Mkutano Mkuu
Kuiona Familia ya Mungu kupitia Lenzi ya Ujumuishi
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


11:30

Kuiona Familia ya Mungu kupitia Lenzi ya Ujumuishi

Ninaamini tunaweza, kupitia jicho la imani, kutokukuza vitu na kujitazama sisi wenyewe na familia zetu kwa tumaini na furaha.

Wakati binti yetu wa mwisho, Berkeley, alipokuwa mdogo, nilianza kutumia miwani ya kusomea–miwani ambayo inavuta na kukuza kila kitu. Siku moja, tukiwa tumeketi pamoja tukisoma kitabu, nilimtazama kwa upendo lakini pia kwa huzuni kwa sababu, ghafla, alionekana kuwa mtu mzima sana. Niliwaza, “Muda unakimbia kiasi hiki? Amekuwa mkubwa sana!”

Nilipoinua miwani yangu ya kusomea ili kufuta chozi, nilitambua, “Oo ngoja—yeye si mkubwa; ni miwani hii tu! Usijali!”

Wakati mwingine tunachoweza kuona ni ule mtazamo wa karibu, uliokuzwa wa wale tunaowapenda. Usiku wa leo, ninawaalika msikuze na mtazame kwa lenzi tofauti—lenzi ya milele ambayo inaangazia picha kuu, hadithi yako kubwa zaidi.

Wakati wa harakati za awali za mwanadamu kwenda anga ya mbali, roketi zisizo na rubani hazikuwa na madirisha. Lakini kwa misheni ya Apollo 8 kwenda mwezini, wanaanga walikuwa na dirisha moja. Walipokuwa wakielea angani, walivutiwa na nguvu ya kuiona dunia yetu na walipiga picha hii yenye kuvutia, ikiteka fikira za ulimwengu mzima! Wanaanga hao walipata msisimko wenye nguvu sana kiasi kwamba umepewa jina: Athari ya Ujumuishi.

Dunia jinsi inavyoonekana kutoka angani.

NASA

Kuangalia kutokea kwenye eneo jipya hubadilisha kila kitu. Msafiri mmoja wa anga alisema “hupunguza vitu hadi kwenye kiasi ambacho unadhani kila kitu kinaweza kudhibitiwa. … Tunaweza kufanya hili. Amani duniani—hakuna shida. Huwapa watu aina hiyo ya ujasiri … aina hiyo ya nguvu.”1

Kama wanadamu, tuna mtazamo wa kidunia, lakini Mungu huona ujumuishi mkuu wa ulimwengu. Anaona uumbaji wote, sisi sote na amejaa tumaini.

Je, inawezekana kuanza kuona kama Mungu anavyoona hata tunapoishi kwenye uso wa sayari hii—kuhisi ujumuishi huu wa hisia? Ninaamini tunaweza, kupitia jicho la imani, kutokukuza vitu na kujitazama sisi wenyewe na familia zetu kwa tumaini na furaha.

Maandiko yanalikubali hili. Moroni anazungumza kuhusu wale ambao imani yao ilikuwa yenye “nguvu kupita kiasi” hata “kweli waliona … kwa jicho la imani, nao wakafurahia.”2

Kwa jicho lililoelekezwa kwa Mwokozi, walihisi furaha na kujua ukweli huu: Kwa sababu ya Kristo, yote yanafanikiwa. Kila kitu ambacho wewe na wewe na wewe mnahofia—yote yatakuwa sawa! Na wale wanaotazama kwa jicho la imani wanaweza kuhisi itakuwa SAWA sasa.

Nilipitia wakati mgumu mwaka wangu wa pili katika shule ya upili wakati sikuwa nikifanya maamuzi mazuri. Nakumbuka nilimwona mama yangu akilia na kujiuliza ikiwa nimemkatisha tamaa. Wakati huo, nilikuwa na wasiwasi kwamba machozi yake yalimaanisha kwamba amepoteza tumaini kwangu, na ikiwa hakuwa na tumaini kwangu, labda hapakuwa na njia ya kurudi.

Lakini baba yangu alikuwa na uzoefu wa kutokukuza mambo na kuchukua mtazamo mrefu. Alijifunza kutokana na uzoefu kwamba wasiwasi huweza kuonekana kama upendo, lakini havifanani.3 Alitumia jicho la imani kuona kila kitu kitakuwa sawa, na mtazamo wake wa tumaini ulinibadilisha.

