Mkutano Mkuu
Kuhifadhi Sauti ya Watu wa Agano katika Kizazi Kinachoinukia
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


10:13

Kuhifadhi Sauti ya Watu wa Agano katika Kizazi Kinachoinukia

Moja ya majukumu yetu matakatifu ni kuwasaidia watoto wetu kujua kwa kina na mahususi kwamba Yesu ndiye Kristo.

Moja ya nyakati muhimu sana katika Kitabu cha Mormoni ni ziara ya Mwokozi mfufuka kwa watu katika viwanja vya hekalu katika nchi ya Neema. Baada ya siku nzima ya kufundisha, kuponya na kujenga imani, Yesu alielekeza usikivu wa watu kwa kizazi kinachoinukia: “Aliamuru kwamba watoto wao wachanga waletwe.”1 Aliwaombea na kuwabariki mmoja mmoja. Uzoefu ulikuwa mzuri sana kiasi kwamba Mwokozi mwenyewe alilia mara nyingi.

Kisha, akiongea na umati, Yesu alisema:

“Tazama wachanga wenu.”

“Na walipotazama kuona … , wakaona mbingu zikifunguka, na wakaona malaika wakiteremka kutoka mbinguni,” kuwatumikia watoto wao.2

Mara kwa mara nimetkuwa nikifikiria kuhusu tukio hili. Lazima itakuwa limelainisha moyo wa kila mtu! Walimwona Mwokozi. Walimhisi. Walimjua. Aliwafundisha. Aliwabariki. Na Aliwapenda. Ndio maana haishangazi kwamba baada ya tukio hili takatifu, watoto hawa walikua huku wakisaidia kukuza jamii yenye amani, mafanikio na upendo kama wa Kristo ambao ulidumu kwa vizazi vingi.3

Ingekuwa vyema kama watoto wetu wangekuwa na uzoefu kama huo pamoja na Yesu Kristo—kitu ambacho kingefungamanisha mioyo yao Kwake! Anatualika sisi, kama alivyowaalika wazazi wale katika Kitabu cha Mormoni, kuwaleta watoto wetu wadogo Kwake. Tunaweza kuwasaidia wao kumjua Mwokozi na Mkombozi wao kama ilivyokuwa kwa watoto hawa. Tunaweza kuwaonyesha jinsi ya kumpata Mwokozi katika maandiko na kujenga msingi wao juu Yake.4

Hivi karibuni, rafiki mwema alinifundisha kitu ambacho sikukifahamu hapo kabla kuhusu mfano wa mtu mwenye busara aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba. Kulingana na simulizi ya Luka, yule mtu mwenye busara alipokuwa akijenga msingi kwa ajili ya nyumba yake “alichimba chini sana.”5 Hili halikuwa jambo la kawaida au rahisi—lilihitaji jitihada!

Ili tujenge maisha yetu juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, Yesu Kristo, tunahitaji kuchimba chini sana. Tunaondoa kila kitu ambacho si thabiti au kisichohitajika katika maisha yetu. Tunaendelea kuchimba mpaka tumpate Yeye. Na tunawafundisha watoto wetu kujifungamanisha Kwake kupitia ibada na maagano matakatifu, ili kwamba wakati tufani na mafuriko yajapo, na kwa hakika vitakuja, vitakuwa na madhara madogo juu yao “kwa sababu ya mwamba ambao juu yake [wao] wamejengwa.”6

Aina hii ya nguvu haitokei tu. Haipitishwi tu kwa kizazi kijacho kama urithi wa kiroho. Kila mtu lazima achimbe chini sana ili kuupata huo mwamba.

Tunajifunza somo hili kutoka simulizi nyingine katika Kitabu cha Mormoni. Wakati Mfalme Benjamini alipotoa hotuba yake ya mwisho kwa watu wake, walikusanyika kama familia ili kusikiliza maneno yake. Mfalme Benjamini alitoa ushahidi wenye nguvu juu ya Yesu Kristo, na watu waliguswa sana na ushuhuda wake. Walitamka:

“Roho … ameleta mabadiliko makuu ndani yetu, au mioyoni mwetu. …

“Na tunataka tuagane na Mungu wetu ili tutende nia yake … katika maisha yetu yaliyosalia.”8

Mtu anaweza kudhani kwamba watoto wadogo wenye wazazi ambao wameongoka kiasi hicho hatimaye wangeongoka na kufanya maagano wao wenyewe. Lakini, kwa sababu kadhaa ambazo hazikutajwa kwenye kumbukumbu, maagano yaliyofanywa na wazazi hayakuwa na mashiko kwa baadhi ya watoto wao. Miaka kadhaa baadaye, “kulikuwa na wengi wa kizazi kinachoinukia ambao hawakufahamu maneno ya mfalme Benyamini, kwani walikuwa watoto wadogo alipowazungumzia watu wake; na hawakuamini mila za babu zao.

