Minong’ono ya Roho
Wenza wa daima wa Roho Mtakatifu ni moja ya kipawa kikuu cha kiroho ambacho Watakatifu wa Siku za Mwisho wanakifurahia.
Utangulizi
Hivi karibuni, macho ya ulimwengu wa michezo yalifokasi kwenye Kombe la Dunia la Wanawake la FIFA la mwaka 2023 lililofanyika Australia na New Zealand. Wanariadha wa madaraja ya kimataifa wanaowakilisha timu za mataifa zaidi ya 200 kutoka kote ulimwenguni walionyesha vipaji vyao, kujitolea kwao, talanta na uanariadha walipokuwa wakishindania heshima ya juu kabisa ya ulimwengu wa soka.
Tunastaajabu juu ya wachezaji katika michezo ya aina nyingi na fani zingine ambazo hufikia kiwango cha juu kabisa cha sanaa zao. Tunazungumzia karama au vipawa vyao walivyopewa na Mungu. Hii inajumuisha wale wenye vipaji vya dansi, sarakasi, muziki sanaa, maigizo, hisabati, sayansi na vingine vingi. Kila mtu wa namna hiyo anaonyesha vipaji alivyopewa na Mungu ambavyo kisha huboreshwa na kunolewa kwa juhudi za maisha yote, kujifunza na mazoezi. Karama zitolewazo na Mungu hutengeneza watu walio na vipaji.
Kutumia Karama za Kiroho
Tukitazama kupitia lenzi za injili, Mungu huwajalia watoto Wake karama nyingi za kiroho, vikiwafanya wao wawe watu wenye karama za kiroho. Waumini wa Kanisa wanaoshika maagano wanatunukiwa vipawa vya Kiroho, ambavyo vinajumuisha karama ya ushuhuda wa Yesu Kristo kama Mwokozi wetu, kipawa cha Roho Mtakatifu, karama ya imani ya kuponya na kuponywa, karama ya utambuzi, karama ya kupokea miujiza, karama za hekima na maarifa.1 Bwana anatualika kutafuta kwa dhati karama zilizo bora, hata karama za kiroho. Yeye anatoa karama za kiroho ili kutubariki na ili tuzitumie katika kuwabariki wengine.2
Tukirejea kwenye analojia ya wachezaji wenye vipaji, ni muhimu kukumbuka kwamba karama pekee haimfanyi mtu kuwa mbobezi. Bila kujali ubora wa kipaji cha asili, ni kupitia maumivu na mazoezi makali na juhudi kwamba wachezaji wananoa na kuboresha ufundi wao ili kufikia kiwango cha juu cha ustadi. Hata zawadi zilizopokelewa na kufunguliwa mara nyingi ziliambatana na lugha ya kuogofya “matengenezo yatahitajika.”
Vivyo hivyo, nimeangalia mchirizo wa kujifunza unaohusiana na karama za kiroho. Kutumia karama za kiroho kunahitaji mazoezi ya kiroho. “Kuwa na mwongozo wa Roho Mtakatifu katika maisha yako kunahitaji kazi ya kiroho. Kazi hii inajumuisha sala ya dhati na usomaji endelevu wa maandiko. Pia inajumuisha kushika maagano yako na amri za Mungu. … Inajumuisha kupokea sakramenti kwa kustahili kila wiki.”3
Ni yapi matunda ya kufanyia kazi karama za kiroho? Yanajumuisha minong’ono kutoka kwa Roho ambayo hutusaidia kukabiliana na mahitaji ya kila siku na kutuonyesha kipi cha kufanya na kusema—baraka za amani na faraja. Tunaposikiliza na kutenda kwenye minong’ono ya kiroho, Roho Mtakatifu hukuza uwezo wetu na viwango vyetu kupita kile tunachoweza kufanya sisi wenyewe. Karama hizi za thamani zitatusaidia katika kila kipengele cha maisha yetu.4
Wenza wa daima wa Roho Mtakatifu ni moja ya kipawa kikuu cha kiroho ambacho Watakatifu wa Siku za Mwisho wanakifurahia.
