Mkutano Mkuu
Kutoa Ushahidi juu ya Yesu Kristo kwa Maneno na Matendo
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


9:45

Kutoa Ushahidi juu ya Yesu Kristo kwa Maneno na Matendo

Tunapojitahidi kuishi maisha yetu kulingana na injili ya Yesu Kristo, mwenendo wetu utakuwa ushuhuda hai wa Mkombozi wetu.

Wakati wa ubatizo, moja ya ahadi tunazoweka ni kwamba tuko radhi kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo. Dhumuni langu leo ni kutukumbusha kwamba tunaweza kumwonesha Mungu kwamba tunajichukulia jina la Mwanaye juu yetu kwa kutoa ushuhuda wa maneno na matendo, mara nyingi kadiri tuwezavyo, kwamba Yesu ndiye Kristo.

Wakati akiwahudumia na kuwafundisha watu katika mabara ya Amerika baada ya Ufufuko Wake, Mwokozi alitangaza:

“Je, hawajasoma maandiko, ambayo yanasema, lazima mjivike juu yenu jina la Kristo, ambalo ni jina langu? Kwani, kwa jina hili ndilo mtaitwa nalo katika siku ya mwisho;

“Na yeyote ajichukuliaye jina langu na kuvumilia hadi mwisho, huyo ndiye atakayeokolewa katika siku ya mwisho.”1

Rais Russell M. Nelson ametufundisha kwamba “kujichukulia juu yetu jina la Mwokozi kunajumuisha kutangaza na kushuhudia kwa wengine—kupitia matendo na maneno yetu—kwamba Yesu ndiye Kristo.”2

Kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunayo baraka na fursa ya kusimama kama mashahidi wa Bwana na jina Lake mahali popote tulipo.3 Tunapojitahidi kuishi maisha yetu kulingana na injili ya Yesu Kristo, mwenendo wetu utakuwa ushuhuda hai wa Mkombozi wetu na jina Lake. Zaidi ya hayo, tunamshuhudia Kristo kwa maneno kwa kushiriki na wengine kile tunachokiamini, tunachokihisi au kukijua juu ya Yesu Kristo.

Kwa unyenyekevu tunapotoa ushuhuda wetu juu ya Bwana kupitia maneno na matendo yetu, Roho Mtakatifu huthibitisha4 kwa wale wenye nia halisi na akili iliyo tayari kwamba Yesu hakika ndiye Kristo.5

Ningependa kushiriki mifano miwili ya hivi karibuni na yenye kuvutia ya waumini wanaomwonesha Mungu kwamba wanajichukulia juu yao jina la Yesu Kristo kwa kumzungumzia na kutoa ushahidi safi juu ya Bwana katika mikutano ya Kanisa.

Mfano wa kwanza: Wakati mimi na mke wangu, Elaine tulipokwenda Hispania mwaka 2022, tulihudhuria mikutano ya Jumapili kwenye tawi dogo la Kanisa huko. Nilipokuwa nimeketi jukwaani na mke wangu kwenye mkusanyiko, niligundua kwamba aliketi kando ya mwanamke mzee. Mkutano wa sakramenti ulipomalizika, nilitembea kwenda kwa Elaine na kumwomba anitambulishe kwa rafiki yake mpya. Alifanya hivyo na kubainisha kwamba mwanamke huyu, ambaye hakuwa muumini wa Kanisa, amekuwa akija Kanisani kwa takribani miaka miwili sasa. Niliposikia hilo, nilimuuliza mwanamke huyu mwenye hofu ya Mungu kile kilichomfanya arejee na kuhudhuria mikutano yetu kwa muda mrefu hivyo. Mwanamke kwa upendo alijibu, “ninapenda kuja hapa kwa sababu mnazungumza juu ya Yesu Kristo katika mikutano yenu.”

Hakika, waumini wa Kanisa katika tawi lile huko Hispania walizungumza, walifundisha na kushuhudia juu ya Kristo katika mikutano yao.

Mfano wa pili: Baada ya kuhudumu katika Eneo la Brazil, wito mpya ulikuja wa kuhudumu makao makuu ya Kanisa. Tulipohamia Jiji la Salt Lake mwishoni mwa Julai ya mwaka huu, tulihudhuria mikutano ya Jumapili kwenye kata yetu mpya na yenye kupendeza. Moja ya mikutano hii ulikuwa mkutano wa mfungo na ushuhuda. Baada ya kupokea sakramenti kwa unyenyekevu, waumini walisimama na kutoa shuhuda zao za kugusa mioyo juu ya Mwokozi mmoja baada ya mwingine. Mkutano ulikuwa umefokasi kwa Yesu Kristo na kwa dhahiri tulimhisi Roho. Tulijengwa na imani yetu iliimarishwa. Ikiwa marafiki wa Kanisa, wanaotafuta ukweli kwa dhati, wangekuwa kwenye mkutano ule, wangetambua kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo.