“Hawakuamini yale ambayo yalikuwa yamezungumzwa kuhusu ufufuo wa wafu, wala hawakuamini kuhusu kuja kwa Kristo. …

“Na hawakubatizwa; wala hawakujiunga na kanisa. Na walikuwa watu tofauti kulingana na imani yao.”9

Ni jambo la huzuni kiasi gani! Kwa kizazi kinachoinikia, si ya kutosha kwa imani katika Yesu Kristo kuwa “mila za babu zao.” Wanahitaji kumiliki imani katika Kristo wao wenyewe. Kama watu wa agano wa Mungu, tunawezaje kuweka ndani ya mioyo ya watoto wetu hamu ya kufanya na kushika maagano pamoja Naye?

Tunaweza kuanza kwa kufuata mfano wa Nefi: “Na tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo, tunatoa unabii kumhusu Kristo, na tunaandika kulingana na unabii wetu, ili watoto wetu wajue chanzo cha kutegemea kwa ajili ya msamaha wa dhambi zao.”10 Maneno ya Nefi yanamaanisha jitihada endelevu, zisizokoma za kuwafundisha watoto wetu kuhusu Kristo. Tunaweza kuhakikisha kwamba sauti ya watu wa agano haiko kimya katika masikio ya kizazi kinachoinukia na kwamba Yesu si mada ya Jumapili- pekee.11

Sauti ya watu wa agano inapatikana katika maneno yetu wenyewe ya ushuhuda. Inapatikana katika maneno ya manabii walio hai. Na inatunzwa kwa nguvu katika maandiko. Ndio hapo ambapo watoto wetu watamjua Yesu na kupata majibu ya maswali yao. Ndio hapo watakapojifunza wao wenyewe mafundisho ya Kristo. Ndio hapo watakapopata tumaini. Hii itawaandaa kwa ajili ya wakati wote wa maisha ya kutafuta ukweli na kuishi katika njia ya agano.

Ninaupenda ushauri huu kutoka kwa Rais Russell M. Nelson:

“Je, ni wapi tunaweza kwenda Kumsikiliza Yeye?

“Tunaweza kwenda kwenye maandiko. Yanatufundisha kuhusu Yesu Kristo na injili Yake, ukuu wa Upatanisho Wake na mpango mkuu wa Baba yetu wa furaha na ukombozi. Kuzama kila siku katika neno la Mungu ni muhimu kwa uhai wa kiroho, hasa katika siku hizi za ongezeko la mabadiliko ya ghafla. Tunaposherehekea katika maneno ya Kristo kila siku, maneno ya Kristo yatatuambia jinsi ya kukabiliana na ugumu ambao hatukufikiria tungekabiliana nao.”12

Je, kusherehekea maneno ya Kristo na kumsikia Yeye kunakuwaje? Ndiyo, inakuwa katika njia yo yote uipendayo wewe! Inaweza kuwa kukusanyika na familia yako kuzungumza kuhusu vitu ambavyo Roho Mtakatifu amekufundisha katika kujifunza kwako maandiko ukitumia Njoo, Unifuate. Inaweza kuwa kukusanyika kila siku na watoto wako ili kusoma mistari michache kutoka kwenye maandiko na kisha kutafuta fursa za kujadili mlichojifunza wakati mkiwa pamoja. Tumia njia bora kwako na familia yako na kisha jaribu kuboresha kila siku.

Tafakari pendekezo hili kutoka Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: “Ikichukuliwa kwa mtu mmoja mmoja, jioni ya nyumbani moja, kikao cha kujifunza maandiko, au mazungumzo ya injili yawezekana isionekane kukamilisha kitu. Lakini mkusanyiko wa jitihada ndogo ndogo, rahisi, zenye kujirudia, zinaweza kuwa na nguvu zaidi na zenye kuimarisha kuliko nyakati chache za kukumbukwa au somo kubwa moja. … Kwa hivyo usikate tamaa, na usiogope kuhusu kukamilisha kitu kikubwa kila wakati. Uwe na mwendelezo tu katika jitihada zako.”13

Moja ya majukumu yetu matakatifu ni kuwasaidia watoto wetu kujua kwa kina na mahususi kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai, Mwokozi na Mkombozi wao binafsi, ambaye ni kichwa cha Kanisa Lake! Hatuwezi kuruhusu sauti yetu ya agano kuzimwa au kuwa kimya pale azungumziwapo Yeye.