Nilipomaliza shule ya upili na kwenda BYU, baba yangu alituma barua, akinikumbusha mimi nilikuwa nani. Alikuwa mshangiliaji wangu, na kila mtu anahitaji mshangiliaji: Mtu ambaye hakuambii, “Bado hukimbii haraka vya kutosha,” kwa upendo wanakukumbusha kwamba unaweza.

Baba alitoa mfano wa ndoto ya Lehi. Kama Lehi, baba alijua kwamba huwakimbizi ili uwakamate wale unaowapenda unaohisi wamepotea. “Wewe kaa hapo ulipo na uwaite. Unaenda kwenye mti, baki kwenye mti huo, endelea kula tunda na, ukiwa na tabasamu usoni, endelea kuwapungia mkono wale unaowapenda na kuonesha kwa mfano kwamba kula tunda hilo ni jambo la furaha!”4

Mtazamo huu umenisaidia wakati ambapo sikuwa na furaha ninapojikuta kwenye mti, nikila tunda na kulia kwa sababu nina wasiwasi; kweli, hiyo inasaidiaje? Badala yake, na tuchague tumaini—tumaini katika Muumba wetu na sisi kwa sisi, likichochea uwezo wetu wa kuwa bora kuliko tulivyo hivi sasa.

Muda mfupi baada ya Mzee Neal A. Maxwell kufariki, mwanahabari alimuuliza mwanaye ni kitu gani angekikumbuka zaidi. Alisema chakula cha jioni nyumbani kwa wazazi wake, kwa sababu aliondoka kila mara akihisi kama baba yake alimwamini.

Hii ilikuwa wakati ambao watoto wetu watu wazima walikuwa wanaanza kuja nyumbani kwa ajili ya chakula cha jioni cha Jumapili na wenzi wao. Katika siku za wiki nilijikuta nikitengeneza orodha akilini mwangu ya mambo ambayo ningeweza kuwakumbusha Jumapili, kama vile “Labda jaribu kuwasaidia zaidi watoto ukiwa nyumbani,” au “Usisahau kuwa msikilizaji mzuri.”

Niliposoma maneno ya Kaka Maxwell, nilitupilia mbali orodha hizo na kunyamazisha sauti hiyo yenye ukosoaji, kwa hiyo nilipowaona watoto wangu wakubwa kwa muda huo mfupi tu kila juma, nilifokasi kwenye mambo mengi mazuri waliyokuwa wakifanya tayari. Wakati mwana wetu mkubwa, Ryan, alipofariki miaka michache baadaye, nakumbuka nikishukuru kwamba wakati wetu pamoja ulikuwa wenye furaha na chanya zaidi.

Kabla ya kuchangamana na mpendwa wetu, je, tunaweza kujiuliza swali “Je, kile ninachokaribia kufanya au kusema ni cha manufaa au cha kuumiza?” Maneno yetu ni mojawapo ya nguvu zetu kuu, na wanafamilia ni kama ubao wa kibinadamu, wakisimama mbele yetu wakisema, “Andika unachofikiria kunihusu!” Jumbe hizi, ziwe za kukusudia au bila kukusudia, zinapaswa kuwa za tumaini na za kutia moyo.5

Kazi yetu siyo kumfundisha mtu ambaye anapitia wakati mgumu kwamba ni wabaya au wanakatisha tamaa. Mara chache tunaweza kuhisi kuchochewa kusahihisha, lakini mara nyingi hebu tuwaambie wapendwa wetu kwa njia zinazotamkika na zisizotamkika ujumbe wanaotamani kuusikia: “Familia yetu inahisi kuwa kamili na iliyokamilika kwa sababu uko ndani yake.” “Utapendwa kwa maisha yako yote—bila kujali kinachotokea.”

Wakati mwingine, tunachohitaji ni huruma zaidi kuliko ushauri; kusikiliza zaidi kuliko mhadhara; mtu anayesikia na kujiuliza, “Ningehisije kusema yale waliyoyasema hivi punde?”

Kumbuka familia ni maabara zilizotolewa na Mungu ambapo tunabaini mambo, kwa hivyo makosa na hesabu zisizo sahihi si tu haviwezekani, lakini hutokea. Na je, haingependeza kama, mwisho wa maisha yetu, tungeona kwamba mahusiano hayo, hata nyakati hizo zenye changamoto, ndivyo vitu vilivyotusaidia kuwa zaidi kama Mwokozi wetu? Kila mchangamano mgumu ni fursa ya kujifunza jinsi ya kupenda katika kiwango kikubwa zaidi—kiwango kama cha Mungu.6

Hebu tuvute mbali ili kuona mahusiano ya familia kama njia yenye nguvu ya kutufunza masomo tuliyokuja hapa kujifunza kadiri tunavyomgeukia Mwokozi.

