Maandiko Matakatifu
Musa 7


Mlango wa 7

(Desemba 1830)

Henoko anafundisha, anawaongoza watu, na kuiondoa milima—Mji wa Sayuni unaanzishwa—Henoko anaona mapema kuja kwa Mwana wa Mtu, dhabihu Yake ya upatanisho, na ufufuko wa Watakatifu—Yeye anauona mapema Urejesho, Kukusanyika, Ujio wa Pili, na kurudi kwa Sayuni.

1 Na ikawa kwamba Henoko aliendelea na hotuba yake, akisema: Tazama, baba yetu Adamu alifundisha mambo haya, na wengi wameamini na wamekuwa wana wa Mungu, na wengi hawajaamini, nao wameangamia katika dhambi zao, nao wanatazamia kwa uwoga, katika wasi wasi, kwa ajili ya uchungu mkali wa ghadhabu ya Mungu itakayomwagwa juu yao.

2 Na tangu wakati ule na kuendelea Henoko akaanza kutoa unabii, akisema kwa watu, kwamba: Nilipokuwa nikisafiri, na kusimama juu ya mahali panapoitwa Mahuja, na nikamlilia Bwana, ikaja sauti kutoka mbinguni, ikisema—Geuka, na uende juu ya mlima Simioni.

3 Na ikawa kwamba nikageuka kwenda juu ya ule mlima; na nikiwa nimesimama juu ya mlima, nikaona mbingu zimefunguka, nami nikavikwa utukufu;

4 Nami nikamwona Bwana; naye alikuwa amesimama mbele ya uso wangu, naye akasema nami, hata kama vile mtu asemavyo na mwingine, uso kwa uso; naye akaniambia: Angalia, na nitakuonyesha ulimwengu kwa kipindi cha vizazi vingi.

5 Na ikawa kwamba nikaona katika bonde la Shumu, na lo, watu wengi ambao walikaa katika mahema, ambao walikuwa watu wa Shumu.

6 Na tena Bwana akaniambia: Angalia; nami nikaangalia upande wa kaskazini, nami nikawaona watu wa Kanaani, waliokuwa wakiishi katika mahema.

7 Na Bwana akaniambia: Toa unabii; nami nikatoa unabii, nikisema: Tazama watu wa Kanaani, ambao ni wengi, watakwenda vitani dhidi ya watu wa Shumu, na watawauwa ili wapate kuwaangamiza kabisa; na watu wa Kanaani watajigawa wenyewe katika nchi, nayo nchi itakuwa kame na isiyozaa, na hakuna watu wengine watakaoishi hapo ila watu wa Kanaani;

8 Kwa maana tazama, Bwana atailaani nchi kwa joto kali, na ukame wake utadumu milele; na ukaja weusi juu ya watoto wote wa Kanaani, hivyo wakadharauliwa miongoni mwa watu wote.

9 Na ikawa kwamba Bwana akaniambia: Angalia; nami nikaangalia, na kuona nchi ya Sharoni, na nchi ya Henoko, na nchi ya Omneri, na nchi ya Heni, na nchi ya Shemu, na nchi ya Haneri, na nchi ya Hanania, na wakazi wao wote;

10 Na Bwana akaniambia: Nenda kwa watu hawa, na uwaambie—Watubu, nisije nikatoka na kuwapiga kwa laana, nao wakafa.

11 Naye akanipa amri kwamba yanipasa kubatiza katika jina la Baba, na la Mwana, aliyejaa neema na kweli, na la Roho Mtakatifu, awashuhudiaye Baba na Mwana.

12 Na ikawa kwamba Henoko aliendelea kuwasihi watu wote kutubu, isipokuwa waliokuwa watu wa Kanaani;

13 Na imani ya Henoko ilikuwa kubwa sana kwamba aliwaongoza watu wa Mungu, na maadui zao walikuja kupigana nao; na yeye alinena neno la Bwana na nchi ikatetemeka, na milima ikakimbia, hata kulingana na amri yake; na mito ya maji iligeuzwa uelekeo wake; na ngurumo za simba ilisikika nyikani; na mataifa yote yaliogopa sana, hivyo neno la Henoko lilikuwa lenye nguvu, na lugha ambayo Mungu alimpa ilikuwa yenye nguvu kubwa.

