Masomo ya Uzazi wa Kiungu
Wazazi wanaingia katika ushirikiano na Baba yao wa Mbinguni ili kuwaongoza watoto wao wa thamani kurudi mbinguni.
Je, umewahi kumshika mtoto mchanga mikononi mwako? Kuna nuru inayotoka kwa kila mtoto mchanga, ikileta muunganiko maalumu wa upendo ambao unaweza kujaza mioyo ya wazazi wao kwa shangwe.1 Mwandishi mmoja kutoka Mexico aliandika hivi: “Nimejifunza kwamba mtoto mchanga anapobana kidole cha baba yake kwenye ngumi yake ndogo, anakuwa amemshika baba yake milele.”2
Uzazi ni mojawapo ya uzoefu wa kipekee zaidi maishani. Wazazi wanaingia katika ushirikiano na Baba yao wa Mbinguni ili kuwaongoza watoto wao wa thamani kurudi mbinguni.3 Leo ningependa kushiriki baadhi ya masomo ya uzazi yanayopatikana katika maandiko na kufundishwa na manabii walio hai ili kutusaidia tuache urithi wetu wa uzazi.
Kwea Mpaka Uwanda wa Juu zaidi wa Utamaduni wa Injili
Ni lazima tukwee kwenye uwanda wa juu zaidi wa utamaduni wa injili pamoja na familia zetu. Rais Russell M. Nelson alitangaza: “Familia zinastahili mwongozo kutoka mbinguni. Wazazi hawawezi kuwashauri watoto vya kutosha kutoka kwenye uzoefu binafsi, woga au huruma.”4
Ingawa asili zetu za kitamaduni, mitindo ya malezi na uzoefu binafsi vinaweza kuwa muhimu kwa malezi, uwezo huu hautoshi kuwasaidia watoto wetu kurudi mbinguni. Tunahitaji ufikiaji wa “seti iliyoinuliwa zaidi ya maadili na … desturi,”5 utamaduni wa upendo na matarajio, ambapo tunachangamana na watoto wetu “katika njia ya juu zaidi, takatifu zaidi.”6 Rais Dallin H.Oaks alielezea utamaduni wa injili kama “njia ya kipekee ya maisha, seti ya maadili na matarajio na desturi. … Utamaduni huu wa injili unatokana na mpango wa wokovu, amri za Mungu na mafundisho ya … manabii walio hai. Utamaduni huu hutuongoza katika jinsi tunavyolea familia zetu na kuishi maisha yetu binafsi.”7
Yesu Kristo ndiye kiini cha utamaduni huu wa injili. Kukubali utamaduni wa injili katika familia zetu ni muhimu kwa kujenga mazingira yenye rutuba ambapo mbegu ya imani inaweza kustawi. Ili kupanda hadi uwanda wa juu, Rais Oaks alitualika “kuacha mila au desturi zozote binafsi au za familia ambazo ni kinyume na mafundisho ya Kanisa la Yesu Kristo.”8 Wazazi, vitisho kwa upande wetu kwa lengo la kuanzisha utamaduni wa injili vinaweza kumruhusu adui kuweka msingi katika nyumba zetu au, mbaya zaidi, katika mioyo ya watoto wetu.
Tunapochagua kufanya utamaduni wa injili kuwa utamaduni mkuu katika familia yetu, basi kwa ushawishi mkubwa wa Roho Mtakatifu,9 mitindo yetu ya sasa ya malezi, mila na desturi vitapepetwa, kupangiliwa, kuboreshwa na kuimarishwa.
Fanya Nyumbani Pawe Kiini cha Kujifunza Injili
Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba nyumbani panapaswa kuwa “kiini cha kujifunza injili.”10 Dhumuni la kujifunza injili ni “kuongeza uongofu wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kutusaidia sisi tuwe zaidi kama Wao.”11 Hebu tuchunguze majukumu matatu muhimu ya uzazi yaliyoelezwa na manabii na mitume ambayo yanaweza kutusaidia tuanzishe utamaduni wa juu wa injili katika nyumba zetu.
Kwanza: Fundisha kwa Uhuru
Baba wa Mbinguni alimpa mwongozo Adamu kuhusu Yesu Kristo na mafundisho Yake. Alimfundisha “kuwafundisha watoto [wake] vitu hivi kwa uhuru.”12 Kwa maneno mengine, Baba wa Mbinguni alimfundisha Adamu kufundisha mambo haya kwa uhuru, kwa ukarimu, na bila kizuizi.13 Maandiko yanatuambia kwamba “Adamu na Hawa walilibariki jina la Mungu, na wakafanya vitu vyote vijulikane kwa wana wao na mabinti zao.”14
Tunawafundisha watoto wetu kwa ukarimu pale tunapotumia wakati mzuri pamoja nao. Tunafundisha bila vizuizi pale tunapojadili mada nyeti kama vile muda wa kutazama runinga, kutumia nyenzo ambazo Kanisa limetoa.15 Tunafundisha kwa uhuru pale tunapojifunza maandiko pamoja na watoto wetu tukitumia Njoo, Unifuate na kumruhusu Roho kuwa mwalimu.
Pili: Kielelezo cha Ufuasi
Katika kitabu cha Yohana, tunasoma kwamba Wayahudi kadhaa walipomwuliza Mwokozi kuhusu mwenendo Wake, Yesu alielekeza umakini kwa mtu ambaye ni kielelezo Chake, Baba Yake. Alifundisha, “Mwana hawezi kufanya neno mwenyewe, ila lile ambalo amwona Baba analitenda.”16 Wazazi, ni kipi tunahitaji kuwa kielelezo kwa watoto wetu? Ufuasi.