Je, kipawa hiki ni muhimu kiasi gani? Rais Russell M. Nelson amejibu swali hili kwa njia rahisi alipoeleza kwamba “katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila ushawishi wenye mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu.”5
Jinsi ya Kumwalika na Kutambua Minong’ono ya Roho
Katika kipindi cha huduma yangu, nimepata ombi kote ulimwenguni kutoka kwa kila mtu la kutaka kujua namna ya kumwalika na kutambua minong’ono ya Roho Mtakatifu. Minong’ono ya Roho ni ya binafsi na huja katika njia tofauti. Tumebarikiwa, hata hivyo, kuwa na maneno ya manabii, wa kale na wa sasa, yakitupatia utambuzi wa thamani wa jinsi ya kupokea mwongozo kutoka kwa Roho.
Acha nitoe kanuni nne za mwongozo ambazo zinaweza kuwa za msaada kwako katika kumwalika na kutambua minong’ono ya Roho.
Simama katika Mahali Patakatifu
Ya kwanza ni kusimama mahali patakatifu.6 Hivi karibuni nilishiriki katika ufunguzi wa Hekalu la Tokyo Japan. Mapokeo ya mwaliko rasmi uliotumwa kwa vyombo vya habari na kwa wageni maalumu yalipita matarajio. Mamia walishiriki katika matembezi haya ya hekalu. Wageni waliguswa sana na uzuri wa hekalu, ikijumuisha vielelezo na michoro yenye uhusiano wa kina, na utamaduni wa Japani. Kuu zaidi lilikuwa ni unyenyekevu na heshima iliyoonyeshwa kutoka kwa wageni wakati ibada za mababu zilipokuwa zikielezewa katika vyumba ambamo ibada hizi zingefanyika. Lakini cha kugusa moyo zaidi ilikuwa msukumo wa Roho.
Tukio moja nikiwa na afisa mmoja maarufu wa serikali lilibaki katika moyo wangu. Kufuatia wakati wa tafakuri ya kimya katika chumba cha selestia, akiwa ameguswa kwa hisia na kwa kina alinong’ona sikioni mwangu, “Hata hewa ambayo ninavuta katika chumba hiki ni ya tofauti.” Nikatambua anajaribu kuelezea uwepo wa Roho Mtakatifu, ambaye, ndiye, anakaa katika maeneo matakatifu. Kama unatumaini kumhisi Roho, uwe katika mahali ambapo Roho anaweza kuwepo kwa urahisi.
Mahekalu yetu na nyumba zetu ni maeneo yaliyo matakatifu zaidi katika sehemu zilizowekwa wakfu. Ndani yake kwa urahisi zaidi tunamwalika na kumtambua Roho. Maeneo mengine matakatifu yanajumuisha nyumba za mikutano, majengo ya seminari na vyuo, na maeneo ya historia ya Kanisa na vituo vya wageni. Simama katika mahali patakatifu.
Simama na Watu Watakatifu
Pili, simama na watu watakatifu. Nitaelezea kanuni ya pili yenye mwongozo nikitumia kumbukumbu nyingine.
Kamwe sitasahau kushiriki katika ibada iliyofanyika katika uwanja maarufu wa michezo. Kwa kawaida, uwanja huu ulijazwa na mashabiki wakorofi wenye kushangilia timu yao ya nyumbani na pengine hata kuwazomea wapinzani wao. Lakini kwa usiku huu, hali ya hewa ilibadilika sana. Uwanja ulijaa maelfu ya vijana waliokusanyika ili kutoa heshima na kukumbuka maisha ya Nabii Joseph Smith. Toni yao ya staha, ukimya; shukrani; na mioyo iliyojaa sala, iliujaza uwanja kwa uwepo wa Roho Mtakatifu. Ningeweza kuona haya katika nyuso zao. Ilikuwa kipawa cha Roho Mtakatifu katika matendo, akithibitisha shuhuda zilizokuwa zikitolewa juu ya Joseph Smith na Urejesho wa injili.
