“Eliya na Makuhani wa Baali,” Hadithi za Agano la Kale (2022)
“Eliya na Makuhani wa Baali,” Hadithi za Agano la Kale
1 Wafalme 18
Eliya na Makuhani wa Baali
Nabii wa Bwana dhidi ya makuhani wa uwongo
Ufalme wa Israeli uliendelea kuteseka kwa kukosa maji. Mfalme Ahabu aliwaambia watu kumfuata mungu wa uwongo aliyeitwa Baali.
Mungu alimtuma Eliya nabii kukutana na Ahabu. Eliya aliwaalika watu wote kwenye kilele cha mlima. Aliwaalika mfalme na makuhani wake kwenye shindano ili kuona ikiwa Bwana au Baali ndiye alikuwa Mungu wa kweli.
Eliya alielezea shindano. Yeye na makuhani wangeweka sadaka ya ng’ombe juu ya madhabahu, lakini hawakutakiwa kuwasha moto wao wenyewe. Badala yake, makuhani wangeomba kwa Baali ili ashushe moto. Kisha Eliya angeomba kwa Bwana ili ashushe moto. Eliya alijua kwamba ni Mungu wa kweli pekee angeweza kushusha moto.
Makuhani wa Baali waliomba kwa mungu wao kuanzia asubuhi mpaka mchana, lakini hakuna kilichotokea. Eliya aliwadhihaki na kusema mungu wao Baali atakuwa amelala.
Makuhani walishikwa na hasira, wakaruka juu ya madhabahu na kupiga kelele mpaka jioni. Walitumaini mungu wao angejibu, lakini bado hakukuwa na moto.
Kisha ikafika zamu ya Eliya. Yeye alimjengea Bwana madhabahu, akachimba mfereji kuzunguka madhabahu na kuandaa sadaka.
Eliya aliwaomba watu wajaze maji mapipa manne na kuyamwaga juu ya kuni za madhabahu yake mara tatu. Maji yalilowesha kuni na madhabahu. Yalijaza mfereji wote.
Eliya alimuomba Bwana aonyeshe nguvu za kweli za Mungu. Moto wa Bwana ulishuka chini na kuteketeza sadaka, kuni, mawe na maji. Watu walifahamu kwamba Mungu wa Eliya alikuwa Mungu wa kweli. Eliya aliomba kwamba ukame uweze kukoma, na Bwana alituma mvua.