Mkutano Mkuu
Nguvu ya Uponyaji ya Mwokozi juu ya Visiwa vya Bahari
Mkutano mkuu wa Oktoba 2023


Nguvu ya Uponyaji ya Mwokozi juu ya Visiwa vya Bahari

Kupitia baraka za hekaluni, Mwokozi huwaponya watu binafsi, familia na mataifa.

Miaka ya 1960 baba yangu alifundisha katika Chuo cha Kanisa cha Hawaii huko Laie, ambako ndiko nilikozaliwa. Dada zangu wakubwa saba walisisitiza wazazi wangu waniite “Kimo,” jina la Kihawaii. Tuliishi karibu na Hekalu la Laie Hawaii wakati lilipohudumia idadi kubwa ya waumini wa Kanisa katika Eneo la Asia Pasifiki, ikijumuisha Japani.1 Wakati huu, makundi ya Watakatifu wa Kijapani walianza kuja Hawaii kupokea baraka za hekalu.

Mmoja wa waumuni hawa alikuwa dada kutoka kisiwa cha kupendeza cha Okinawa. Hadithi ya safari yake kuelekea Hekalu la Hawaii ni ya maajabu. Miongo miwili kabla, dada huyu alikuwa ameolewa katika ndoa ya kitamaduni ya Kibudha. Miezi michache tu baadaye, Japani ilivamia Pearl Harbor, Hawaii, ikiiweka Marekani kwenye mgogoro na Japani. Kufuatia mapigano kama yale ya Midway na Iwo Jima, vuguvugu la vita liliwarudisha nyuma majeshi ya Wajapani kwenye fuko za kisiwa chake cha nyumbani, Okinawa, kikosi cha mwisho kikisimama dhidi ya majeshi ya Muungano mbele ya sehemu muhimu za Japani.

Kwa miezi mitatu ya vita kali mnamo 1945, Vita ya Okinawa ilipiganwa. Boti 1,300 za kivita za Marekani zilikizingira na kukishambulia kisiwa hiki. Vifo vya wanajeshi na raia vilikuwa vya kutisha. Leo, mnara wa kipekee huko Okinawa una orodha ya zaidi ya majina yanayojulikana 240,000 ya watu waliokufa katika vita.2

Katika jaribio hatari la kukimbia kifo, mwanamke huyu wa Okinawa, mumewe na watoto wawili wadogo walitafuta hifadhi ndani ya pango la mlima. Walivumilia madhila yasiyoelezeka kwa wiki na miezi iliyofuatia.

Usiku mmoja usio na tumaini katikati ya vita, akiwa na familia yake yenye njaa na mumewe akiwa amezirai, dada huyu alifikiria kuyahitimisha mateso ya familia yake kwa bomu la kurusha, ambalo mamlaka husika walikuwa wamempa yeye na wengine kwa kusudi hilo. Hata hivyo, alipokuwa akijiandaa kufanya hivyo, uzoefu wenye nguvu wa kiroho ulijifunua ambao ulimpa maana halisi ya uhalisia wa Mungu na upendo Wake kwake, kitu ambacho kilimpa nguvu ya kusonga mbele. Katika siku zilizofuatia, alimsaidia mumewe kuzinduka na aliishibisha familia yake kwa majani, asali kutoka kwenye mizinga ya mwituni na viumbe vilivyopatikana kwenye kijito cha karibu. Cha kustaajabisha, walivumilia miezi sita ndani ya pango hadi wanakijiji wa pale walipowaambia kwamba vita ilikuwa imeisha.

Familia iliporejea nyumbani na kuanza kujenga upya maisha yao, mwanamke huyu Mjapani alianza kutafuta majibu kuhusu Mungu. Taratibu alichochea imani katika Yesu Kristo na hitaji la kubatizwa. Hata hivyo, alijiuliza juu ya wapendwa wake ambao walikufa bila ufahamu wa Yesu Kristo na ubatizo, ikijumuisha mama yake, aliyefariki wakati akimzaa.

