“Pasaka,” Hadithi za Agano la Kale (2022)
“Pasaka,” Hadithi za Agano la Kale
Pasaka
Kulindwa na Bwana
Farao hangewaacha Waisraeli kuwa huru, hivyo Bwana akamwambia Musa kwamba Yeye angeleta pigo moja la mwisho. Mtoto mzaliwa wa kwanza wa kila familia katika nchi ya Misri angekufa, hata mzaliwa wa kwanza wa wanyama wao.
Bwana aliahidi kwamba kama Waisraeli wangefuata maelekezo Yake, pigo litapita juu yao na halitowadhuru.
Bwana aliwaambia kila familia ya Israeli kutoa dhabihu ya mwanakondoo dume aliye mkamilifu na kupaza damu yake juu ya fremu ya milango ya nyumba zao.
Bwana aliwaambia Waisraeli kupika na kumla haraka yule mwanakondoo. Wakati wakila, yawapasa wawe wamevaa na tayari kuondoka na kuziacha nyumba zao. Kama Waisraeli wakifanya mambo haya, wazaliwa wao wa kwanza wangekuwa salama kutokana na pigo hilo.
Kama Bwana alivyoonya, pigo likaja. Wazaliwa wote wa kwanza katika Misri walikufa, ikijumuisha mwana mkubwa wa Farao. Lakini pigo likapita kando kwenye nyumba zenye damu kwenye fremu za mlango. Wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli wakaokolewa kwa sababu walimtii Bwana.
Farao alipoona mwanae mwenyewe alikuwa amekufa kwa sababu ya pigo hili, akawaambia Musa na Haruni wawachukue Waisraeli wote na waondoke Misri.
Waisraeli wakaondoka, lakini Farao alikasirika. Alikusanya jeshi lake na magari ya kukokotwa na farasi na akawafukuzia Waisraeli.
Waisraeli wakapiga kambi kwenye Bahari ya Shamu. Punde Farao na jeshi lake likawafikia. Waisraeli walipowaona Wamisri wakiwajia, waliogopa. Lakini Musa aliwaambia Waisraeli kwamba Bwana angewalinda.
Wamisri walivyokuwa wakikaribia, Bwana akamwambia Musa anyoshe juu fimbo yake. Musa akafanya, na Bwana akaigawanya bahari. Waisraeli wakavuka bahari kwenye nchi kavu. Wakawakimbia Farao na jeshi lake.
Jeshi la Wamisri liliwafukuzia Waisraeli. Baada ya Waisraeli wote kuvuka salama upande mwingine wa bahari, Bwana akaachilia maji yashuke chini. Jeshi la Wamisri likazama baharini.
Mwishowe Waisraeli wakawa huru. Wakaimba nyimbo, wakacheza, na wakamshukuru Bwana. Daima walikumbuka Pasaka kama wakati Bwana alipookoa maisha yao na kuwaongoza kutoka Misri.