Kuweni Wafuasi wa Amani wa Kristo
Ninashuhudia kwamba “wafuasi wa amani wa Kristo” watapata amani ya binafsi katika maisha haya na muunganiko mtukufu wa mbinguni.
Sisi tunaishi katika wakati ambao “wafuasi wa amani wa Kristo”1 wanakumbana na changamoto za kipekee. Wale wanaoamini katika, kuabudu kwa unyenyekevu na kushuhudia juu ya Yesu Kristo mara zote wamekumbana na majaribu, taabu na dhiki.2 Mimi pamoja na mke wangu, Mary, si wa tofauti. Katika miaka michache iliyopita, tumeona marafiki zetu wengi wa karibu wa shule ya upili na wenzi wetu wamisionari, baadhi ya wake wao wa thamani, na wafanyakazi wenza wa awali wakifariki dunia au, kama Rais Russell M. Nelson alivyosema, kuhitimu hadi upande mwingine wa pazia. Tumeona baadhi ya waliolelewa katika imani na tumaini wakitoka kwenye njia ya agano.
Cha kusikitisha, tulipoteza mjukuu wa kiume wa miaka 23 ambaye alikufa katika ajali mbaya ya gari. Baadhi ya marafiki wapendwa, wanafamilia na wenza wetu pia wamepatwa na changamoto kali za afya.
Wakati majaribu yanapotokea, tunaomboleza na kujitahidi kubebeana mizigo.3 Tunaomboleza kwa mambo ambayo hayatatimia na nyimbo ambazo hazitaimbwa.4 Mambo mabaya hutokea kwa watu wema katika safari hii ya maisha. Moto mkali huko Maui Hawaii, Chile kusini na Kanada mashariki ni mifano ya matukio ya kutisha ambayo watu wema wakati mwingine hukabiliana nayo.
Tunasoma katika Lulu ya Thamani Kuu kwamba Bwana alimfunulia Ibrahimu asili ya milele ya roho. Ibrahimu alijifunza juu ya maisha yetu ya kabla ya dunia, kuteuliwa kabla, Uumbaji, kuchaguliwa kwa Mkombozi, na maisha haya ya duniani, ambayo ni hali ya pili ya mwanadamu.6 Mkombozi alitangaza:
“Tutaifanya dunia mahali ambapo hawa watapata kukaa;
“Nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru.”6
Sasa sisi sote tuko hapa katika hali ya pili ya safari yetu ya kusonga mbele kuelekea ufalme wa utukufu kama sehemu ya mpango mkuu wa Mungu wa wokovu na kuinuliwa. Tumebarikiwa na haki ya kujiamulia na tunakabiliwa na majaribu ya maisha ya duniani. Huu ndio muda uliotengwa kwa ajili yetu kujitayarisha kukutana na Mungu.7 Tumebarikiwa kumjua Yesu Kristo na jukumu Lake katika mpango huo. Tunayo fursa ya kuwa waumini wa Kanisa Lake la urejesho—Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kama wafuasi wa amani wa Kristo, tunajitahidi kuishi amri Zake. Haijawahi kuwa rahisi kwa wafuasi Wake. Wala haikuwa rahisi kwa Mwokozi kutimiza kwa uaminifu misheni Yake ya duniani.
Maandiko yako wazi: wengi wataangukia kwenye mtazamo wa “kula, kunywa, na kushangilia, kwa maana kesho tutakufa”.8 Wasioamini wengine hurejea kwenye makundi ya giza ya washiriki wenye nia moja wanaotetea “jambo jipya linalofuata”9 na falsafa za wanadamu.10 Hawajui mahali pa kupata ukweli.11
Wafuasi wa amani wa Kristo hawafuati njia zozote zile. Sisi ni wachangamfu, wanaoshiriki katika jumuiya tunamoishi. Tunapenda, tunashiriki na kuwaalika watoto wote wa Mungu kufuata mafundisho ya Kristo.12 Tunafuata ushauri wa nabii wetu mpendwa, Rais Nelson: tunachagua nafasi ya mtunza amani, sasa na siku zote.13 Mtazamo huu uliovuviwa unapatana na maelekezo ya maandiko na unabii.
Mnamo 1829 Kanisa lililorejeshwa lilikuwa bado halijaanzishwa, wala Kitabu cha Mormoni kilikuwa hakijachapishwa. Kikundi kidogo cha watu waliokuwa wakihangaika, wakiongozwa na Roho wa Mungu, walimfuata Nabii Joseph Smith. Bwana alimfunulia Joseph ushauri wa nyakati ngumu: “Msiogope, enyi kundi dogo; tendeni mema; acha dunia na jahanamu ziungane dhidi yenu, kwani kama mmejengwa juu ya mwamba wangu, haziwezi kuwashinda.”14 Yeye pia anawashauri wao:
“Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.