Roho hawezi kuzuiliwa kuhudhuria kusanyiko la watu watakatifu. Kama unatumaini kumhisi Roho, kuwa na watu ambao Roho anaweza kuwepo kwa urahisi. Mwokozi alilisema hili kwa njia hii: “Kwa kuwa walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, mimi nipo papo hapo katikati yao.”7 Kwa vijana, fikiria mikusanyiko yenu ya watu watakatifu, akidi na madarasa, KNV na seminari, shughuli za kata na kigingi—hata kwaya za kata. Chagua kuwa na watu na kwenda mahali ambapo wema unapatikana. Tafuta nguvu zako kwenye idadi. Tafuta marafiki wazuri. Kuweni marafiki wazuri. Saidianeni popote mlipo. Simama na watu watakatifu.
Shuhudia juu ya Kweli Takatifu
Tatu, shuhudia juu ya kweli takatifu mara nyingi uwezavyo. Mfariji daima anashiriki sauti Yake pale tunaposhuhudia kwa sauti zetu. Roho anatoa ushahidi sawa kwa mzungumzaji na msikilizaji.
Nakumbuka wakati mmoja nilitembea kwa teksi dakika 45 katika Jiji la New York. Baada ya kuwa na mazungumzo matamu ya injili pamoja na dereva kwa wakati wote wa safari yangu ya kwenda uwanja wa ndege, nilimlipa na kujiandaa kushuka. Kisha nilitambua kwamba sikuwa nimetoa ushuhuda wa kile nilichokishiriki. Nilitulia, nikashiriki naye ushuhuda rahisi na mfupi, ukimwalika Roho, na kuleta machozi katika macho yetu sote wawili.
Unapotafuta na kutumia fursa ya kushiriki ushuhuda wako na wengine, utatengeneza nyakati za kumtambua Roho wewe mwenyewe.
Msikilize Roho Mtakatifu
Kanuni ya mwisho ni kumsikiliza Roho Mtakatifu. Yeye anaweza kuwa mwenza wetu daima, lakini anazungumza kwa sauti ndogo, tulivu. Nabii Eliya aligundia kwamba sauti ya Bwana haikuwa katika upepo, tetemeko la nchi, au moto bali ilikuwa “sauti ndogo tulivu.”8 “Si sauti ya radi” badala yake “sauti tulivu ya upole kamili, kama vile mnong’ono”, na bado inaweza “kupenya hata kwenye roho”9
Rais Boyd K. Packer alisema: “Roho hapati usikivu wetu kwa kupiga kelele au kututikisa kwa mkono mzito. Badala yake kwa kunong’ona. Anashawishi kwa upole kiasi kwamba kama tuna shughuli nyingi tunaweza tusimsikie kabisa.”10 Nimetambua kwamba wakati mwingine sauti Yake ni tulivu sana, au kama ninashughulika sana, mpendwa wangu anaipata kwa ajili yangu. Wakati mwingi imetokea wakati minong’ono ya Roho Mtakatifu imekuja kwangu kupitia kwa mke wangu, Lesa. Wazazi au viongozi waadilifu wanaweza pia kupokea mwongozo wenye ushawishi wa kiungu kwa ajili yako.
Kelele, ghasia, na mabishano yaliyozagaa ulimwenguni yanaweza yakaishinda sauti ndogo, tulivu ya Roho Mtakatifu. Tafuta mahali patulivu, sehemu takatifu ambapo unaweza kutafuta kupokea mwongozo kutoka kwa Roho.
Maneno Kadhaa ya Tahadhari
Unapozingatia kanuni hizi za kumwalika na kumtambua Roho, zingatia maneno yafuatayo ya mwongozo wa tahadhari.11
Thibitisha misukumo yako ya kiroho. Kwa mfano, misukumo kutoka kwa Roho itakuwa sambamba na maandiko na mafundisho ya manabii walio hai.
Kuwa na uhakika kwamba hisia unazopokea zinaoana na jukumu lako. Isipokuwa umeitwa kwa mamlaka sahihi, misukumo kutoka kwa Roho haitolewi kwako wewe ili kuwashauri au kuwasahihisha wengine.
Mambo ya kiroho hayalazimishwi. Unaweza kukuza mtazamo na mazingira ambayo yanamwalika Roho, na unaweza kujiandaa wewe mwenyewe, lakini huwezi kulazimisha jinsi gani au lini ushawishi uje. Kuwa mvumilivu na utumaini kwamba utapokea kile unachohitaji wakati muda ukiwa sahihi.
