Bwana, Tungependa Kumwona Yesu
Sisi tunataka kumwona Yesu jinsi Yeye alivyo na kuhisi upendo Wake.
Upofu wa Kutambua Uso
Siku moja katika majira ya kuchipua ya 1945, kijana mmoja aliamka katika hospitali ya kijeshi. Alikuwa na bahati ya kuwa hai—alikuwa amepigwa risasi nyuma ya sikio, lakini madaktari walimfanyia upasuaji, na sasa angeweza kutembea na kuzungumza kawaida.
Kwa bahati mbaya, risasi hiyo iliharibu sehemu ya ubongo wake uliotambua nyuso. Sasa anamtazama mkewe bila chembe ya utambuzi; hakuweza kumtambua mama yake mwenyewe. Hata sura kwenye kioo ilikuwa ngeni kwake—hakuweza kujua ikiwa ni ya mwanaume au mwanamke.1
Amekuwa kipofu wa kutambua nyuso—hali inayoathiri mamilioni ya watu.2
Watu ambao wana upofu wa kutambua uso hujaribu kuwatambua wengine kwa kukariri sheria—sheria ya kumtambua binti kwa kovu lake au rafiki kwa mtembeo wa kuburuza miguu.
Kukua
Hapa kuna hadithi ya pili, karibu na nyumbani: Kama mvulana mdogo, mara nyingi nilimwona mama yangu kama mtunga sheria. Aliamua wakati ningeweza kucheza na wakati gani kwenda kulala au, vibaya zaidi, kuondoa magugu kwenye uwanja.
Ni wazi yeye alinipenda. Lakini mara nyingi sana na kwa aibu yangu, nilimwona tu kuwa “Yeye Ambaye Ni Lazima Atiiwe.”
Miaka kadhaa baadaye ndipo nilipomwona kama mtu halisi. Nina aibu kusema kwamba kamwe sikuwahi kutambua dhabihu yake au kujiuliza ni kwa nini kwa miaka mingi aliweza kuvaa sketi zile zile mbili kuu kuu (huku mimi nikipata nguo mpya za shule) au kwa nini, baada ya siku kwisha, alichoka sana na alitaka nilale mapema.
Tunaweza Kuwa Vipofu wa Kutambua Uso
Labda umegundua kwamba hadithi hizi mbili kwa kweli ni hadithi moja—kwa miaka mingi sana, nilikuwa na upofu wa kutambua uso. Nilishindwa kumuona mama yangu kama mtu halisi. Niliona sheria zake lakini sikuziona katika upendo wake.
Ninakuambia hadithi hizi mbili ili kutoa hoja moja: ninashuku kwamba unamfahamu mtu fulani (labda ni wewe ndiyo huyo mtu) ambaye anaugua aina fulani ya upofu wa utambuzi wa uso wa kiroho.
Unaweza kusumbuka kumwona Mungu kama Baba mwenye upendo. Unaweza kutazama mbinguni na kuona sio uso wa upendo na rehema lakini mzigo wa sheria ambazo lazima zipitie njia yako. Labda unaamini kwamba Mungu anatawala katika mbingu Zake, anazungumza kupitia manabii Wake na anampenda dada yako, lakini kwa siri unashangaa kama anakupenda wewe.3 Labda umehisi fimbo ya chuma katika mkono wako lakini bado hujahisi Upendo wa Mwokozi wako unaelekea wapi.4
Nadhani mnawajua watu kama hawa kwa sababu kwa muda mrefu, nilikuwa mtu kama huyu—nilikuwa na upofu wa uso wa kiroho.
Nilidhani maisha yangu yalikuwa kufuata tu sheria na kujilinganisha na viwango vya dhahania. Nilijua Mungu alikupenda wewe kikamilifu lakini binafsi sikuhisi hilo. Nina hofu kwamba niliwaza zaidi kufika mbinguni kuliko kuwa na Baba yangu wa Mbinguni.