Hebu tukubali, katika ulimwengu ulioanguka, hakuna njia ya kuwa mwenzi, mzazi, mwana au binti, mjukuu, mkufunzi au rafiki mkamilifu—lakini kuna njia milioni za kuwa mwema.7 Hebu tubaki kwenye mti, tukipokea upendo wa Mungu, na kuushiriki. Kwa kuwainua watu karibu nasi, tunapanda pamoja.

Kwa bahati mbaya, kumbukumbu ya kula tunda haitoshi; tunahitaji kula tena na tena kwa njia zinazoweka upya lenzi yetu na kutuunganisha na ujumuishi wa mbinguni kwa kufungua maandiko, ambayo yamejazwa na nuru, ili kufukuza giza; tukipiga magoti hadi maombi yetu ya kawaida yawe na nguvu. Hapo ndipo mioyo inapotulia, na tunaanza kuona jinsi Mungu anavyoona.

Katika siku hizi za mwisho, huenda kazi yetu kuu itakuwa kuwahusu wapendwa wetu—watu wazuri wanaoishi katika ulimwengu mwovu. Tumaini letu hubadilisha jinsi wanavyojiona wao ni akina nani hasa. Na kupitia lenzi hii ya upendo wataona wao watakuwa nani.

Lakini adui hataki sisi au wapendwa wetu turudi nyumbani pamoja. Na kwa sababu tunaishi kwenye sayari ambayo imefungwa kwenye muda na idadi ya miaka yenye ukomo,8 adui huendeleza hali halisi ya hofu ndani yetu. Ni vigumu kuona, tunapovutwa karibu, kwamba mwelekeo wetu ni muhimu zaidi kuliko kasi yetu.

Kumbuka, “Ikiwa unataka kwenda haraka, nenda peke yako. Ikiwa unataka kwenda mbali, nendeni pamoja.”9 Tunashukuru kwamba Mungu tunayemwabudu hafungwi na muda. Anawaona wapendwa wetu jinsi walivyo na sisi jinsi tulivyo hasa.10 Hivyo ana subira kwetu, akitumainia tutakuwa na subira sisi kwa sisi.

Nitakubali kuna nyakati ambapo dunia, makao yetu ya muda, huhisi kama kisiwa cha huzuni—wakati ambapo nina jicho moja la imani na jicho jingine linalia.11 Je, unaijua hisia hii?

Nilikuwa nayo Jumanne.

Je, badala yake tunaweza kuchagua mtazamo aminifu wa nabii wetu anapoahidi miujiza katika familia zetu? Kama tutafanya hivyo, shangwe yetu itaongezeka hata msukosuko ukiongezeka. Yeye anaahidi kwamba athari ya ujumuishi inaweza kuonekana sasa, bila kujali hali zetu.12

Kuwa na jicho hili la imani sasa ni kupokea tena, au mwangwi, wa imani tuliyokuwa nayo kabla hatujafika kwenye sayari hii. Inaona kupita mashaka ya sasa, ikituruhusu “kufanya mambo yote tuliyonayo kwa uchangamfu; na kisha … kusimama tuli.”13

Je, kuna jambo gumu katika maisha yako hivi sasa, jambo ambalo una wasiwasi haliwezi kutatuliwa? Bila jicho la imani, hiyo inaweza kuonekana kama Mungu amepoteza uangalizi wa mambo, na je, hiyo ni kweli?

Au labda hofu yako kuu ni kwamba utapitia wakati huu mgumu peke yako, lakini hiyo ingemaanisha kwamba Mungu amekuacha, na je, hiyo ni kweli?

Ni ushahidi wangu kwamba Mwokozi ana uwezo, kwa sababu ya Upatanisho Wake, kugeuza ndoto yoyote mbaya unayopitia kuwa baraka. Yeye ametupatia ahadi “kwa ahadi isiyobadilika” kwamba tunapojitahidi kumpenda na kumfuata Yeye, “mambo yote ambayo kwayo [sisi] tumeteswa yatafanya kazi kwa pamoja kwa faida [yetu].”14 Mambo yote.

Na kwa sababu sisi ni watoto wa agano, tunaweza kuomba hisia hii ya tumaini sasa!

Ingawa hatuko katika familia iliyo kamilifu, tunaweza kukamilisha upendo wetu kwa wengine hadi uwe upendo wa kudumu, usiobadilika, bila kujali ni aina gani ya upendo—aina ya upendo unaounga mkono mabadiliko na kuruhusu ukuaji na kurejea nyumbani.

