Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Somo la 39: Muziki Hunifanya Kuwa na Furaha


Somo la 39

Muziki Hunifanya Kuwa na Furaha

Madhumuni

Ni kumsaidia kila mtoto kuelewa kwamba muziki mzuri unaweza kutusaidia kuhisi furaha na kutukumbusha juu ya Baba wa Mbinguni na Yesu.

Maandalizi

  1. Kwa maombi jifunze Samweli 16:19–23; Etheri 6:2–12; na Mafundisho na Maagano 25:12.

  2. Vifaa vinavyohitajika:

    1. Biblia, Kitabu cha Mormoni, na nakala ya Mafundisho na Maagano.

    2. Picha 1-61, Kutoka Nauvoo (Picha za Sanaa za Injili 410; 62493); Daudi Akimchezea Mfalme Saulo; picha 1-69, Mashua za Wayaredi.

  3. Fanya maandalizi yanayohitajika kwa Shughuli zo zote za Kuboresha unazotaka kutumia.

Taarifa kwa mwalimu: Ukitaka unaweza kumwalika mwalimu wa muziki wa watoto wa Msingi ili kukusaidia katika somo hili.

Shughuli za Kujifunza

Mwaalike mtoto atoe maombi ya kufungua.

Shughuli ya Usikivu

Acha watoto wafanye duara na kuimba “If You’re Happy” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 266) mara kadhaa, wakitumia vifungu vya maneno kama vile “gonga kwa vidole vyako,” na “pepesa macho yako.” Buni vitendo kama inavyopendezwa na maneno.

Kama una furaha na unajua, piga makofi.

Kama una furaha na unajua, piga makofi.

Kama una furaha na unajua.

Basi uso wako utaonyesha.

Kama una furaha na unajua, piga makofi.

  • Ulijisikia vipi ulipoimba wimbo huu?

Muziki mzuri unaweza kutusaidia kujisikia wenye furaha

Elezea muziki wa furaha, maridadi, au wa amani unaweza kutusaidia kujisikia vyema moyoni. Tunapokuwa na huzuni, kukasirika, au kuwa na hofu, muziki mzuri unaweza kutusaidia kujisikia furaha tena.

Hadithi

Onyesha picha 1-68, Daudi Akimchezea Mfalme Saulo. Simulia hadithi ya Daudi akimchezea kinubi Mfalme Saulo ambaye alikuwa anaumwa, kama inavyopatikana katika 1 Samweli 16:19–23.

  • Kwa nini unafikiri muziki wa Daudi ulimfanya Mfalme Saulo kujisikia vyema?

  • Ni chombo gani cha muziki unapendelea kusikiliza?

Kwa kifupi igiza kucheza vyombo hivi bila kuimba vinapotajwa.

Shughuli

Acha kila mtoto ajifanye anacheza chombo cha muziki, kama vile piano, violin, fluti, au kinubi, wakati wewe ukiimba wimbo wa watoto wa Msingi unaojulikana bila kufungua mdomo.

Wimbo

Elezea kwamba kuimba pia kunaweza kutusaidia sisi kujisikia furaha. Imba “Happy Song” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 264), ukitumia matendo yaliyooelezwa hapo chini.

Mabata bwawani wanaimba wimbo wa furaha (fungua na ufunge dole gumba na vidole kama vile mdomo wa bata).

Mama kuku analia siku nzima (weka mikono kama vile mabawa).

Ndege katika viota vyao (weka mikono kama umbo la kiota) na upepo vileleni mwa miti (punga mikono juu ya kichwa kama vile miti ikipigwa na upepo).

Wote wanajiunga kuimba wimbo wa furaha.

(© 1963 na D. C. Heath and Company. Umepigwa chapa tena kwa Idhini.)

  • Ni nyimbo gani za watoto wa Msingi ambazo zinakusaidia kujisikia mwenye furaha?

Wimbo

Acha watoto wachague wimbo waupendao, na uimbe pamoja nao.

Hadithi

Onyesha picha 1-61, Kuondoka kutoka Nauvoo, na usimulie hadithi ifuatayo kwa maneno yako mwenyewe:

Wakati watangulizi walipoacha nyumba zao huko Nauvoo na kwenda magharibi, walifungasha kila kitu walichoweza katika magari ya kukokotwa au mikokoteni iliyokuwa imefunikwa. Iliwabidi waache vitu vyao vingi nyuma kwa sababu hakukuwa na nafasi ya kubeba. Safari ilikuwa ngumu, na watangulizi hawa kwa kawaida walikuwa wanachoka sana mwisho wa siku.

Usiku watangulizi hawa walikusanya wanyama wao na magari yao katika duara na kuwasha moto mkubwa katikati ya ile duara. Brigham Young, nabii, alijua watu wangekuwa na furaha katika safari yao kama wangekuwa na muziki. Aliwahamasisha waimbe na kucheza. Watangulizi waliokuwa wameleta fidla, tarumbeta, na ngoma walizitumia kucheza muziki. Kila mtu aliimba na kucheza karibu na moto. Mojawapo ya wimbo walioupenda ilikuwa “Njooni, Njooni, Watakatifu.” Muziki uliwapa watangulizi hawa nguvu na ujasiri. Wakati walipokwenda kulala usiku baada ya kuimba na kucheza, walijisikia furaha.