Kama wazazi, tunaweza kufundisha umuhimu wa kumweka Mungu kwanza wakati tunapojadili amri ya kwanza, lakini tunakuwa kielelezo tunapoweka kando vivuruga mawazo vya kiulimwengu na kuitakasa siku ya Sabato kila juma. Tunaweza kufundisha umuhimu wa maagano ya hekaluni wakati tunapozungumza kuhusu fundisho la ndoa ya selestia, lakini tunakuwa kielelezo tunapoheshimu maagano yetu, tukiwatendea wenzi wetu kwa utu.
Tatu: Alika Kutenda
Imani katika Yesu Kristo inapaswa kuwa kiini cha shuhuda za watoto wetu, na shuhuda hizi lazima zije kwa kila mtoto kwa njia ya ufunuo binafsi.17 Ili kuwasaidia watoto wetu katika ujenzi wa shuhuda zao, tunawahimiza watumie haki yao ya kujiamulia kuchagua kilicho chema18 na kuwatayarisha kwa maisha yote kwenye njia ya agano ya Mungu.19
Ingekuwa busara kumhimiza kila mmoja wa watoto wetu kukubali mwaliko wa Rais Nelson wa kuwajibika juu ya ushuhuda wake kuhusu Yesu Kristo na injili Yake, kuufanyia kazi, kuutunza ili ukue, kuulisha ukweli, na kutouchafua kwa falsafa za uongo za wanaume na wanawake wasioamini.20
Haki, Malezi Yenye Kusudi
Madhumuni matakatifu ya Baba yetu wa Mbinguni kama mzazi yalifahamishwa katika ufunuo uliotolewa kwa Musa: “Kwani tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”21 Rais Nelson ameongeza, “Mungu atafanya kila awezalo, bila kukiuka haki yako ya kujiamulia, ili kukusaidia wewe usikose baraka kuu zaidi katika milele yote.”22
Kama wazazi, sisi ni mawakala wa Mungu katika utunzaji wa watoto wetu.23 Ni lazima tufanye kila tuwezalo ili kuunda mazingira ambapo watoto wetu wanaweza kuhisi ushawishi Wake wa kiungu.
Baba wa Mbinguni hakukusudia kamwe sisi kama wazazi tuketi kando kama watazamaji, tukitazama maisha ya kiroho ya watoto wetu yakiendelea. Acha nionyeshe wazo hili la uzazi wenye kusudi kwa uzoefu binafsi. Nilipokuwa nikihudhuria Msingi katika tawi dogo huko Guatemala, wazazi wangu walianza kunifundisha kuhusu thamani ya baraka za patriaki. Mama yangu alitenga muda kushiriki uzoefu wake wa kupokea baraka zake za patriaki. Alinifundisha mafundisho yanayohusiana na baraka za patriaki, na alitoa ushuhuda juu ya baraka zilizoahidiwa. Uzazi wake wenye kusudi ulinitia moyo ili niwe na hamu ya kupokea baraka zangu za patriaki.
Nilipokuwa na umri wa miaka 12, wazazi wangu walinisaidia kumtafuta patriaki. Hili lilikuwa jambo la lazima kwa sababu hakukuwa na patriaki katika wilaya tuliyoishi. Nilisafiri kwenda kwa patriaki ambaye alikuwa kwenye kigingi umbali wa kilomita 156. Ninakumbuka waziwazi wakati patriaki alipoweka mikono yake juu ya kichwa changu ili kunibariki. Nilijua kwa uthibitisho wenye nguvu za kiroho, pasipo shaka, kwamba Baba yangu wa Mbinguni alinijua.
Kwa mvulana wa miaka 12 kutoka mji mdogo, hiyo ilimaanisha kila kitu kwangu. Moyo wangu uligeukia kwa Baba yangu wa Mbinguni siku hiyo kwa sababu ya malezi yenye lengo ya mama na baba yangu, na nitawashukuru milele.
Dada Joy D. Jones, Rais Mkuu wa zamani wa Msingi, alifundisha: “Hatuwezi kusubiri mazungumzo kutokea yenyewe tu kwa watoto wetu. Kuongoka kwa bahati siyo kanuni ya injili ya Yesu Kristo.”24 Mialiko yetu ya upendo na yenye mwongozo wa kiungu inaweza kuleta mabadiliko katika jinsi watoto wetu wanavyotumia haki yao ya kujiamulia. Rais Nelson alisisitiza “Hakuna kazi nyingine inayopita ile ya uzazi wenye uadilifu, wenye kusudi!”25
Hitimisho
Wazazi, ulimwengu huu umejaa falsafa, tamaduni na mawazo yanayoshindania usikivu wa watoto wetu. Jengo kubwa na pana hutangaza uanachama wake kila siku kwa kutumia mikondo ya sasa ya vyombo vya habari. “Lakini katika kipawa cha Mwanawe,” nabii Moroni alifundisha, “Mungu ametayarisha njia bora zaidi.”26
Tunaposhirikiana na Mungu kupitia maagano na kuwa mawakala Wake katika malezi ya watoto wetu, Yeye atatakasa nia zetu, atatia msukumo mafundisho yetu na kuchochea mialiko yetu ili “watoto wetu wapate kujua ni chanzo gani wanaweza kutafuta ondoleo la dhambi zao.”27 Katika jina la Yesu Kristo, amina.