14 Pia ikajitokeza nchi kutoka kilindi cha bahari, na hivyo uwoga mkubwa ulikuwa juu ya maadui wa watu wa Mungu, kiasi kwamba walikimbia na kusimama mbali na walikwenda juu ya nchi ambayo ilijitokeza kutoka kilindi cha bahari.

15 Na mapandikizi ya watu wa nchi, pia, yalisimama mbali; na hapo ikaenda laana juu ya watu wote ambao walipigana dhidi ya Mungu;

16 Na tangu wakati ule na kuendelea pakawepo vita na umwagaji wa damu miongoni mwao; lakini Bwana alikuja na kukaa pamoja na watu wake, nao walikaa katika haki.

17 Uwoga juu ya Bwana ulikuwa juu ya mataifa yote, utukufu wa Bwana ukawa mkubwa sana, juu ya watu wake. Naye Bwana akaibariki nchi, nao walibarikiwa juu ya milima, na juu ya mahali palipoinuka, na wakastawi.

18 Na Bwana akawaita watu wake Sayuni, kwa sababu wao walikuwa wa moyo mmoja na wazo moja, na waliishi katika haki; na hapakuwa na maskini miongoni mwao.

19 Na Henoko aliendeleza kuhubiri kwake katika haki kwa watu wa Mungu. Na ikawa katika siku zake, kwamba alijenga mji ambao uliitwa Mji Mtakatifu, hata Sayuni.

20 Na ikawa kwamba Henoko aliongea na Bwana; naye akamwambia Bwana: Hakika Sayuni itakaa katika usalama milele. Lakini Bwana akamwambia Henoko: Sayuni nimeibariki, bali mabaki ya watu nimewalaani.

21 Na ikawa kwamba Bwana akamwonyesha Henoko wakazi wote wa dunia; naye akawaona, na lo, Sayuni, baada ya muda, ikatwaliwa juu mbinguni. Na Bwana akamwambia Henoko: Tazama makao yangu milele.

22 Na Henoko pia aliona mabaki ya watu waliokuwa wana wa Adamu; na wakawa mchanganyiko wa uzao wote wa Adamu isipokuwa uzao wa Kaini, kwa kuwa uzao wa Kaini walikuwa weusi, na hawakuwa na mahali miongoni mwao.

23 Na baada ya Sayuni ikatwaliwa juu mbinguni, Henoko aliona, na lo, mataifa yote ya dunia yalikuwa mbele yake;

24 Na hapo kikaja kizazi baada ya kizazi; na Henoko akawa yuko juu na amenyakuliwa, hata kifuani mwa Baba, na Mwana wa Mtu; na tazama, uwezo wa Shetani ulikuwa juu ya uso wote wa dunia.

25 Naye aliwaona malaika wakishuka kutoka mbinguni; naye akasikia sauti kubwa ikisema: Ole, ole kwa wakazi wa dunia.

26 Naye akamwona Shetani; na akiwa na mnyororo mkubwa mkononi mwake, nao uliifunika uso wote wa dunia kwa giza; naye akaangalia juu na kucheka, nao malaika zake wakafurahi.

27 Na Henoko akawaona malaika wakishuka kutoka mbinguni, wakiwashuhudia Baba na Mwana; na Roho Mtakatifu akawashukia wengi, nao wakanyakuliwa Sayuni kwa uwezo wa mbinguni.

28 Na ikawa kwamba Mungu wa mbinguni akaangalia juu ya mabaki ya watu, na akalia; na Henoko analishuhudia, akisema: Yawezekanaje basi mbingu kulia, na kumwaga machozi yao kama vile mvua juu ya milima?

