Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Somo la 25: Mimi Naipenda Familia Yangu Yote


Somo la 25

Mimi Naipenda Familia Yangu Yote

Madhumuni

Ni kumsaidia kila mtoto kuona upendo kwa wana familia wote.

Maandalizi

  1. Kwa maombi jifunze Luka 1:36–44, 56.

  2. Vifaa vinavyohitajika:

    1. Biblia.

    2. Picha 1-3, Familia yenye Upendo; picha 1-18, Yohana Mbatizaji Akimbatiza Yesu (Sanaa ya Picha za Injili 208; 62133);Picha 1-54, Hekalu la Salt Lake (Sanaa ya Picha za Injili 502; 62433) au picha ya hekalu la sehemu yako.

  3. Fanya maandalizi yanayohitajika kwa Shughuli zo zote za Kuboresha unazotaka kutumia.

Shughuli za Kujifunza

Mwalike mtoto atoe maombi ya kufungua.

Shughuli ya Usikivu

Imba “Happy Song” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 198), pamoja na watoto.

Nampenda mama, naye ananipenda.

Sisi twampenda baba, ndiyo bwana;

Yeye anatupenda, na unaona,

Sisi ni familia yenye furaha.

Nampenda dada; naye ananipenda.

Sisi twampenda kaka, ndio bwana;

Yeye anatupenda, na unaona,

Sisi ni familia yenye furaha.

(Kutoka Merrily We Sing, © 1948, 1975 by Pioneer Music Press, Inc. [a division of Jackman Music]. Imetumika kwa Idhini.)

Waulize watoto wasimulie kuhusu kitu ambacho wao hufanya pamoja na familia zao wakati wa wiki. Acha kila mtoto amtaje mtu mmoja katika familia yake, kama vile baba, mama, kaka, au dada.

  • Ni nani mwingine aliye sehemu ya familia yako.

Kina babu na bibi, shangazi, na binamu ni sehemu muhimu ya familia zetu

Onyesha picha 1-7, Familia yenye Upendo.

  • Ni kwa namna gani familia hii inafanana na familia yako?

  • Ni kwa namna gani familia hii inatofautiana na familia yako?

  • Ni watu gani ambao ni babu na bibi katika picha hii?

Elezea kwamba babu na bibi ni wazazi wa mama na baba zetu. Sisi wote tuna babu na bibi, ingawa wakati mwingine hatuwajui vyema kwa sababu wameishaaga dunia au wanaishi mbali sana.

  • Ni wangapi kati yenu mnawajua babu na bibi zenu?

  • Je, babu na bibi zenu wanaishi karibu au mbali sana?

  • Ni nini unapenda kufanya ukiwa pamoja nao?

Wimbo

Imbeni au semeni maneno ya “Grandmother” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 200), mkitumia vitendo vifuatavyo. Rudia kama ungependa, ukitumia Babu badala ya Bibi katika kila mstari wa mwisho katika kila aya.

Nipe busu (vidole midomoni, halafu viondoe kwa pozi).

Unanikumbatie (jikumbatie kwa mikono).

Unatabasamu unaponiona, pia (tabasamu).

Natamani kila mtoto ulimwenguni kote (nyoosha mikono).

Angekuwa na bibi kama wewe (onyesha kwa kidole).

Unanisomea kitabu (jifanye unashikilia kitabu);

Unaniimbia wimbo (fungua mdomo sana kama vile unaimba).

Unaninong’onezea kuwa unanipenda (kunja kiganja mdomoni).

Natamani kila mtoto ulimwenguni kote (nyoosha mikono).

Angekuwa na bibi kama wewe (onyesha kwa kidole).

  • Nani mwingine aliye katika familia yako? (Shangazi, wajomba, na binamu.)

Kwa ufupi elezea jinsi mashangazi, wajomba, na binamu wanavyohusiana (kwa mfano mjomba wako ni kaka ya mama.) Waache watoto waseme kuhusu mashangazi, wajomba na binamu zao.

Hadithi

Onyesha Biblia na uwakumbushe watoto kwamba tunaweza kusoma kuhusu maisha ya Yesu katika kitabu hiki. Fungua Luka 1:36–44, 56 na uelezee kwamba kabla ya Yesu kuzaliwa, Mariamu alikuwa amemtembelea Elisabeti binamu yake, ambaye pia alikuwa mjamzito. Mtoto wa Elisabeti aliitwa Yohana, na alikuwa binamu na rafiki ya Yesu. Wakati Yohana na Yesu walipokuwa watu wazima Yohana alimbatiza Yesu. Onyesha picha 1-18, Yohana Mbatizaji Akimbatiza Yesu, na waache watoto waonyeshe Yesu na Yohana.