Pata taswira ya furaha yake wakati akina dada wawili wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho walipofika nyumbani kwake na kumfundisha kwamba watu wanaweza kujifunza kuhusu Yesu Kristo katika ulimwengu wa roho. Alifurahishwa na mafundisho kwamba wazazi wake wangeweza kuchagua kumfuata Yesu Kristo baada ya kifo na kuukubali ubatizo wake kwa niaba yao ndani ya sehemu takatifu zinazoitwa mahekalu. Yeye na familia yake waliongoka kwa Mwokozi na walibatizwa.

Familia yake ilifanya kazi kwa bidii na walianza kufanikiwa, wakiongeza watoto wengine watatu. Walikuwa waaminifu na walishiriki kikamilifu Kanisani. Kisha, pasipo kutarajia, mumewe aliugua kiharusi na kufariki, kitu kilichomsukuma afanye kazi zaidi ya moja kwa masaa mengi kwa miaka mingi ili kuwakimu watoto wake watano.

Baadhi ya watu kwenye familia na ujirani wake walimkosoa. Walimlaumu na kunganisha masumbuko yake kwenye uamuzi wake wa kujiunga na Kanisa la Kikristo. Pasipo kuyumbishwa na janga hili kubwa na ukosoaji mkali, alishikilia imani yake katika Yesu Kristo, akidhamiria kusonga mbele, akitumaini kwamba Mungu alimjua na siku angavu zilikuwa mbeleni.3

Miaka michache kufuatia kifo cha ghafla cha mumewe, rais wa misheni huko Japani alihisi kuwahimiza waumini wa Kijapani wajiandae kuhudhuria hekaluni. Rais wa misheni alikuwa ni askari mstaafu w Mmarekani wa vita ya Okinawa, ambayo dada yule wa Okinawa na familia yake walidhurika sana.4 Hata hivyo, yule dada mnyenyekevu alimwambia rais kwamba: “Rais alikuwa mmoja wa adui aliyechukiwa wakati wa vita lakini sasa alikuwa pale na injili ya upendo na amani. Hili, kwangu mimi, ilikuwa muujiza.”5

Baada ya kusikia ujumbe wa rais wa misheni, dada mjane alitamani kuunganishwa na familia yake hekaluni siku moja. Hata hivyo, haikuwezekana, kwa sababu ya pesa na tatizo la lugha.

Kisha suluhisho kadhaa za ubunifu ziliibuka. Gharama zingeweza kupunguzwa nusu ikiwa waumini wa Japani wangekodi ndege yote ili kwenda Hawaii katika msimu usio wa shughuli nyingi.6 Waumini pia walirekodi na kuuza santuri zenye jina Watakatifu Wajapani Wanaimba. Baadhi ya waumini hata waliuza nyumba. Baadhi waliacha kazi ili kufanikisha safari hiyo.7

Changamoto nyingine kwa waumini ilikuwa ni kwamba mawasilisho ya hekaluni hayakupatikana kwa Kijapani. Viongozi wa Kanisa walimwita kaka wa Mjapani kusafiri mpaka Hekalu la Hawaii ili kutafsiri ibada ya endaumenti.8 Alikuwa ni mwongofu wa Mjapani wa kwanza baada ya vita, baada ya kufundishwa na kubatizwa na wanajeshi waaminifu Mmarekani.9

Wakati waumini wenye endaumenti wa Wajapani wanaoishi Hawaii waliposikia tafsiri kwa mara ya kwanza walilia. Muumini mmoja aliandika, “tumekwenda hekaluni mara nyingi sana. Tumesikia ibada kwa Kingereza. [Lakini] hatukuwahi kamwe kumhisi roho … wa kazi za hekaluni kama tunavyomhisi sasa [tukiisikia] kwa lugha yetu ya asili.”10