29 Na Henoko akamwambia Bwana: Yawezekanaje wewe kulia, kwa maana wewe u mtakatifu, nawe ni wa kutoka milele yote hadi milele yote.

30 Na kama ingeliwezekana mwanadamu aweze kuhesabu vipande vya dunia, ndiyo, mamilioni ya dunia kama hii, isingelikuwa mwanzo wa idadi ya viumbe vyako; na mapazia yako bado yamekunjuliwa; na bado wewe ungali hapo, na kifua chako kiko hapo; nawe pia u mwenye haki; u mwenye huruma na mwema milele;

31 Nawe umeichukua Sayuni kifuani kwako mwenyewe, kutoka viumbe vyako vyote, kutoka milele hadi milele yote; na hakuna kingine ila amani, haki, na kweli ndiyo makao ya kiti chako cha enzi; na neema itakwenda mbele ya uso wako na pasipokuwa na mwisho; yawezekanaje basi wewe kulia?

32 Bwana akamwambia Henoko: Tazama ndugu zako hawa; wao ni kazi ya ustadi wa mikono yangu wenyewe, nami niliwapa maarifa yao, katika siku ile niliyowaumba; na katika Bustani ya Edeni, nikampa mtu haki ya kujiamulia;

33 Na kwa ndugu zako Mimi niliwaambia, na pia nikawapa amri, kwamba yawapasa kupendana, na kwamba yawapasa kunichagua Mimi, Baba yao; lakini tazama, wao hawana urafiki jamaa zao, nao wanaichukia damu yao wenyewe;

34 Na moto wa uchungu wa hasira yangu unawaka dhidi yao; na katika hali yangu kali ya kutokufurahia nitaleta gharika juu yao, kwa maana hasira yangu kali inawaka dhidi yao.

35 Tazama, Mimi ndimi Mungu; Mtu wa Utakatifu ndilo jina langu; Mtu wa Ushauri ndilo jina langu; na Bila Mwisho na Milele ndilo jina langu, pia.

36 Kwa sababu hiyo, ninaweza kuunyosha mkono wangu na kuvishika viumbe vyote nilivyoviumba; na jicho langu laweza kuvitoboa pia, na miongoni mwa kazi za ustadi wa mikono yangu yote hapajawa na uovu mkubwa kama miongoni mwa ndugu zako.

37 Lakini tazama, dhambi zao zitakuwa juu ya vichwa vya baba zao; Shetani atakuwa ndiye baba yao, na huzuni ndiyo itakuwa hukumu yao; na mbingu yote italia juu yao, hata kazi yote ya ustadi wa mikono yangu; kwa sababu hiyo mbingu zote hazipaswi kulia, zikiwaona hawa watakaoteseka?

38 Lakini tazama, hawa ambao macho yako yapo juu yao wataangamia katika gharika; na tazama, nitawafungia; gereza niliyoiandaa kwa ajili yao.

39 Na Yule ambaye nimemchagua ameomboleza mbele ya uso wangu. Kwa sababu hiyo, yeye ameteseka kwa ajili ya dhambi zao; ili mradi wao wakitubu katika siku ile ambayo Mteule wangu atakaporejea kwangu, na hadi siku hiyo wao watakuwa katika mateso;

40 Kwa hiyo, kwa ajili hii mbingu zitalia, ndiyo, na kazi zote za ustadi wa mikono yangu.

41 Na ikawa kwamba Bwana akasema na Henoko, na akamwambia Henoko matendo yote ya wanadamu; kwa hiyo, Henoko alijua, na akautazama uovu wao, na huzuni yao, na akalia na akaunyosha mikono yake, na moyo wake ukavimba na kupanuka kama milele; na moyo wake ukatamani; na milele yote ikatikisika.

42 Na Henoko pia akamwona Nuhu, na familia yake; kwamba uzao wote wa wana wa Nuhu ulipaswa kuokolewa kwa wokovu wa kimwili;

43 Kwa hiyo Henoko aliona kuwa Nuhu alijenga safina; na kwamba Bwana alitabasamu juu yake, naye aliishika mkononi mwake mwenyewe; lakini juu ya mabaki ya waovu gharika iliwajia na kuwameza.