Wana familia wanaweza kuwa marafiki wa dhati

Elezea kwamba wana familia wetu wote wanaweza kuwa marafiiki zetu wa dhati. Kama una jamaa ambaye ni mwandani, waambie watoto jinsi unavyojisikia kuhusu mtu huyu.

  • Kwa nini wewe unapenda kuwa pamoja na familia yako?

Wimbo

Imba “A Happy Family” tena pamoja na watoto. Wakati huu jumuisha mistari ya shangazi, mjomba, binamu, na babu na bibi.

  • Je, unafanya nini na mashangazi, wajomba, binamu, na kina babu na bibi?

Waambie watoto kuhusu kukutana tena kwa familia au wakati mwingine ambapo familia yako ilikusanyika pamoja kwa hafla maalum. Waache watoto waseme kuhusu karamu za familia au matembezi wanayoweza kukumbuka.

Elezea kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walipanga kwa ajili yetu tuwe na familia zetu milele. Onyesha picha 1-54, Hekalu la Salt Lake, na picha ya hekalu la sehemu yenu. Kwa ufupi elezea kwamba kama tunaoana katika hekalu na kuishi kwa wema, tunaweza kuwa na familia zetu milele.

Ushuhuda

Waambie watoto kuhusu upendo wako kwa wanafamilia wako. Sisitiza kwamba familia zetu ni baraka kwetu. Wahimize watoto wawe na upendo na wakarimu kwa wanafamilia wao.

Shughuli za Kuboresha

Chagua baadhi ya shughuli hizi ili uzitumie katika somo hilo.

  1. Kwa idhini ya rais wako wa Msingi, waalike babu au bibi wa mmoja wa watoto wa darasa, au mtu katika kata ambaye ni babu au bibi aje kutembelea darasa. Acha mgeni awasimilie watoto kuhusu upendo wake kwa wajukuu. (Au unaweza kumwalika shangazi, mjomba, au binamu ya mmoja wa watoto kuzungumza kuhusu upendo wake kwa wanafamilia wote)

  2. Lete picha moja au zaidi ya familia yako, hasusani zile zinazojumuisha kina babu au bibi, mashangazi, wajomba, au binamu. Waache watoto wakutambue wewe na mtu mwingine wanayemjua (kama mwenzi wako au watoto) katika picha. Waambie watoto kuhusu watu wengine katika picha.

  3. Mpe kila mtoto kibandiko chenye jina la mwanafamilia, kama vile “Mama,” “Baba,” “Dada,” “Babu,” “Bibi,” “Mjomba,” “Shangazi,” au “Binamu.” (Kama una watoto wachache katika darasa lako, tumia tu baadhi ya majina; kama una watoto wengi katika darasa lako, zaidi mtoto mmoja wanaweza kuwa na majina yanayofanana.) Acha mtoto aje mbele ya chumba na useme jina lililo katika kibandiko chake. Elezea kwamba familia ni muhimu na zilipangiwa kuwa pamoja. Acha watoto watengeneze duara na kushikana mikono. Waambie wafanye vitendo kadhaa huku wakishikana mikono, kama vile kubembeza mikono yao, wakitembea katika duara, na wakiimba “A Happy Family.”

  4. Imbeni au semeni maneno ya “I Have a Family Tree” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk 199).

  5. Acha mtoto achore picha ya babu na bibi yake au jamaa zake wengine. Andika picha hii Babu na Bibi zangu au kile kinachofaa.

Shughuli za Ziada Kwa Watoto Wadogo

  1. Tengeneza sanduku au mfuko uliochorwa moyo kuashiria upendo. Kata picha rahisi au michoro ambayo inawawakilisha wana familia wa karibu na jamaa. Waulize watoto, “Ni nani anakupenda?” Watoto wanapojibu, weka picha inayofaa katika sanduku au mfuko. Picha zote sandukuni au mfukoni, ziinue juu na waambie watoto, “Watu wote hawa wanawapenda sana.”

  2. Weka mikato ya wanafamilia (ona shughuli 1, hapo juu) kwenye meza au sakafuni. Acha watoto wazunguke au wafunge macho huku ukiondoa mkato mmoja. Acha watoto wabahatishe ni nani asiyekuwepo. Rudia mara nyingi kama ungependa kufanya hivyo. Weka mikato yote tena na uwaambie watoto kwamba Baba wa Mbinguni anataka familia ziwe pamoja na yeye tena, pasipo kukosekana hata mmoja.

  3. Imba “When We’re Helping” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 198), ukitumia majina ya jamaa wa familia badala ya mama. Acha waigize mambo wanayoweza kufanya ili kuwasaidia wanafamilia hawa.