Baadaye mwaka huo huo, watu wazima 161 na watoto walianza safari yao kutoka Tokyo na kuelekea mpaka Hekalu la Hawaii. Kaka mmoja Mjapani alisema kuhusu safari hiyo: “Nilipotazama nje ya ndege na kuiona Pearl Harbor na kukumbuka kile nchi yetu ilichokifanya kwa watu hawa mnamo Desemba 7, 1941, nilipata hofu moyoni mwangu. Je, watatukubali? Lakini kwa mshangao wangu walionesha upendo na ukarimu mkubwa kuliko nilivyowahi kuona maishani mwangu.”11

Picha
Watakatifu Waapani wanakaribishwa kwa mataji ya maua.

Kuwasili kwa Watakatifu Wajapani, waumini wa Hawaii waliwakaribisha Wao kwa mataji ya maua yasiyo na idadi huku wakikumbatiana na mabusu mashavuni, mila ngeni kwenye utamaduni wa Kijapani. Baada ya siku 10 zenye uzoefu mwingi huko Hawaii, Watakatifu Wajapani waliaga kwa wimbo “Aloha Oe” ulioimbwa na Watakatifu wa Kihawaii.12

Safari ya pili ya Hekaluni iliyopangwa kwa ajili ya waumini Wajapani ilimjumuisha dada mjane wa Okinawa. Alisafiri maili 10,000 (16,000-km) shukrani kwa zawadi kutoka kwa wamisionari waliotumikia katika tawi lake na waliokuwa wamekula milo mingi kwake. Akiwa ndani ya hekalu, alitiririka machozi ya furaha aliposimama kama mbadala kwa ajili ya ubatizo wa mama yake na aliunganishwa kwa mumewe aliyefariki.

Matembezi ya hekaluni kutoka Japani kwenda Hawaii yaliendelea mara kwa mara mpaka Hekalu la Tokyo Japan lilipowekwa wakfu mnamo 1980, na kuwa hekalu la 18. Mnamo Novemba ya mwaka huu, hekalu la 186 litawekwa wakfu huko Okinawa, Japani. Limejengwa karibu na pango huko Okinawa ya kati ambapo mwanamke huyu na familia yake walipata hifadhi.13

Japo sikuwahi kukutana na dada huyu wa kupendeza kutoka Okinawa, urithi wake unaendelea kupitia uzao wake, wengi wao nawajua na kuwapenda.14

Baba yangu, askari mstaafu wa Pasifiki wa Vita ya Pili ya Dunia, alifurahishwa nilipopokea wito wangu kutumikia huko Japani kama mmisionari kijana. Nilifika Japani muda mfupi tu baada ya Hekalu la Tokyo kuwekwa wakfu na niliona dhahiri upendo wao kwa ajili ya hekalu.

Maagano ya hekaluni ni zawadi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa wafuasi waaminifu wa Mwanaye, Yesu Kristo. Kupitia hekalu, Baba yetu wa Mbinguni huwaunganisha watu binafsi na familia kwa Mwokozi na kwa kila mmoja.

Rais Russell M. Nelson alitamka mwaka jana:

“Kila mtu anayefanya maagano katika birika za ubatizo na hekaluni—na kuyashika—ameongeza upatikanaji wa uweza wa Yesu Kristo. …

“Thawabu ya kushika maagano na Mungu ni uweza wa kimbingu—nguvu ambayo inatuimarisha sisi ili kustahimili majaribu yetu, vishawishi na maumivu yetu ya moyo vyema zaidi. Nguvu hii inarahisisha njia yetu.”15

Kupitia baraka za hekaluni, Mwokozi huwaponya watu binafsi, familia na mataifa—hata wale ambao wakati mmoja walisimama kama maadui wenye chuki. Bwana aliyefufuka alitangaza kwa jamii iliyokuwa imajaa machafuko katika Kitabu cha Mormoni kwamba wale wanaolicha “jina langu, yule Mwana wa Haki atawashukia na uponyaji katika mabawa yake.”16

Nina shukrani kuwa shahidi kwenye utimizwaji wa ahadi ya Bwana kwamba “wakati unakaribia ambako ufahamu wa Mwokozi utapenya kila taifa, kabila, lugha, na watu,”17 ikiwa ni pamoja na “visiwa vya bahari.”18

Ninashuhudia juu ya Mwokozi Yesu Kristo na juu ya nabii na mitume Wake katika siku hizi za mwisho. Kwa dhati ninatoa ushahidi wa nguvu ya kimbingu ya kuunganisha mbinguni kile kilichounganishwa duniani.