Ni kazi ya Mwokozi kuwarudisha wapendwa wetu nyumbani. Ni kazi Yake na kwa wakati Wake. Ni kazi yetu kutoa tumaini na moyo ambao kupitia hivyo wanaweza kuja nyumbani. “Hatuna mamlaka [ya Mungu] ya kuhukumu wala uwezo wake wa kukomboa, lakini tumeidhinishwa kutumia upendo wake.”15 Rais Nelson pia amefundisha kwamba wengine wanahitaji upendo wetu zaidi ya hukumu yetu. “Wanahitaji kupata upendo msafi wa Yesu Kristo unaoakisiwa katika maneno na matendo yetu.”16

Upendo ndiyo kitu kinachobadilisha mioyo. Ni nia safi kuliko zote, na wengine wanaweza kuihisi. Na tushikilie kwa nguvu maneno haya ya kinabii yaliyotolewa miaka 50 iliyopita: “Hakuna nyumba iliyoshindwa isipokuwa ikate tamaa ya kujaribu.”17 Hakika, wale wanaopenda zaidi na kwa kipindi kirefu zaidi hushinda!

Katika familia za kidunia, tunafanya tu yale ambayo Mungu amefanya nasi—kuelekeza njia na kutumaini wapendwa wetu wataenda upande huo, tukijua njia wanayoisafiria ni juu yao wenyewe kuichagua.

Na watakapopita upande wa pili wa pazia na kusogea karibu na ule “mvuto” wa upendo wa makao ya mbinguni,18 ninaamini watahisi si wageni kwa sababu ya jinsi walivyopendwa hapa.

Acha tutumie hiyo lenzi ya ujumuishi na kuwaona watu tunaowapenda na kuishi nao kama wenzetu kwenye sayari yetu nzuri.

Wewe na Mimi? Tunaweza kufanya hili! Tunaweza kusubiria na kutumaini! Tunaweza kubaki kwenye mti na kula tunda huku tukiwa na tabasamu usoni mwetu, na kuruhusu Nuru ya Kristo machoni mwetu iwe kitu ambacho wanaweza kutegemea katika nyakati zao za giza zaidi. Na wanapoiona nuru ikidhihirika katika nyuso zetu, watavutwa kwayo. Kisha tunaweza kusaidia kufokasi tena uangalifu wao kwenye chanzo cha asili cha upendo na nuru, “nyota angavu na ya asubuhi,” Yesu Kristo.19

Ninatoa ushuhuda wangu kwamba haya—yote haya—yatakuwa bora zaidi kuliko wewe na mimi tunavyoweza kufikiria! Kwa jicho la imani kwa Yesu Kristo, na tuone kwamba kila kitu kitakuwa sawa mwishowe na tuhisi kuwa itakuwa sawa sasa. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Anousheh Ansari, katika “The Overview Effect and Other Musings on Earth and Humanity, According to Space Travelers,” cocre.co.

  2. Etheri 12:19; msisitizo umeongezwa.

  3. Ona Jody Moore, “How to Say Hard Things,” Better than Happy (podcast), Sept. 18, 2020, episode 270.

  4. Ronald E. Bartholomew, imetumiwa kwa ruhusa; ona pia 1 Nefi 8:10; 11:21–22.

  5. Ona James D. MacArthur, “The Functional Family,” Marriage and Families, vol. 16 (2005), 14.

  6. Inafanywa iwezekane kadiri tunavyo “Omba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu” (Moroni 7:48).

  7. Msemo wa kauli iliyohusishwa na Jill Churchill.

  8. Ona Richard Eyre, Life before Life: Origins of the Soul … Knowing Where You Came from and Who You Really Are (2000), 107.

  9. Traditional proverb.

  10. Ona Mafundisho na Maagano 93:24, 26.

  11. Ona Robert Frost, “Birches,” in Mountain Interval (1916), 39.

  12. Ona Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona, Nov. 2016, 81–84; ona pia “Acha Mungu Ashinde,” Liahona, Nov. 2020, 92–95.

  13. Mafundisho na Maagano 123:17.

  14. Mafundisho na Maagano 98:3; msisitizo umeongezewa.

  15. Wayne E. Brickey, Inviting Him In: How the Atonement Can Change Your Family (2003), 144.

  16. Ona Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,“ Liahona, Mei 2023, 100.

  17. Teachings of Presidents of the Church: Harold B. Lee (2000), 134.

  18. Ona Paul E. Koelliker, “Yeye Kwa Kweli Anatupenda,” Liahona, Mei 2012, 18.

  19. Ufunuo wa Yohana 22:16.