“Malkia Esta,” Hadithi za Agano la Kale (2022)
“Malkia Esta,” Hadithi za Agano la Kale
Esta 2–5; 7–9
Malkia Esta
Shujaa wakati wa hatari
Baadhi ya Waisraeli waliitwa Wayahudi. Esta alikuwa Myahudi aliyeishi Persia. Wazazi wake walikufa, hivyo binamu yake Mordekai alimtunza. Alialikwa kwenye jumba la mfalme pamoja na wasichana wengine katika ufalme. Mfalme alitaka malkia mpya, na alimchagua Esta.
Mfalme alikuwa na mtumishi aliyeitwa Hamani ambaye alipandishwa cheo kuwa na nguvu kubwa. Hamani alimsaidia mfalme kuongoza nchi. Mfalme alimfanya kila mmoja kumsujudia Hamani.
Lakini Mordekai hakumsujudia Hamani. Mordekai angemsujudia Bwana pekee. Hii ilimfanya Hamani awe na hasira. Alitaka kumwadhibu Mordekai na Wayahudi wote.
Hamani alimwambia mfalme kwamba Wayahudi hawakufuata sheria za mfalme. Hivyo mfalme alimruhusu Hamani kutengeneza sheria mpya: siku moja iliyopangwa, Wayahudi wote wangeuawa.
Mordekai alimwomba Esta azungumze na mfalme. Mfalme angeweza kubadilisha sheria ya Hamani na kuwaokoa Wayahudi. Lakini Esta alikuwa na hofu. Wakati mwingine mfalme aliwaua watu waliokwenda kuzungumza naye bila ya mwaliko.
Mordekai alimwomba Esta awafikirie Wayahudi ambao wangeuawa. Mordekai alisema Bwana yawezakuwa alimweka Esta kwenye jumba la mfalme ili awaokoe Wayahudi.
Esta alifahamu kwamba alilazimika kuzungumza na mfalme, hata ikiwa ingemaanisha kwamba angeuawa. Esta aliwaomba Wayahudi wote na watumishi wake wafunge pamoja naye.
Baada ya kufunga kwa siku tatu, Esta alijitayarisha na kwenda kuonana na mfalme.
Wakati alipomkaribia mfalme, mfalme alimnyooshea fimbo yake. Hii ilimaanisha mfalme alifurahi kumwona na asingemuua. Alimuuliza ni nini alichotaka. Esta alimwambia mfalme kwamba watu wake walikuwa hatarini. Kwa sababu ya sheria ya Hamani, yeye pamoja na Wayahudi wote katika ufalme wangeuawa.
Mfalme alimkasirikia Hamani na kuamuru auawe. Mfalme alitengeneza sheria mpya ambayo iliwalinda Wayahudi. Sasa waliruhusiwa kujilinda ikiwa yeyote angejaribu kuwaumiza.
Imani ya Esta katika Bwana na ujasiri wake wa kuzungumza na mfalme viliwaokoa watu wake. Badala ya kifo na huzuni, kulikuwa na sherehe. Wayahudi walisherehekea.