Unaweza kuhisi kutotosheleza kwenye jukumu hili, lakini hupaswi kuhisi mpweke. Kwa mfano, mabaraza ya kata yameidhinishwa kuandaa vikao vya baraza la mwalimu kwa ajili ya wazazi. Katika vikao hivi vya robo muhula, wazazi wanaweza kukusanyika kujifunza kutokana na uzoefu wa kila mmoja, kujadili jinsi wanavyoimarisha familia zao na kujifunza kanuni muhimu za kufundisha kama Kristo. Kikao hiki kinapaswa kufanyika wakati wa saa ya pili ya ibada ya kanisa.14 Kinaongozwa na mshiriki wa kata aliyechaguliwa na askofu na hufuata mfumo wa kawaida wa vikao vya baraza la mwalimu, akitumia Kufundisha katika Njia ya Mwokozi kama nyenzo kuu.15 Maaskofu, kama kata yako haifanyi vikao vya baraza la mwalimu kwa sasa kwa ajili ya wazazi, kutana na rais wako wa Shule ya Jumapili na baraza la kata ili mjipange.16

Wapendwa marafiki zangu katika Kristo, mnafanya vyema sana kuliko mnavyodhani. Wewe endelea tu kuweka juhudi. Watoto wako wanaangalia, wanasikiliza na kujifunza. Unapowafundisha, utakuja kujua uhalisia wao wa kweli kama wana na mabinti wapendwa wa Mungu. Wanaweza kumsahau Mwokozi kwa kipindi fulani, lakini nakuahidi, Mwokozi kamwe hatawasahau! Nyakati hizo ambazo Roho Mtakatifu huzungumza nao zitabakia katika mioyo yao na akili zao. Na siku moja watoto wako wataakisi ushuhuda wa Enoshi: Ninajua wazazi wangu ni watu wa haki, “kwani [wao] wamenifundisha … katika malezi na maonyo ya Bwana—na jina la Mungu wangu libarikiwe kwa hayo.”17

Na tukubali mwaliko wa Mwokozi na kuwaleta watoto wetu Kwake. Tufanyapo hivyo, wao watamwona Yeye. Watamhisi. Watamjua. Yeye atawafundisha. Atawabariki. Na, Ee, atawapenda kiasi gani. Na, Ee, ni jinsi gani ninampenda. Katika jina Lake takatifu, Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. 3 Nefi 17:11.

  2. 3 Nefi 17:23–24; ona pia 3 Nefi 5:11–22.

  3. Ona 4 Nefi 1:1–22.

  4. Ona Luka 6:47–49; Helamani 5:12.

  5. Luka 6:48.

  6. Helamani 5:12

  7. Ona Mosia 2:5.

  8. Mosia 5:2, 5. Kumbuka kwamba “hapakuwa yeyote, ila tu watoto wadogo, ambao hawakuingia kwenye agano na kujichukulia juu yao jina la Kristo” (Mosiah 6:2).

  9. Mosia 26:1–2, 4.

  10. 2 Nefi 25:26.

  11. “Kuna mambo mengi ya kufundisha katika injili ya urejesho ya Yesu Kristo—kanuni, amri, unabii na hadithi za maandiko. Lakini haya yote ni matawi ya mti huo huo, kwa sababu vyote hivi vina dhumuni moja: kuwasaidia watu wote kuja kwa Kristo na wakamilishwe ndani Yake (ona Yaromu 1:11; Moroni 10:32). Hivyo basi, bila kujali unalofundisha, kumbuka kwamba hakika wewe unafundisha kuhusu Yesu Kristo na jinsi ya kuwa kama Yeye Alivyo” (Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2022], 6).

  12. Russell M. Nelson, “Msikilize Yeye,” Liahona,, Mei 2020, 89.

  13. Kufundisha katika Njia ya Mwokozi31.

  14. Upendeleo maalumu unaweza kufanywa kwa wazazi wanao fundisha Msingi, kama vile kukutana wakati wa dakika 20 za muda wa kuimba za Msingi au kufanya kikao tofauti katika muda mwingine (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 17.4, Maktaba ya Injili).

  15. Waumini na viongozi wanaweza kuagiza Kufundisha katika Njia ya Mwokozi kupitia Huduma za Usambazaji. Pia inaweza kupatikana kidijitali katika Gospel Library.

  16. Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla13.5.

  17. Enoshi 1:1. Kumbuka kwamba miongoni mwa kizazi kinachoinukia cha wasioamini katika kitabu cha Mormoni walikuwa Alma mdogo na wana wa Mosia. Wakati Alma mdogo hatimaye alipotambua hitaji lake la kubadili maisha yake, alikumbuka kile baba yake alichomfundisha kuhusu Yesu Kristo—mafundisho ambayo ni dhahiri hakuyajali. Lakini kumbukumbu yake ilibakia, na kumbukumbu hiyo ilimwokoa Alma kiroho (ona Alma 36:17–20).