Hii ni kazi ya Mwokozi, na mahekalu ni nyumba Yake takatifu.

Kwa msimamo usioyumba, ninatamka kweli hizi katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Hekalu la Laie Hawaii liliwekwa wakfu mnamo 1919 na Rais Heber J. Grant. Kama mtume, alifungua Kanisa huko Japani mnamo 1901. Lilikuwa ni hekalu la tano na la kwanza kujengwa nje ya bara la Amerika.

  2. Mnamo Machi 2, 2023, kulikuwa na majina 241,281 yaliyochongwa kwenye mnara

  3. Ona Gordon B. Hinckley, “Keep the Chain Unbroken” (Brigham Young University devotional, Nov. 30, 1999), 4, speeches.byu.edu.

  4. Dwayne N. Andersen alijeruhiwa kwenye Mapigano ya Okinawa. Alitumikia kama rais wa misheni huko Japani mnamo 1962 mpaka 1965 na alikuwa rais wa kwanza wa hekalu la Tokyo Japan, kuanzia 1980 mpaka 1982.

  5. Nilikutana na wanafamilia yake wakati mke wangu na mimi tukitumikia kama viongozi wa misheni huko Tokyo. Walinipa taarifa kutoka kwenye historia ya familia binafsi ya matukio yao.

  6. Ona Dwayne N. Andersen, An Autobiography for His Posterity, 102–5, Church History Library, Salt Lake City.

  7. Ona Dwayne N. Andersen, 104.

  8. Ona Edward L. Clissold, “Translating the Endowment into Japanese,” Stories of the Temple in Lā‘ie, Hawai‘i, comp. Clinton D. Christensen (2019), 110–13.

  9. Mtafsiri, Tatsui Sato, alibatizwa Julai 7, 1946, na mwanajeshi wa Mmarekani, C. Elliott Richards. Mke wa Tatsui, Chiyo Sato, alibatizwa siku hiyo hiyo na Boyd K. Packer. Neal A. Maxwell alipigana kwenye vita ya Okinawa, na L. Tom Perry alikuwa kati ya wanajeshi wanamaji wa kwanza kufika pwani ya Japani kufuatia mkataba wa amani. Wazee Packer, Maxwell na Perry walikuwa washiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili.

  10. In Clissold, “Translating the Endowment into Japanese,” 112.

  11. In Dwayne N. Andersen, “1965 Japanese Excursion,” Stories of the Temple in Lā‘ie, Hawai‘i, 114.

  12. Ona Andersen, “1965 Japanese Excursion,” 114, 117.

  13. Baadae kwenye kikao hiki cha mkutano mkuu wa Oktoba 2023, Rais Russell M. Nelso alitangaza mahekalu mapya 20, ikijumuisha la Osaka Japan, ambalo litakuwa la tano huko Japani.

  14. Wakati wa misheni yetu huko Tokyo kuanzia 2018 haddi 2021, katikati ya changamoto za janga la UVIKO, familia yake ilitoa upendo na kujali kwangu mimi na mke wangu, kitu ambacho daima tutakuwa na shukrani nacho.

  15. Russell M. Nelson, “Ushinde Ulimwengu na Upate Pumziko,” Liahona, Nov. 2022, 96.

  16. 3 Nefi 25:2.

  17. Mosia 3:20.

  18. 2 Nefi 29:7.

Chapisha