“Kutimiza Ahadi Yake,” Rafiki, Machi. 2023, 10–11.
Kutimiza Ahadi Yake
Nilimdanganya Baba. Sasa nini kinafuata?
Hadithi hii ilitokea huko Ghana.
“Siku sita tu hadi ubatizo wangu!” Happiness alisema. Siku ni kama imefika.
“Je, uko tayari?” Baba alimwuliza.
“Nafikiri hivyo,” alisema Happiness.
“Wakati unapobatizwa, unafanya agano,” Baba alisema. “Je, unakumbuka hiyo inamaanisha nini?”
“Ni ahadi, si ndio?”
Baba aliitikia kwa kichwa. “Ndiyo! Wewe unaahidi kumfuata Yesu Kristo na kushika amri. Baba wa Mbinguni anaahidi kukubariki na kukusaidia.
Happiness alitabasamu. Alijua kuwa ilikuwa ahadi muhimu. Alikuwa na shauku ya kufanya ubatizo!
Mwishowe siku ya ubatizo wake ilifika. Happiness alibadilisha na kuvaa nguo nyeupe. Watoto wengine wawili walikuwa wakibatizwa pia. Wote waliangalia maji yakijazwa kwenye kisima cha ubatizo.
Ilipofika zamu yake, Happiness na Baba waliingia kwenye kisima. Baba alisema sala ya ubatizo. Kisha Happiness aliziba pua yake, na Baba akamzamisha kabisa ndani ya maji.
Alipoinuliwa kutoka majini, Happiness alihisi vizuri sana. Alitaka kutimiza ahadi yake ya kumfuata Yesu. Alitaka kuhisi safi na mwenye furaha milele. Hakutaka kufanya uchaguzi usio sahihi tena.
Siku chache baadaye, Happiness aliamka na kuwasha maji moto ili akaoge. Ilichukuwa muda mrefu kwa maji kupata moto. Hivyo Happiness akawasha TV. Alitaka kuangalia katuni wakati akisubiri.
Happiness alicheka alipokuwa akiangalia wanyama wakiongea kwenye skrini. Onyesho hili lilikuwa lenye kuburudisha! Punde akawa amesahau yote kuhusu maji moto.
Saa moja baadaye, Baba akaingia ndani ya chumba. “Ni kwa muda gani maji moto yamewashwa?” aliuliza.
Happiness akatazama juu. Alikuwa ameangalia TV kwa muda mrefu kuliko alivyokusudia!
“Siyo muda mrefu,” Happiness alisema. “Kwa dakika chache tu.” Alizima ile TV na kukimbia kwenda kuoga.
Lakini siku hiyo yote, Happiness alikuwa akijihisi vibaya kwa ndani. Baada ya ubatizo wake yeye alitaka kamwe asifanye uchaguzi mbaya. Lakini sasa alikuwa amemwongopea baba!
Happiness alishusha pumzi kwa nguvu. Alijua nini alitakiwa kufanya.
“Baba,” Happiness alisema. “Nilisema uongo. Niliacha maji moto kwa muda mrefu, lakini bila kukusudia. Samahani!
“Ni SAWA. Asante kwa kuniambia,” Baba alisema.
“Ninahisi vibaya sana kwa sababu nimevunja ahadi yangu ya ubatizo,”
Baba alikaa chini na Happiness kwenye kochi. “Wakati wewe ulipobatizwa, hukuahidi kuwa mkamilifu. Uliahidi kujaribu kwa bidii kumfuata Yesu.
Happiness aliitikia kwa kichwa. Hiyo ilimfanya ahisi vizuri kidogo.
“Na unajua unaweza kufanya nini unapofanya uchaguzi usio sahihi? Baba aliuliza.
“Kutubu?” alisema Happiness.
“Hilo ni sahihi! Tunapotubu, Baba wa Mbinguni anatusamehe. Ndipo tunaweza kuwa wasafi kama tulivyokuwa siku tulipobatizwa. Kutubu ni sehemu ya kutimiza ahadi yako ya ubatizo.”
Happiness alitabasamu. “Ninaenda kusali na kumuomba Baba wa Mbinguni ili anisamehe.” Alifurahi kuwa aliweza kutimiza ahadi yake ya ubatizo.