa jozi ya magongo na skuta ya magoti. Mya, mwongozaji wetu, aliangalia bandeji yangu, na kusema, “Mh, sidhani kama utaweza kutembea njia hii katika hali hiyo.”
“Pengine siwezi,” nilijibu. “Lakini hakuna kinachonizuia kujaribu.” Aliitikia kwa kichwa, na tulianza. Ninampenda kwa ajili ya hilo, kwa kuamini ningeweza kutembea njia ile nikiwa nimevunjika mguu.
Nilitembea kwenye njia yenye mteremko na miamba kwa muda mimi mwenyewe. Kisha, akisukumwa na udhati wa msimamo wangu, Mya alitoa kamba nyembamba, akaifunga kwenye mishikio ya skuta, na akaanza kuvuta. Alinivuta juu vilimani, kupitia vichaka vya milimao, na kwenye kingo za Bahari ya Galilaya. Mwisho wa safari, nilitoa shukrani kwa mwongozaji wangu mzuri, ambaye alikuwa amenisaidia nikamilishe jambo ambalo kamwe nisingeweza kulikamilisha peke yangu.
Bwana alipomwita Henoko asafiri kote nchini na ashuhudie juu Yake, Henoko alisita.1 Alikuwa kijana mdogo, si mwepesi wa kusema. Ni kwa jinsi gani angetembea njia ile katika hali yake? Alipofushwa na kile kilichokuwa kimevunjika ndani yake. Jibu la Bwana kwenye kile kilichomzuia lilikuwa rahisi na la papo hapo: “Tembea pamoja nami.”2 Kama vile Henoko, tunapaswa kukumbuka kwamba Yule aliyejeruhiwa na kuvunjwa kwa ajili yetu3 ataruhusu maisha haya yafanye kazi ndani yetu, lakini Yeye hatotuacha tukabiliane na changamoto hizo peke yetu.4 Licha ya uzito wa hadithi yetu, au hali ya sasa ya njia yetu, Yeye atatualika tutembee pamoja Naye.5
Mfikirie kijana mdogo kwenye matatizo ambaye alikutana na Bwana nyikani. Yakobo alikuwa amesafiri mbali na nyumbani. Katika usiku wa giza, aliota ndoto ambayo si tu ilikuwa na ngazi lakini pia ilikuwa na ahadi muhimu sana za agano, ikijumuisha kile ninachopenda kukiita ahadi ya vidole vitano.6 Usiku ule, Bwana alisimama kando ya Yakobo, akajitambulisha kama Mungu wa baba wa Yakobo, na kisha akaahidi:
-
Nipo pamoja nawe.
-
Nitakulinda kila uendako.
-
Nami nitakuleta tena mpaka nchi hii.
-
Sitakuacha.
-
Nitakufanyia hayo niliyokuambia.7
Yakobo alikuwa na uchaguzi wa kufanya. Angechagua kuishi maisha yake akiwa na ufahamu wa Mungu wa baba yake, au angechagua kuishi maisha katika msimamo wa agano pamoja Naye. Miaka kadhaa baadaye Yakobo alishuhudia juu ya maisha ndani ya ahadi za agano la Bwana: “Mungu … alinisikia siku ya shida yangu, na akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea.”8 Kama vile alivyofanya kwa Yakobo, Bwana atatujibu kila mmoja wetu katika siku yetu ya dhiki ikiwa tutachagua kuunganisha maisha yetu na Yake. Yeye ameahidi kutembea pamoja nasi njiani.
Tunaweza kuita matembezi haya njia ya agano—njia inayoanza na agano la ubatizo na kuongoza kwenye maagano ya kina zaidi tunayoyafanya hekaluni. Pengine unasikia maneno hayo na kufikiria orodha ya kuweka tiki. Pengine yote uyaonayo ni njia yenye masharti. Kwa mtazamo wa karibu jambo la kuvutia zaidi hufunuliwa. Agano si tu kuhusu mkataba, japokuwa hilo ni muhimu. Ni kuhusu uhusiano. Rais Russel M. Nelson alifundisha, “Njia ya agano ni kuhusu uhusiano wetu na Mungu.”9
Fikiria agano la ndoa. Tarehe ya ndoa ni muhimu, lakini chenye umuhimu sawa ni uhusiano unaojengwa kupitia maisha ya pamoja baada ya hapo. Ndivyo ilivyo kweli kwa uhusiano wa agano na Mungu. Masharti yameshaweka na kutakuwa na matarajio huko njiani. Na bado Yeye anamwalika kila mmoja wetu aje kadiri tunavyoweza, kwa kusudi halisi la moyo, na “tusonge mbele”9 tukiwa Naye kando yetu, tukitumaini kwamba baraka Zake zilizoahidiwa zitakuja. Maandiko hutukumbusha kwamba mara nyingi baraka hizo huja katika wakati Wake na kwa njia Yake: Miaka 38.11 miaka 12,12 papo hapo.13 Kadiri njia itakavyokuwa na mahitaji, ndivyo usaidizi Wake utakavyokuwa.14
Yake ni misheni ya upendo. Yesu Kristo atakutana nasi pale tulipo na jinsi tulivyo. Hii ndiyo kwa nini ya bustani, msalaba na kaburi. Mwokozi alitumwa atusaidie tushinde.15 Lakini kubaki pale tulipo hakutaleta ukombozi tunaoutafuta. Kama vile ambavyo hakumwacha Yakobo mavumbini, Bwana hatarajii kumwacha yeyote kati yetu pale tulipo.