Tumia maamuzi yako mwenyewe yaliyo bora zaidi. Wakati mwingine tunataka kuongozwa na Roho katika mambo yote. Hata hivyo, mara nyingi Bwana anataka sisi tutumie akili tuliyopewa na Mungu na kutenda katika njia ambazo zinaendana na uelewa wetu ulio bora zaidi. Rais Dallin H. Oaks alifundisha:
“Hamu ya kuongozwa na Bwana ni nguvu, lakini inahitaji kuambatana na ufahamu kwamba Baba yetu wa Mbinguni hutuachia maamuzi mengi kwa ajili ya uchaguzi wetu binafsi. … Watu ambao hujaribu kuhamisha ufanyaji uamuzi wote kwa Bwana na kuomba kwa ajili ya ufunuo katika kila uchaguzi punde watapata hali ambazo kwazo wanasali kwa ajili ya mwongozo ila hawaupati. …
“Tunapaswa kujifunza mambo katika akili zetu. … Kisha tunapaswa kusali kwa ajili ya mwongozo na kuufanyia kazi. … Kama hatutapokea maongozi, tunapaswa kutenda kulingana na maamuzi yetu bora.”12
Hitimisho pamoja na Mwaliko
Katika kuhitimisha, Watakatifu wa Siku za Mwisho wanapaswa kuwa watu wenye vipawa, wanaoshika maagano. Pamoja na hayo, inabaki kwa kila mmoja wetu kutafuta kutumia karama zetu za kiroho na kisha kualika na kujifunza kutambua minong’ono ya Roho. Kanuni nne ongozi za kutusaidia sisi katika kazi zetu muhimu za kiroho ni:
-
Simama katika mahali patakatifu.
-
Simama na watu watakatifu.
-
Shuhudia juu ya kweli takatifu.
-
Msikilize Roho Mtakatifu.
Uwezo wako wa kumwalika na kutambua minong’ono ya Roho utakua hatua kwa hatua. “Kuijua vyema lugha ya Roho ni kama kujifunza lugha nyingine. Ni mchakato wa pole pole ambao unahitaji bidii, na jitihada yenye uvumilivu.”13
Nikirejea kule tulikoanzia, tafadhali kumbuka kwamba kama Watakatifu wa Siku za Mwisho mmejaaliwa na Mungu. Ona tukio hili katika Jumapili ya mfungo, ambalo lilisimuliwa kwangu hivi karibuni. Mtoto mdogo, akiwa amesimama juu ya stuli, hakuwa akionekana vizuri kwenye mimbari. Baba yake alikuwa amesimama kando yake akimtia moyo na kumsaidia kwa mnong’ono laini sikioni mwake wakati kwa fahari akisema “Mimi ni Mtoto wa Mungu.”
Ushuhuda mwingine uliofuatia ulikuja kutoka kwa kijana mkubwa aliyeanza kwa sauti ya woga: “Natamani ningekuwa na mtu akininong’oneza sikioni mwangu kama vile.” Kisha akawa na mnururiko wa ushawishi na kushuhudia, “Ninaye mtu huyo ananinong’oneza sikioni mwangu kama hivyo—Roho Mtakatifu!”
Ninafunga kwa mwaliko mahususi kwa vijana wote! Wengi wenu mnaanza siku kwa kusimama mbele ya kioo. Kesho, wiki hii, mwaka huu, daima, tulia unapojitazama mwenyewe kwenye kioo. Fikiria, au sema kwa sauti kama unapenda, “Lo, hebu nitazame. Mimi ni wa ajabu! Mimi ni mwana wa Mungu, Yeye ananijua! Yeye ananipenda! Nina kipawa—nina kipawa cha Roho Mtakatifu kama mwenza wangu wa daima!”
Ninaongeza ushuhuda wangu kwenu, Watakatifu wa Siku za Mwisho mliojaaliwa, na Mungu Baba, Yesu Kristo na Roho Mtakatifu, ambaye anatoa ushuhuda juu Yao. Katika jina la Yesu Kristo, amina.