Ikiwa wewe, kama mimi, wakati mwingine unachezesha midomo tu lakini “huimbi wimbo wa upendo wa ukombozi,”5 tunaweza kufanya nini?
Jibu, kama Rais Russell M. Nelson anavyotukumbusha, daima ni Yesu.6 Na hiyo ni habari nzuri sana.
Bwana, Tungependa Kumwona Yesu
Kuna mstari mfupi katika Yohana ambao ninaupenda. Mstari unasimulia juu ya kundi la wayunani wanaomwendea mwanafunzi wa Yesu wakiwa na ombi muhimu. “Bwana,” wanasema, “sisi [tungependa] kumwona Yesu.”7
Hilo ndilo sote tunalotaka—tunataka kumwona Yesu jinsi Yeye alivyo na kuhisi upendo Wake. Hii inapaswa kuwa sababu ya karibu kila kitu tunachofanya kanisani—na hasa katika kila mkutano wa sakramenti. Ikiwa unajiuliza ni aina gani ya somo la kufundisha, ni aina gani ya mkutano wa kupanga na kama ukate tamaa juu ya mashemasi na kucheza mpira wa kukwepa, unaweza kuchukua mstari huu kama mwongozo wako: je, hii itasaidia watu kumwona na kumpenda Yesu Kristo? Na kama sio, basi jaribu kitu kingine.
Nilipotambua kwamba nilikuwa na upofu wa uso wa kiroho, kwamba niliona sheria na sio uso wa neema ya Baba, nilijua hili halikuwa tatizo la Kanisa. Wala si la Mungu, na haikumaanisha kila kitu kilipotea; ni jambo ambalo sisi sote tunapaswa kujifunza. Hata mashahidi wa mwanzo wa Ufufuko mara nyingi walikutana uso kwa uso na Bwana aliyefufuka na lakini hawakumtambua; kutoka Kaburi la Bustanini mpaka pwani ya Galilaya, wafuasi Wake wa kwanza “walimwona Yesu amesimama, wala hawakujua ya kuwa ni Yesu.”8 Ilibidi wajifunze kumtambua Yeye, nasi vivyo hivyo.9
Hisani
Nilipotambua nilikuwa mpofu kiroho nilianza kufuata ushauri wa Mormoni wa kuomba “kwa nguvu zote za moyo” ili kujazwa na upendo ulioahidiwa kwa wafuasi Wake—upendo wangu Kwake na upendo Wake kwangu—na “kumwona jinsi alivyo … na kuwa na tumaini hili.”10 Niliomba kwa miaka mingi ili kuweza kufuata amri kuu ya kwanza ya kumpenda Mungu na kuhisi kwamba “ukweli ukweli mkuu wa kwanza … ni kwamba Mungu anatupenda sisi kwa moyo Wake wote, nguvu, akili na uwezo.”11
Injili
Pia nilisoma na kusoma tena na kusoma tena Injili kuu nne—wakati huu haikuwa kwa ajili ya kudondoa sheria Zake bali kuona Yeye ni nani na kipi Yeye hukipenda. Na, punde, nilisombwa na mto wa upendo uliotiririka kutoka Kwake.
Yesu alitangaza mwanzoni, kwamba Yeye alikuja “kuwaponya waliovunjika moyo, kuwatangazia wafungwa uhuru wao, na vipofu kupata kuona tena.”12
Hiyo haikuwa tu orodha ya mambo ya kufanya au mahusiano mazuri ya umma; ndiyo umbo la upendo Wake.
Fungua Injili bila mpangilio; karibu katika kila ukurasa tunamwona Yeye akiwatunza watu wanaoteseka—kijamii, kiroho, na kimwili. Aliwagusa watu waliochukuliwa kuwa najisi na wasio wasafi13 na kuwalisha wenye njaa.14
Ni hadithi gani pendwa kwako kuhusu Yesu Kristo? Nadhania inamuonyesha Mwana wa Mungu akinyoosha mkono kumkumbatia au kutoa tumaini kwa mtu mnyonge—mkoma,15 Msamaria anayechukiwa,16 mwenye dhambi aliyetuhumiwa na mwenye kashfa,17 au adui wa taifa.18 Rehema ya aina hiyo inashangaza.