“… Kuweni waaminifu, zishikeni amri zangu, na mtaurithi ufalme wa mbinguni.”15
Ni wazi kwamba, hatima yetu ya mbinguni haibadilishwi tunapopatwa na dhiki. Katika Waebrania tunashauriwa “kukikaribia kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”16 Yesu Kristo ni “sababu ya wokovu wa milele.”17
Ninapenda maneno ya Mormoni, yaliyonukuliwa na mwanawe Moroni, akipongeza “wafuasi wa amani wa Kristo … kwa sababu ya kutembea kwenu kwa amani pamoja na watoto wa watu.”18
Kwa wale kati yetu katika Kanisa tunaojitahidi kuwa “wafuasi wa amani wa Kristo,” siku angavu zaidi inatungoja tunapofokasi kwa Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Majaribu ni sehemu ya maisha ya duniani na hutokea katika maisha ya kila mtu duniani kote. Hii ni pamoja na migogoro mikubwa kati ya nchi na watu binafsi.
Viongozi wa kanisa huulizwa mara kwa mara, “Kwa nini Mungu mwenye haki anaruhusu mambo mabaya yatokee, hasa kwa watu wazuri?” na “Kwa nini wale wenye haki na wako katika utumishi wa Bwana hawana kinga dhidi ya majanga hayo?”
Hatujui majibu yote; hata hivyo, tunajua kanuni muhimu zinazoturuhusu kupitia majaribu, taabu na dhiki kwa imani na uthabiti kwa matumaini ya kesho nzuri inayomngojea kila mmoja wetu. Hakuna mfano bora zaidi uliopo katika maandiko kuhusiana na kupita katika dhiki kuliko neno la Bwana kwa Joseph Smith, Nabii, alipokuwa mfungwa katika Jela ya Liberty.
Bwana kwa sehemu alitamka:
“Kama mataya yale ya jahanamu yataachama kinywa wazi kwa ajili yako, fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako.
“Mwana wa Mtu amejishusha chini yao wote. Je, wewe u mkuu kuliko yeye?
“… Usiogope mwanadamu awezacho kukutenda, kwani Mungu atakuwa pamoja nawe milele na milele.19
Ni wazi tuna Baba wa Mbinguni ambaye anatujua na anatupenda sisi binafsi na kuelewa mateso yetu kikamilifu. Mwanawe, Yesu Kristo, ni Mwokozi na Mkombozi wetu.
Rais Russell M. Nelson na Rais M. Russell Ballard wote walisisitiza sana umuhimu wa toleo jipya la pili la Hubiri Injili Yangu.20 Mimi ninashiriki ari yao. Toleo hili jipya, linalokuza andiko takatifu, linatangaza kwa nguvu:
“Katika dhabihu Yake ya upatanisho, Yesu Kristo alichukua juu Yake maumivu yetu, mateso na udhaifu. Kwa sababu ya hili, Yeye anajua ‘kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na udhaifu wao’ (Alma 7:12; ona pia mstari wa 11). Yeye anatualika, ‘Njooni kwangu,’ na tunapofanya hivyo, Yeye hutupatia pumziko, tumaini, nguvu, mtazamo na uponyaji (Mathayo 11:28; ona pia mstari wa 29–30).
“Tunapomtegemea Yesu Kristo na Upatanisho Wake, Anaweza kutusaidia kuvumilia majaribu yetu, magonjwa na uchungu. Tunaweza kujazwa na furaha, amani, na faraja. Yale yote ambayo si haki juu ya maisha yanaweza kufanywa kuwa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.”21
Tunaweza kwa furaha kuwa wafuasi wa amani wa Kristo.
Mpango wa furaha wa Baba yetu kwa watoto Wake haujumuishi tu maisha ya kabla ya duniani na maisha ya duniani lakini pia uwezekano wa uzima wa milele, ikijumuisha muungano mkuu na mtukufu pamoja na wale ambao tumewapoteza. Makosa yote yatasahihishwa, na tutaona kwa uwazi kamili na mtazamo na uelewa usio na dosari.
Viongozi wa Kanisa wamelinganisha mtazamo huu na mtu anayeingia katikati ya mchezo wa kuigiza wenye matukio matatu.22 Wale wasio na maarifa ya mpango wa Baba hawaelewi kile kilichotokea katika tukio la kwanza au maisha kabla ya kuja duniani na madhumuni yaliyowekwa huko; wala hawaelewi ufafanuzi na azimio ambalo huja katika tukio la tatu, ambalo ni utimilifu mtukufu wa mpango wa Baba.
