“Yakobo na Esau,” Hadithi za Agano la Kale (2022)
“Yakobo na Esau,” Hadithi za Agano la Kale
Mwanzo 25–27
Yakobo na Esau
Kaka wawili na haki moja ya mzaliwa wa kwanza
Isaka na Rebeka walikuwa na wavulana mapacha, Yakobo na Esau. Esau alikuwa mwindaji hodari. Yakobo aliishi maisha ya kawaida na alimfuata Bwana.
Esau alizaliwa kwanza. Mzaliwa wa kwanza kwa kawaida alipokea baraka ya haki ya mzaliwa wa kwanza kutoka kwa baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ilimaanisha angeongoza familia na kuwa na ardhi kubwa na wanyama wengi ili kusaidia kuitunza familia. Lakini Esau alijijali zaidi yeye mwenyewe kuliko familia yake, na hakuwatii wazazi wake na Bwana.
Siku moja Esau alirudi kutoka mawindoni. Alikuwa na njaa kali na akamwomba Yakobo ampe chakula. Bwana alitaka Yakobo apate baraka ya haki ya mzaliwa wa kwanza kwa sababu Esau hakuistahili. Yakobo alimwomba Esau wabadilishane haki ya mzaliwa wa kwanza kwa chakula. Esau alikubali na akampa Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
Mwanzo 25:23, 29–34; Waebrania 11:20
Rebeka na Isaka walitaka kile kilicho bora kwa ajili ya watoto wao. Walikuwa na huzuni kwamba Esau aliendelea kufanya mambo aliyotaka yeye na si ambayo Bwana alitaka.
Isaka alikuwa mzee na kipofu. Kabla hajafa, alimuomba Esau kuwinda na kumpikia mnyama ili ale na afurahi.
Rebeka alijua kwamba ilikuwa ni muda kwa Isaka kutoa baraka ya haki ya mzaliwa wa kwanza.
Rebeka alimwomba Yakobo atafute wanyama wawili ili aweze kupika chakula kabla ya Esau kurejea. Kisha Yakobo angepokea baraka.
Yakobo alivalia kama Esau na kuleta chakula kwa baba yake. Isaka alimpa Yakobo baraka ya haki ya mzaliwa wa kwanza. Wakati Esau aliporejea, alimkasirikia sana Yakobo. Lakini haki ya mzaliwa wa kwanza ilimwendea Yakobo kwa sababu alitii amri za Bwana na Esau hakutii.