Jaribu kuandika kila wakati Yeye anaposifia au kuponya au kula na mtu wa nje, na utapungukiwa na wino kabla ya kumaliza kitabu cha Luka.
Nilipoona hili, moyo wangu uliruka katika utambuzi wa upendo, na nikaanza kuhisi kwamba Yeye angeweza kunipenda. Kama vile Rais Nelson alivyofundisha, “Kadri unavyojifunza zaidi juu ya Mwokozi, ndivyo itakavyokuwa rahisi kutumaini rehema Yake, upendo Wake usio na kikomo.”19 Na ndivyo utakavyomwamini na kumpenda zaidi Baba yako wa Mbinguni.
Mzee Holland ametufundisha kwamba Yesu alikuja kutuonyesha “Mungu Baba yetu wa Milele ni nani na yuko vipi, jinsi Yeye alivyojitoa kikamilifu kwa watoto Wake katika kila umri na taifa.”21
Paulo alisema Mungu ni “Baba wa rehema [zote], na Mungu wa faraja yote.”21
Kama unamwona Yeye kwa njia tofauti, tafadhali endelea kujaribu.
Maagano na Kumbatio la Mungu
Manabii hutualika kutafuta uso Wake.22 Ninachukulia hili kama ukumbusho kwamba tunamwabudu Baba yetu, sio kanuni, na kwamba hatufiki tamati mpaka tumwone Yesu kama uso wa upendo wa Baba yetu;23 na tumfuate Yeye, si tu amri Zake.24
Wakati manabii na mitume wanapozungumza kuhusu maagano, wao si kama makocha wanaopiga kelele kutoka benchini, wakituambia “tujaribu zaidi!” Wanatutaka sisi tuone maagano yetu kimsingi ni kuhusu mahusiano25 na yanaweza kuwa tiba ya upofu wa uso wa kiroho.26 Sio sheria za kupata upendo Wake; Yeye tayari anakupenda kikamilifu. Changamoto yetu ni kuelewa na kuyafinyanga maisha yetu kuwa upendo huo.27
Tunajaribu kuona kupitia maagano yetu, kama vile dirishani, kwenye uso nyuma ya rehema ya Baba.
Maagano ndiyo umbo la kumbatio la Mungu.
Mto wa Upendo wa Mungu
Hatimaye, tunaweza kujifunza kwa kumwona Yeye kwa kumtumikia Yeye. “Kwani mtu awezaje kumjua bwana ambaye hajamtumikia?”28
Miaka michache iliyopita, nilipata wito ambao sikuufurahia. Niliamka mapema, nikiwa na wasiwasi—lakini nikiwa na msemo akilini ambao sikuwahi kuusikia hapo awali: kwamba kuhudumu katika Kanisa hili ni kusimama katika mto wa upendo wa Mungu kwa watoto Wake. Kanisa hili ni jamii ya watu wachapakazi wenye sururu na sepeto, wakijaribu kusaidia kusafisha njia ya mto wa upendo wa Mungu kuwafikia watoto Wake mwishoni mwa mstari.
Bila kujali wewe ni nani, jana yako, kuna nafasi yako katika Kanisa hili.29
Chukua sururu na sepeto na ujiunge na timu. Saidia kubeba upendo Wake kwa watoto Wake na baadhi ya upendo huo utarejea kwako.30
Na tutafute uso Wake wa upendo, kumbatio Lake la agano, na kisha kuungana mkono kwa mkono na watoto Wake, na kwa pamoja tutaimba “Mkombozi wa Israeli”:
Nirejeshee, Mwokozi
Nuru yako;
Faraja ya roho nipe;
Na ile shauku
ya kuja kwako
Moyo tumaini iipe.31
Na tutafute uso Wake wa upendo na tuwe vyombo vya rehema Zake kwa watoto Wake.32 Katika jina la Yesu Kristo, amina.