Jibu Daima ni Yesu Kristo
Maswali au shida zozote mlizonazo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo.
Wapendwa akina kaka na akina dada, tumelishwa kiroho kwa kipindi cha siku hizi mbili zilizopita. Muziki wa kwaya ulikuwa mzuri sana. Wale ambao wamezungumza wamekuwa vyombo vya Bwana. Ninaomba kwamba mtamtafuta Roho Mtakatifu apate kuwaongoza katika kujifunza kwenu mnapotafakari kweli zilizofunzwa kutoka kwenye mimbari hii. Kweli hizi hakika zimetumwa kutoka mbinguni.
Wiki moja kutoka leo itakuwa Jumapili ya Pasaka. Haya ni maadhimisho muhimu sana ya kidini kwa wafuasi wa Yesu Kristo. Sababu muhimu ya kusherehekea Krismasi ni kwa sababu ya Pasaka. Somo la Njoo, Unifuate la wiki hii litakushawishi wewe usome kuingia kwa Mwokozi kwa ushindi katika Yerusalemu, usafishaji Wake wa hekalu, mateso Yake ndani ya Bustani ya Gethsemane, Kusulubiwa Kwake, Ufufuko Wake mtukufu, na hatimaye kujitokeza Kwake kwa Wafuasi Wake.1
Furahieni mistari hii mitakatifu na mpate kila njia mnayoweza kumshukuru Baba yetu wa Mbinguni kwa kutuletea Mwanaye wa Pekee.2 Kwa sababu ya Yesu Kristo, tunaweza kutubu na kusamehewa dhambi zetu. Kwa sababu Yake, kila mmoja wetu atafufuka.
Pia ninawaalika mjifunze tena tukio la Mwokozi akiwatokea Wanefi katika mabara ya Amerika, kama ilivyorekodiwa katika Nefi 3 . Si muda mrefu kabla ya kutokea huko, sauti Yake ilisikika miongoni mwa watu, ikijumuisha maneno haya ya kusihi:
“Je mtarudi kwangu sasa, na kutubu dhambi zenu, na kugeuka ili niwaponye?
“… Tazama, mkono wangu wa rehema umenyoshwa kwenu, na yeyote atakayekuja, nitampokea.”3
Wapendwa akina kaka na akina dada, Yesu Kristo anatoa mwaliko huo huo kwenu leo. Ninawasihi mje Kwake ili kwamba Yeye aweze kuwaponya ninyi! Yeye atawaponya ninyi kutokana na dhambi pale mnapotubu. Yeye atawaponya ninyi kutokana na huzuni na hofu. Yeye atawaponya ninyi kutokana na majeraha ya ulimwengu huu.
Maswali au shida zozote mlizonazo, jibu daima linapatikana katika maisha na mafundisho ya Yesu Kristo. Jifunzeni zaidi kuhusu Upatanisho Wake, upendo Wake, rehema Yake, fundisho Lake, na injili Yake ya urejesho ya uponyaji na ukuaji. Mgeukie Yeye! Mfuate Yeye!
Yesu Kristo ndiyo sababu ya sisi kujenga mahekalu. Kila moja ni nyumba Yake takatifu. Kufanya maagano na kupokea ibada muhimu katika hekalu, vile vile kutafuta kusogea karibu Naye hekaluni, kutabariki maisha yenu katika njia ambayo hakuna aina nyingine ya kuabudu inaweza. Kwa sababu hii, tunafanya yote yaliyo katika uwezo wetu kufanya baraka za hekalu kupatikana zaidi kwa waumini wetu kote ulimwenguni. Leo, nina shukrani kutangaza mipango yetu ya kujenga hekalu jipya katika kila maeneo yafuatayo:
-
Retalhuleu, Guatemala
-
Iquitos, Peru
-
Teresina, Brazili
-
Natal, Brazili
-
Tuguegarao City, Ufilipino
-
Iloilo, Ufilipino
-
Jakarta, Indonesia
-
Hamburg, Ujerumani
-
Lethbridge, Alberta, Kanada
-
San Jose, California
-
Bakersfield, California
-
Springfield, Missouri
-
Charlotte, Carolina ya Kaskazini
-
Winchester, Virginia
-
Harrisburg, Pennsylvania
Wapendwa akina kaka na dada zangu, ninatoa ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo anaelekeza mambo ya Kanisa Lake. Ninashuhudia kwamba kumfuata Yeye ndiyo njia pekee ya furaha endelevu. Ninajua kwamba nguvu Zake zinawashukia watu Wake wenye kushika agano, ambao “wamejikinga kwa utakatifu na kwa nguvu za Mungu katika utukufu mkuu.”4 Nashuhudia hivyo, kwa upendo wangu na baraka kwa kila mmoja wenu, katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.