Ni baraka iliyoje kuona kwamba mikutano ya Kanisa letu ni fursa teule kwa ajili yetu kushuhudia juu ya Kristo na kumpa Mungu ishara kwamba tunafurahia katika kujichukulia jina la Mwanaye juu yetu.

Sasa, ngoja nitaje mfano wenye nguvu wa kujichukulia juu yetu jina la Yesu Kristo kwa kutoa ushuhuda juu Yake kupitia matendo.

Agosti iliyopita, nilifuatana na Mzee Johnathan S. Schmitt kwenye ufunguzi wa Hekalu la Feather River California katika jiji la Yuba. Huko, nilipata baraka ya kuyaongoza makundi kwenye ziara ya hekaluni. Moja ya makundi haya lilijumuisha muumini wa Kanisa, Virgil Atkinson, na marafiki saba wa imani zingine. Karibu na mwisho wa ziara, kwenye chumba cha kuunganishia cha hekaluni, Kaka Atkinson alipata hisia wakati alipoelezea upendo wake kwa ajili ya rafiki zake ambao walikuwa wamekuja hekaluni siku ile. Ghafla punde tu baada ya kufanya hivyo, mwanamke kwenye kundi alisimama na kusema, “Sote tunampenda Virgil. Kamwe hajawahi kulazimisha imani yake kwetu. Lakini haionei aibu pia. Anaishi tu kile anachokiamini.”

Kwa miaka mingi, maisha kama ya Kristo ya Kaka Atkinson yalisimama kama ushuhuda wenye nguvu kwa rafiki zake. Mfano wake ni uthibitisho imara kwamba amejichukulia juu yake jina la Kristo.

Katika kuhitimisha, acha nishiriki somo nililojifunza kuhusu jinsi ya kujichukulia juu yetu jina la Kristo na kumshuhudia Yeye kwa kutumia jina sahihi la Kanisa.

Rais Nelson, nabii wa Mungu aliye hai, katika hotuba ya mkutano mkuu wa 2018 yenye kichwa cha habari “Jina Sahihi la Kanisa,” alisema: “Hili ni sahihisho. Hii ni amri ya Bwana. Joseph Smith hakulipa jina Kanisa lililorejeshwa kupitia yeye; wala Mormoni hakufanya hivyo. Ilikuwa ni Mwokozi Mwenyewe aliyesema, ‘Kwani ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho’ [Mafundisho na Maagano 115:4].”6

Sote tuliondoka kwenye mkutano mkuu siku ile tukiwa na msimamo na ari ya kumfuata nabii na kutumia jina lililofunuliwa la Kanisa tangu hapo na kuendelea. Nilikuwa mwangalifu sana kuhakikisha natumia jina sahihi la Kanisa. Nyakati kadhaa za mwanzo ilinibidi niwe makini sana na kutojiruhusu kurejea kwenye njia za zamani. Baada ya majaribio ya mwanzo, nilihisi vizuri kuhusu kutumia jina lililofunuliwa la Kanisa. Ninakiri kwamba mara kadhaa, ningeweza kusema jina la Kanisa kwa haraka sana. Nilihisi wasiwasi kwamba watu wasingetilia umakini kwenye jina kamili la Kanisa na kwamba wangeweza kudhani ni refu sana.

Hata hivyo, baadaye nilitambua kwamba kutaja jina kamili la Kanisa kwa lengo ilinipa fursa za thamani za kulitaja jina la Yesu Kristo na hakika kutoa ushuhuda juu ya Mwokozi kwa kulitangaza jina Lake katika jina la Kanisa Lake. Niligundua pia kwamba nilipotaja jina sahihi la Kanisa kwa wengine, mara nyingi nilimkumbuka Yesu Kristo na kuhisi ushawishi Wake kwenye maisha yangu.

Kwa kumfuata nabii, sote tunaweza kujifunza kushuhudia zaidi juu ya Yesu Kristo kwa kutumia jina sahihi la Kanisa, hivyo kujichukulia kikamilifu juu yetu jina la Bwana.

Asubuhi hii ya Sabato, kwa furaha ninashuhudia kwamba Rais Nelson ni nabii wa Mungu aliye hai na kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni Kanisa la Kristo lililorejeshwa. Kwa unyenyekevu ninatoa ushahidi juu ya Mwana wa Mungu na uungu Wake. Yeye ni Mzaliwa wa Kwanza wa Mungu na Mwana wa Pekee, Mwokozi na Mkombozi wetu, Emanueli.7 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.