Takasika
Toba ya kila siku huturuhusu kutambua mwongozo wa Bwana kupitia Roho Mtakatifu.
Nilipokuwa karibu na umri wa miaka mitano, nilikuwa nikicheza mpira wa miguu na marafiki zangu nyuma ya kanisa katika kijiji changu kidogo huko Côte d’Ivoire. Nakumbuka wazi wazi wito wa mhubiri kwa mkusanyiko wake wa kusafisha mavazi yao kwa maandalizi ya kuwasili kwa Mwokozi. Nikiwa mdogo, nilichukulia wito huo kwa tafsiri iliyo wazi. Nilikimbia nyumbani haraka kadiri miguu yangu midogo ilivyoweza kunibeba na kumsihi mama yangu asafishe nguo zangu chache ili zisiwe na doa tayari kwa ujio wa Mwokozi siku iliyofuata. Ingawa mama yangu alikuwa na mashaka kuhusu kurudi kwa Mwokozi hivi karibuni, bado alinifulia mavazi yangu yaliyo bora.
Asubuhi iliyofuata, nilivaa mavazi ambayo bado yalikuwa na unyevunyevu kidogo na kungoja kwa hamu tangazo la kuwasili kwa Mwokozi. Siku iliposonga na hakuna kilichotokea, niliamua kwenda kwenye nyumba ya mkutano. Nilikatishwa tamaa sana kwa kukuta kanisa likiwa tupu na Mwokozi hajafika. Unaweza kufikiria hisia zangu nilipoenda nyumbani pole pole.
Miaka mingi baadaye, nilipokuwa nikipokea masomo ya wamisionari katika maandalizi ya kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, nilisoma yafuatayo: “Na hakuna kitu kichafu kinachoweza kuingia kwenye ufalme Wake; kwa hivyo hakuna chochote ambacho huingia kwenye pumziko Lake isipokuwa wale ambao wameosha nguo zao ndani ya damu yangu kwa sababu ya imani yao, na kutubu dhambi zao zote, na uaminifu wao hadi mwisho.”
Ufafanuzi niliopata wakati huo ulinisaidia kuelewa ukweli muhimu ambao ulikuwa umetatiza akili yangu ya utoto kwa miaka mingi iliyopita. Ujumbe wa mhubiri ulikuwa umejikta kwenye umuhimu wa usafi wa kiroho. Alihimiza mkusanyiko kutafuta toba, kufanya mabadiliko katika maisha yao, na kumgeukia Mwokozi kwa ajili ya ukombozi.
Baba yetu wa Mbinguni anaelewa safari yetu ya duniani na kutoepukika kwa dhambi katika maisha yetu. Ninashukuru sana kwamba Yeye amemtoa Mwokozi ili kulipia dhambi zetu. Kupitia dhabihu ya ukombozi ya Mwokozi, kila mmoja wetu anaweza kutubu na kutafuta msamaha na kuwa safi. Toba, kanuni ya msingi ya injili, ni muhimu kwa maendeleo yetu ya kiroho na uthabiti tunapopitia changamoto za maisha.
Wakati wa mkutano mkuu wa Aprili 2022, Rais Russell M. Nelson alimwalika kila muumini wa Kanisa kupata uzoefu wa shangwe ya toba ya kila siku. Yeye alisema:
“Tafadhali usiogope au usichelewe kutubu. Shetani anafurahia taabu yako. Ikatize. Tupa mbali ushawishi wake nje ya maisha yako! Anza leo kupata uzoefu wa furaha wa kumvua mtu wa asili. Mwokozi anatupenda siku zote lakini hasa wakati tunatubu. …
Ikiwa unahisi umepotoka nje ya njia ya agano kitambo sana au kwa muda mrefu sana na hauna njia ya kurudi, hiyo si kweli.
Ikiwa kuna jambo ambalo hujatubu kikamilifu, ninakuhimiza kutii wito wa Rais Nelson wa kutoahirisha toba yako. Inaweza kuhitaji ujasiri fulani kushiriki katika mchakato huu; hata hivyo, ninaweza kukuhakikishia kwamba shangwe inayotokana na toba ya kweli inapita ufahamu. Kupitia toba, mizigo yetu ya hatia inaondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na hali ya amani na utulivu. Tunapotubu kwa dhati, tunatakaswa kupitia damu ya Mwokozi, na kuongeza usikivu wetu wa misukumo na ushawishi wa Roho Mtakatifu.
