“Kitabu cha Dinosau,” Rafiki, Machi. 2023, 22–23.
Kitabu cha Dinosau
Sophia alinuna. Kwa nini hawezi kuwapenda dinosau pia?
Sophia na Allie walikuwa mapacha, na walikuwa marafiki wakubwa sana. Walipenda vitu tofauti, lakini hilo lilifanya kuwa burudani zaidi! Walipenda kucheza pamoja.
Siku moja shuleni, Sophia alikwenda kuazima kitabu kuhusu dinosau kutoka maktaba. Alikuwa na shauku ya kukionyesha kwa Allie.
“Wewe huwezi kukisoma hicho,” alisema Timmy, mvulana katika darasa lake.
“Kwa nini?” Sophia aliuliza.
“Ni kitabu cha mvulana,” alisema. “Dinosau ni kwa wavulana”
Sophia alinuna. Kwa nini hawezi kuwapenda dinosau pia? Akakiweka kile kitabu katika begi lake la mgongoni. Hata hivyo alikuwa akienda kukisoma.
Siku nzima, Sophia alifikiria kuhusu kile Timmy alichosema. Bado alijihisi kufadhaika alipofika nyumbani kutoka shuleni.
“Kuna tatizo gani?” Mama aliuliza.
“Timmy kasema mimi siwezi kusoma kitabu kuhusu dinosau,” Sophia alisema. “Kasema dinosau ni kwa wavulana tu. “Hiyo siyo kweli, si ndio?”
“Siyo kweli,” Mama alisema.
Sophia alitazama chini. “Basi kwa nini Timmy aseme hivyo?”
“Pengine yeye hajui msichana mwingine yeyote ambaye anawapenda dinosau,” Mama alisema. “Lakini Baba wa Mbinguni hakutufanya sisi sote sawa. Na Anataka sisi tutendeane kwa ukarimu.
Mama alimpa Sophia kumbatio kubwa. “Pole kwa Timmy kukufanyia hivyo. Baba wa Mbinguni anakupenda. Na mimi vile vile.”
“Asante, mama,” Sophia alisema. Alihisi vizuri sasa.
“Nitakwenda kuongea na mwalimu wako kuhusu hilo, SAWA?” Mama alisema.
Sophia aliitikia kwa kichwa. “SAWA.”
Sophia alienda kucheza pamoja na Allie. Walibuni mchezo unaoitwa Super Princess Raser, ambapo wanasesere wa Allie walikuwa waendesha magari ya mashindano. Kulikuwa na upenyo mdogo wa kutokea, lakini Princess Lightning Cheetah akawa mshindi. Sophia na Allie walishangilia.
“Unataka kuona kitabu cha dinosau nilichopata leo?” Sophia aliuliza.
“Hakika!” Allie alisema
Sophia alitabasamu. Alifurahi kwamba siku zote alipata burudani na Allie.
Siku iliyofuata,mwalimu wa Sophia alikuwa na tangazo. “Darasa,” alisema, “kuna kitu nataka kuwaambieni. Ni SAWA kupenda vitu tofauti. Vitabu vyetu vyote na wanasesere ni kwa ajili ya kila mtu.
Sophia alikuwa na furaha sana! Wakati wa kusoma, yeye alitoa kitabu cha dinosau nje ya begi lake la mgongoni.
Timmy akaja kwenye dawati lake. “Samahani nilisema kuwa usingeweza kusoma kitabu hicho,” Timmy alisema. “Mimi pia ninawapenda dinosau.”
“Ni SAWA,” Sophia alisema. “Je, unataka kusoma na mimi?”
“Hakika!” Timmy aliketi karibu naye. “Asante.”
Sophia alikifungua kile kitabu. Yeye na Timmy walikuwa tofauti, lakini ilikuwa vizuri kushiriki pamoja na rafiki mpya.
Hadithi hii ilitokea huko Marekani.