Yake pia ni misheni ya kuinua. Atafanya kazi ndani yetu16 ili kutuinua mpaka pale Yeye alipo na, kwenye mchakato, anatuwezesha tuwe jinsi Yeye alivyo. Yesu Kristo alikuja kutuinua.17 Yeye anataka kutusaidia tuwe. Hii ndiyo kwa nini ya hekalu.
Lazima tukumbuke: si njia pekee itakayotuinua, ni mwenza—Mwokozi wetu. Na hii ndiyo kwa nini ya uhusiano wa agano.
Nilipokuwa Israeli, nilizuru Ukuta wa Kaskazini. Kwa Wayahudi, hili ni eneo takatifu zaidi katika Israeli. Ndicho chote kilichobakia kwenye hekalu lao. Wengi huvalia nguo zao nzuri wanapotembelea eneo hili takatifu; uchaguzi wao wa nguo ni ishara ya kujitoa kwao katika uhusiano wao na Mungu. Wanazuru ukuta kusoma maandiko, kuabudu, na kumimina sala zao. Ombi kwa ajili ya hekalu katikati yao huchukua kila siku yao, kila sala yao, tamanio lao la nyumba ya agano. Ninavutiwa na kujitoa kwao.
Niliporejea nyumbani kutoka Israeli, nilisikiliza kwa ukaribu sana mazungumzo yanayonizunguka kuhusu maagano. Niligundua watu wakiuliza, kwa nini nitembee njia ya agano? Je, ninahitaji kuingia ndani ya nyumba kwa ajili ya kufanya maagano? Kwa nini ninavaa gamenti takatifu? Je, ninapaswa kuwekeza kwenye uhusiano wa agano na Bwana? Jibu la maswali haya mazuri na muhimu ni rahisi: inategemea na kiwango gani cha uhusiano unaotaka kuwa nao na Yesu Kristo.18 Kila mmoja wetu atapaswa kugundua jibu letu wenyewe kwa maswali hayo binafsi ya kina.
Hili ndilo langu: niinatembea njia hii kama binti “mpendwa wa wazazi wa mbinguni,”19 ambaye ninajulikana kiungu20 na kuaminiwa kwa kina.21 Kama mtoto wa agano, ninastahili kupokea baraka zilizoahidiwa22. Mimi nimechagua23 kutembea pamoja na Bwana. Mimi nimeitwa24 kusimama kama shahidi wa Kristo. Wakati njia inapoonekana kuchosha, ninatiwa nguvu25 kwa neema wezeshi. Kila mara ninapoingia ndani ya nyumba Yake, ninapata uzoefu wa uhusiano wa kina wa agano pamoja na Yeye. Mimi ninatakaswa26 kwa Roho Wake, kuzawadiwa27 vipawa vyake na kuwekwa wakfu28 ili kuujenga ufalme Wake. Kupitia mchakato wa toba ya kila siku na kupokea sakramenti kila wiki, ninajifunza kuwa imara29 na kuzunguka huku na huko nikitenda mema.30 Ninatembea njia hii na Yesu Kristo, nikitazamia siku iliyoahidiwa ambapo Yeye atakuja tena. Ndipo nitafungwa kuwa Wake31 na kuinuliwa juu kama binti mtakatifu32 wa Mungu.
Hii ndiyo sababu ninatembea njia ya agano.
Hii ndiyo sababu ninang’ang’ania ahadi za agano.
Hii ndiyo sababu ninaingia nyumba Yake ya agano.
Hii ndiyo sababu ninavaa gamenti takatifu kama ukumbusho daima.
Kwa sababu ninataka kuishi kwenye msimamo wa uhusiano wa agano pamoja Naye.
Pengine unataka hivyo pia. Anzia pale ulipo.33 Usiruhusu hali yako ikuzuie. Kumbuka, kasi au kujiweka kwenye njia si muhimu kama kupiga hatua.34 Muulize mtu unayemwamini ambaye yuko kwenye njia ya agano akutambulishe kwa Mwokozi ambaye wamemjua. Jifunze zaidi kumhusu Yeye. Wekeza kwenye uhusiano kwa kuingia kwenye agano Naye. Haijalishi umri wako au hali yako. Unaweza kutembea pamoja na Yeye.
Baada ya kumaliza kutembea Njia ya Yesu, Mya hakutwaa kamba yake. Aliiacha imefungwa kwenye skuta yangu. Kwa siku chache zilizofuata wapwa wangu vijana na rafiki zao walifanya zamu kunivuta katika mitaa ya Yerusalemu.35 Walihakikisha sikukosa hadithi za Yesu. Nilikumbushwa nguvu za kizazi chipukizi. Tunaweza kujifunza kutoka kwenu. Mna hamu ya kweli ya kumjua mwongozaji, Yesu Kristo. Tumainieni nguvu ya kamba inayotuvuta Kwake. Mna vipawa vya kuwaongoza wengine Kwake.36
Ninashukuru, tunatembea njia hii pamoja, tukiomba kutiwa moyo njiani.37 Tunaposhiriki uzoefu wetu binafsi pamoja na Kristo tutaimarisha msimamo binafsi. Juu ya hili, ninatoa ushahidi katika jina la Yesu Kristo, amina.