44 Na Henoko akiwa anaona hili, alikuwa na uchungu rohoni mwake, na akawalilia ndugu zake, na akaziambia mbingu: Nitakataa kufarijiwa; lakini Bwana akamwambia Henoko: Inua moyo wako, na ufurahi; na uangalie.

45 Na ikawa kwamba Henoko akaangalia; na kutoka kwa Nuhu, aliziona familia zote za dunia; naye akamlilia Bwana, akisema: Lini siku ya Bwana itakuja? Lini damu ya Wenye Haki itakapomwagwa, ili wale wote wenye kuomboleza wapate kutakaswa na kupata uzima wa milele?

46 Na Bwana akasema: Itakuwa katika kipindi cha meridiani, katika siku za uovu na kulipa kisasi.

47 Na tazama, Henoko aliiona siku ile ya kuja kwa Mwana wa Mtu, hata katika mwili; na roho yake ilifurahia, akisema: Mwenye haki ameinuliwa juu, na Mwanakondoo amechinjwa tangu kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu; na kwa imani mimi ni kifuani mwa Baba, na tazama, Sayuni i pamoja nami.

48 Na ikawa kwamba Henoko aliangalia juu ya dunia; naye akasikia sauti kutoka kifuani mwake, ikisema: Ole, ole wangu mimi, mama wa wanadamu; ninaumia, nimechoka, kwa sababu ya uovu wa watoto wangu. Ni lini nitapumzika, na kuoshwa kutokana na uchafu uliotoka kwangu? Lini Muumba wangu atanitakasa, ili nipate kupumzika, na haki kwa muda ikae juu ya uso wangu?

49 Na Henoko aliposikia dunia ikiomboleza, naye alilia, na akamlilia Bwana, akisema: Ee Bwana, je, hautakuwa na huruma juu ya dunia? Je, hutawabariki watoto wa Nuhu?

50 Na ikawa kwamba Henoko aliendeleza kilio chake kwa Bwana, akisema: Ninakuomba, Ee Bwana, katika jina la Mwanao wa Pekee, hata Yesu Kristo, kwamba uwe na huruma juu ya Nuhu na uzao wake, ili dunia kamwe isipate tena kufunikwa na gharika.

51 Na Bwana hakuweza kumkatalia; naye akaagana na Henoko, na akamwapia kwa kiapo, kwamba ataizuia gharika; na kwamba angewasihi watoto wa Nuhu;

52 Naye akalipeleka tangazo lisilobadilika, ili baki la uzao wake daima wataonekana miongoni mwa mataifa yote, wakati dunia ikiendelea kuwepo;

53 Na Bwana akasema: Heri yeye ambaye kupitia uzao wake Masiya atakuja; kwa maana yeye husema—Mimi ndiye Masiya, Mfalme wa Sayuni, Mwamba wa Mbingu, ambao mpana kama milele; yeyote aingiaye langoni na kupanda kwa njia ya Mimi kamwe hataanguka; kwa hiyo, heri wao niliowazungumza, kwa maana watakuja na nyimbo za shangwe isiyo na mwisho.

54 Na ikawa kwamba Henoko akamlilia Bwana, akisema: Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika mwili, dunia itapumzika? Nakuomba, nionyeshe mambo haya.

55 Na Bwana akamwambia Henoko: Angalia, naye akaangalia na akamwona Mwana wa Mtu ameinuliwa juu ya msalaba, kwa jinsi ya wanadamu.

56 Naye akasikia sauti kubwa; na mbingu zikafunikwa kwa pazia; na viumbe wote wa Mungu waliomboleza; nayo dunia ikiugulia; na miamba kupasuka; na watakatifu wakiamka, na kuvikwa taji mkono wa kuume wa Mwana wa Mtu, kwa mataji ya utukufu;

57 Na roho nyingi zilizokuwa kifungoni zilitoka, na kusimama mkono wa kuume wa Mungu; na waliosalia walihifadhiwa katika minyororo ya giza hadi hukumu ya ile siku iliyo kuu.