Wengi hawathamini kwamba chini ya mpango Wake wa upendo na mpana, wale wanaoonekana kuwa wasio na uwezo, bila kosa lao wenyewe, hawaathiriwi hatimaye.23
Maandiko yako wazi: wafuasi wa amani wa Kristo ambao ni waadilifu, wanaomfuata Mwokozi na kushika amri Zake watabarikiwa. Mojawapo ya maandiko muhimu zaidi kwa wale walio waadilifu, bila kujali hali zao maishani, ni sehemu ya hotuba ya Mfalme Benjamini kwa watu wake. Anaahidi kwamba wale wanaoshika amri kwa uaminifu wanabarikiwa katika mambo yote katika maisha haya na “wanapokelewa mbinguni … [na] kuishi na Mungu katika hali ya furaha isiyo na mwisho.”24
Tunatambua kwamba karibu sisi sote tumepitia dhoruba za kimwili na za kiroho maishani mwetu, nyingine zenye kuharibu. Baba mwenye upendo wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, ambaye ni mkuu wa Kanisa Lake lililorejeshwa, wametupatia maandiko na manabii ili kututayarisha, kutuonya kuhusu hatari, na kutupa mwongozo wa kututayarisha na kutulinda. Maelekezo mengine yanahitaji hatua ya haraka, na mengine hutoa ulinzi kwa miaka mingi katika siku zijazo. Dibaji ya Bwana kwenye Mafundisho na Maagano, sehemu ya 1, inatuonya sisi “kuzingatia maneno ya manabii.”25
Sehemu ya 1 pia inatutahadharisha, “Jitayarisheni, jitayarisheni kwa lile ambalo laja.”26 Bwana huwapa watu Wake nafasi ya kujitayarisha kwa ajili ya changamoto watakazokabiliana nazo.
Bwana alitoa ufunuo wenye nguvu kwa Rais Brigham Young mnamo Januari 14, 1847, huko Winter Quarters.27 Ufunuo huu ni mfano halisi wa Bwana akiwatayarisha watu kwa yale yajayo. Watakatifu waaminifu walikuwa wameanza safari yao ya kwenda kwenye kimbilio la mlimani la Bonde la Salt Lake. Walikuwa wamefanikiwa kujenga Hekalu la Nauvoo na kupokea ibada takatifu za kuokoa. Walikuwa wamefukuzwa kutoka Missouri, na watesi wao walikuwa wamewafukuza kutoka Nauvoo katika msimu wa baridi kali. Ufunuo kwa Brigham ulitoa ushauri wa vitendo kuhusu jinsi ya kujiandaa kwa ajili ya kutoka. Bwana aliweka msisitizo maalumu kuhusu kuwatunza masikini, wajane, yatima na familia za wale wanaohudumu katika Kikosi cha Mormoni kama kundi kuu la Watakatifu walioendelea na safari yao ya hatari.
Mbali na kutoa ushauri mwingine wa kuishi kwa uadilifu, Bwana alikazia kanuni mbili zinazoendelea kutumika leo.
Kwanza, Aliwahimiza “kumsifu Bwana kwa kuimba, kwa kinubi, kwa kucheza, na kwa sala ya kusifu na kutoa shukrani.”28
Pili, Bwana alishauri kama walikuwa na “huzuni, wamlingane Bwana Mungu wao, kwa maombi ya dhati, ili mioyo yao ipate kufurahi.”29
Mawaidha haya mawili ni ushauri mkuu kwa siku zetu wenyewe. Maisha yaliyojaa sifa, muziki na shukrani yamebarikiwa kipekee. Kuwa na furaha na kutegemea usaidizi wa mbinguni kupitia maombi ni njia yenye nguvu ya kuwa wafuasi wa amani wa Kristo. Kujitahidi kila wakati kuwa na moyo mkunjufu husaidia kuepuka kuwa na huzuni.
Mstari wa mwisho wa wimbo wa mtazamo huu unatoa jibu la mwisho katika mtindo mzuri: “Ulimwengu hauna huzuni ambayo mbingu haiwezi kuponya.”30
Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninashuhudia kwamba “wafuasi wa amani wa Kristo” watapata amani ya binafsi katika maisha haya na muunganiko mtukufu wa mbinguni. Ninatoa ushuhuda wa hakika wa uungu wa Mwokozi na uhalisia wa Upatanisho Wake. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.