Mwenza wangu wa milele alizaliwa na ulemavu wa kusikia, na kwa sababu hiyo, lazima avae vifaa vya kusikia. Vumbi na jasho vinaweza kuathiri utendaji wa vifaa hivi, na hivyo kila asubuhi mimi humwona akisafisha kwa bidii mirija ya kuunganisha kabla ya kuvivaa vifaa. Utaratibu huu rahisi lakini thabiti huondoa uchafu wowote, unyevu au mgando, na hivyo kuboresha uwezo wake wa kusikia na kuwasiliana vizuri. Anapopuuza tendo hili la kila siku, uwezo wake wa kusikia huathiriwa siku nzima; maneno yanayosemwa polepole hufifia na hatimaye kutosikika. Kama vile usafishaji wake wa kifaa cha kusikia kila siku unavyomruhusu kusikia vizuri, toba ya kila siku huturuhusu kutambua mwongozo wa Bwana kupitia Roho Mtakatifu.
Karibu na mwisho wa huduma ya Bwana duniani na kabla ya kwenda Kwake kwenye Bustani ya Gethsemane, Yeye aliwaandaa wanafunzi Wake kukabiliana na majaribu yajayo. Yeye aliwahakikishia, akisema: “Lakini huyo Msaidizi, ambaye ni huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha mambo yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.”
Mojawapo ya kazi muhimu za Roho Mtakatifu ni kuonya, kuongoza na kumwelekeza kila mtu ambaye anasikiliza sauti laini, ya ndani kabisa. Kama vile kuziba kwa mirija ya kifaa cha kusaidia kusikia inavyoweza kuzuia utendaji kazi kwa usahihi, muunganiko wetu wa kiroho na Baba yetu wa Mbinguni unaweza pia kuathiriwa, na kusababisha dhana potofu hatari au kushindwa kutii ushauri Wake. Ujio wa mtandao umefanya habari kufikiwa kwa urahisi zaidi kuliko hapo awali. Hilo linaweza kutuongoza kuugeukia ulimwengu ili kupata mwongozo badala ya kumgeukia Mungu. Rais Russell M. Nelson amefundisha, “Katika siku zijazo, haitawezekana kuendelea kuishi kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi wa mara kwa mara wa Roho Mtakatifu.”
Ninashukuru kwamba kila mmoja wetu anaweza kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu wakati wa uthibitisho wetu. Hata hivyo, Rais Dallin H.Oaks alionya kwamba “baraka zinazopatikana kupitia kipawa cha Roho Mtakatifu zinategemea ustahili [na]‘Roho wa Bwana haishi kwenye mahekalu yasiyo matakatifu’ [Helaman 4:24].”
Tunapochagua kwa uangalifu kufuata mwongozo wa manabii na mitume, uwezo wetu wa kumfanya Roho Mtakatifu kama mwenza wetu wa daima hukua. Roho Mtakatifu hutoa uwazi katika kufanya maamuzi, mawazo yenye kuchochea na yenye misukumo ambayo huendanaa na mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni. Kuwa na Roho Mtakatifu kama mwenza wa daima ni muhimu kwa ukuaji wetu wa kiroho.
Hivi karibuni nilipewa jukumu la kuongoza mkutano katika kigingi katika Kigingi cha Salt Lake Granger West huko Utah. Wakati wa tukio hili, nilikutana na rais wa kigingi ambaye kwa bidii amekuza uwezo wake wa kutambua maongozi ya Roho Mtakatifu kupitia maisha ya haki na toba ya kila siku. Kama sehemu ya juhudi zetu za kuhudumu, tuliratibu ziara za kaya tatu. Baada ya kukamilisha ziara yetu ya mwisho, tulijikuta tukiwa na takriban dakika 30 zilizosalia kabla ya ratiba yetu iliyofuata. Tuliposafiri kurudi kwenye kituo cha kigingi, Rais Chesnut alipata hisia ya kutembelea familia moja ya ziada. Sote wawili tulikubali kufuata msukumo huu.
Tulienda kuitembelea familia ya Jones, ambapo tuligundua Dada Jones amekuwa kitandani kwa muda mrefu kwa sababu ya ugonjwa. Ilikuwa dhahiri kwamba alihitaji baraka ya ukuhani. Kwa ruhusa yake, tulimhudumia. Tulipokuwa tukijiandaa kuondoka, Dada Jones aliuliza jinsi tulivyojua kuhusu hitaji lake la haraka la baraka. Ukweli ni, sisi hatukujua. Hata hivyo, Baba yetu wa Mbinguni, ambaye alikuwa anajua mahitaji yake, alijua na kumtia moyo Rais Chesnut kutembelea nyumbani kwake. Tunapokubali mwongozo wa sauti tulivu, ndogo, tunajihami vyema zaidi kuwatumikia wale walio katika shida.
Ninashuhudia juu ya Baba wa Mbinguni mwenye ukarimu na upendo. Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wa wanadamu. Ninashuhudia kwamba Upatanisho wa Yesu Kristo ni halisi na kwamba tunapojifunza kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu, Yeye atatuongoza kutubu na kutumia nguvu za Upatanisho wa Mwokozi katika maisha yetu. Rais Russell M. Nelson ndiye nabii wa kweli na aliye hai wa Bwana, mwenye funguo zote za ukuhani duniani leo. Katika jina la Yesu Kristo, amina.