58 Na tena Henoko aliomboleza na kumlilia Bwana, akisema: Ni lini dunia itapumzika?

59 Na Henoko akamwona Mwana wa Mtu akapaa juu kwa Baba; naye akamlingana Bwana, akisema: Je, hautakuja tena juu ya dunia? Kwa vile wewe ndiye Mungu, nami nakujua, nawe umeniapia, na kuniamuru kwamba nikuombe katika jina la Mwanao wa Pekee; nawe umenifanya mimi, na kunipa haki ya enzi yako, na siyo kwa uwezo wangu, bali kwa neema zako wewe mwenyewe; kwa sababu hiyo, ninakuuliza kama hautakuja tena juu ya dunia.

60 Na Bwana akamwambia Henoko: Kama vile niishivyo, hata hivyo nitakavyokuja katika siku za mwisho, katika siku za uovu na kulipa kisasi, kutimiza kiapo ambacho nimekuapia juu ya watoto wa Nuhu;

61 Nayo siku yaja ambayo dunia itapumzika, lakini kabla ya siku ile mbingu zitatiwa giza, na pazia la giza litaifunika dunia; na mbingu zitatikisika, na dunia pia; na dhiki kubwa itakuwa miongoni mwa wanadamu, lakini watu wangu nitawalinda;

62 Na haki nitaishusha kutoka mbinguni; na ukweli nitaueneza kutoka duniani, ili kutoa ushuhuda wa Mwanangu wa Pekee; ufufuko wake kutoka kwa wafu; ndiyo, na pia ufufuko wa watu wote; na haki na ukweli nitavifanya viifagie dunia kama vile kwa gharika, ili kuwakusanya wateule wangu kutoka pande nne za dunia, kwenda mahali nitakapopatayarisha Mji Mtakatifu, ili watu wangu wapate kufunga viuno vyao, na kutazamia wakati wa kuja kwangu; kwani patakuwepo hema takatifu yangu, na itaitwa Sayuni, Yerusalemu Mpya.

63 Na Bwana akamwambia Henoko: Halafu wewe na mji wako wote mtakutana nao huko, nasi tutawapokea kifuani mwetu, nao watatuona; nasi tunawaangukia shingoni mwao, nao wataanguka shingoni mwetu, nasi tutapigana busu;

64 Na huko kutakuwa na makao yangu, nayo itakuwa Sayuni, ambayo itajitenga kutoka kwa viumbe vyote nilivyovifanya; na kwa kitambo cha miaka elfu dunia itapumzika.

65 Na ikawa kwamba Henoko aliiona siku ya kuja kwa Mwana wa Mtu, katika siku za mwisho, kukaa juu ya dunia katika haki kwa kitambo cha miaka elfu;

66 Lakini kabla ya siku hiyo aliona dhiki kubwa miongoni mwa waovu; na pia aliona bahari, kwamba ilikuwa ikihangaika, na mioyo ya watu ikikata tamaa, ikiangalia kwa hofu kwa ajili ya hukumu za Mwenyezi Mungu, ambazo zitakuja juu ya waovu.

67 Na Bwana akamwonyesha Henoko mambo yote, hata mwisho wa ulimwengu; naye aliiona siku ya wenye haki, saa ya ukombozi wao, na wakapokea utimilifu wa shangwe;

68 Na siku zote za Sayuni, katika siku za Henoko, zilikuwa miaka mia tatu na sitini na mitano.

69 Na Henoko na watu wake wote walitembea pamoja na Mungu, naye alikaa katikati ya Sayuni; na ikawa kwamba Sayuni ikatoweka, kwani Mungu aliipokea kifuani mwake yeye mwenyewe; na kutokea hapo ukaenea uvumi ukisema, Sayuni imekimbia.