Wimbo

Acha watoto wakae chini katika duara na wajifanye kuwa watangulizi waliokaa kuzunguka moto. Imbeni “Pioneer Children Sang As They Walked” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 214) au wimbo mwingine wa watoto wa Msingi unaopendwa na watoto.

Muziki hutusaidia kumkumbuka Baba wa Mbinguni na Yesu

Elezea kwamba muziki wa kanisani hutukumbusha juu ya Baba wa Mbinguni na Yesu. Waombe watoto wafunge macho na kujifanya wanasikiliza muziki unaopigwa kanisani kabla ya mkutano wa Sakramenti.

  • Muziki unaweza kukusaidia vipi kuwa na staha kanisani?

Elezea kuwa Baba wa Mbinguni na Yesu wanapenda kutusikia tukiimba. Soma kwa sauti vishazi viwili vya kwanza vya Mafundisho na Maagano 25:12 (hadi sala kwangu Mimi). Elezea kwamba kuimba nyimbo za kanisa ni kama kusali kwa Baba wa Mbinguni. Tunamshukuru Baba wa Mbinguni kwa baraka anazotupa sisi. Kuimba nyimbo kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu hutukumbusha kwamba wao wanatupenda na wanataka kutusaidia. Elezea kwamba nyimbo tunazoimba katika mkutano wa Sakramenti zinaitwa nyimbo za dini.

  • Kwa nini sisi huimba nyimbo na nyimbo za dini kanisani?

Hadithi

Onyesha picha 1-69, Mashua za Wayaredi, na usimulie hadithi ya Wayaredi wakienda katika nchi ya ahadi, kama inavyopatikana katika Etheri 6:2–12. Elezea kwamba Wayaredi waliimba nyimbo katika safari yao baharini.

  • Kwa nini unafikiri waliimba nyimbo katika safari yao baharini?

  • Je, unafikiri Wayaredii walijisikia vipi upepo na mawimbi yalipopiga mashua zao?

  • Je, kuimba kungewasaidiaje wakati walipokuwa na uoga?

  • Je, ulishawahi kuimba wimbo wakati ulipokuwa na uoga? Je, ilikusaidia vipi?

Ushuhuda

Elezea juu ya wakati muziki ulipokufanya ujisikie furaha. Wakumbushe watoto kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu wanapenda kutusikia tukiimba nyimbo nzuri. Wanapoimba, wanaweza kujisikia furaha na kukumbuka kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu wanawapenda.

Shughuli zenye Kuboresha

Chagua baadhi ya shughuli hizi ili uzitumie katika somo.

  1. Imba “Fun to Do” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 253, “Sing a Song” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 253), au “I Think the World Is Glorious” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk,. 230).

  2. Kama darasa ni dogo, acha kila mtoto achague wimbo wa Msingi aupendao, na kisha waimbe hizo nyimbo pamoja kama darasa.

  3. Tengeneza manyanga ya vikombe vya karatasi kwa ajili ya watoto kutumia kama vyombo vya mdundo wa muziki. Weka mchele au mchanga kidogo ndani ya kikombe cha karatasi. Unganisha kwa gundi kikombe cha pili na kile cha kwanza ili kwamba mchele au mchanga usimwagike. Imba wimbo wa wa watoto wa Msingi wakati huo watoto wanatumia manyanga yao. Pia unaweza kuleta vyombo vingine na kuvitumia kama vyombo vya mdundo wa muziki kama vile njuga, vijiti butu vya kugonganisha pamoja au vipande vya mbao vya kugonganisha.

  4. Cheza wimbo kutoka katika Kitabu cha Nyimbo za Watoto kanda ya kaseti (52505 au 52428) au diski (50505 au 50428), na uwaache watoto waimbe pamoja nazo au waendane nazo.

  5. Kwa maneno yako mwenyewe, simulia hadithi ya wakati Nabii Joseph Smith na viongozi wa Kanisa walipokuwa katika Gereza la Carthage. Watu waovu waliwaweka gerezani licha ya kuwa hawajafanya kosa lo lote. Nabii alijua maisha yake yalikuwa hatarini, na alisikia huzuni sana. Alimwomba rafiki yake John Taylor amwimbie. John pia alikuwa na huzuni sana, na akamwambia Joseph kwamba yeye hakujisikia kuimba, lakini Joseph alimtia moyo. John alipoanza kuimba kuhusu Yesu, kila mtu gerezani alijisikia vyema. Wimbo huo uliwakumbusha wao kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu wanawapenda. Uliwapa nguvu na ujasiri.

Shughuli za Ziada Kwa Watoto Wadogo

  1. Imba baadhi ya nyimbo za watoto zinazopendwa pamoja nao. Au acha watoto wapige makofi huku wakiimba. Zungumza na watoto kuhusu jinsi muziki unavyowafanya kuwa na furaha.

  2. Andaa aina mbali mbali za mitindo ya muziki kwa watoto wasikilize. Hakikisha muziki unafaa kwa siku ya Sabato. Ukitaka waweza kutumia baadhi ya kanda za nyimbo ambazo huambatishwa na kitabu hiki cha kiada.

  3. Waambie watoto kwamba Baba wa Mbinguni ametupa aina nyingi tofauti za muziki. Baadhi ya muziki umetengenezwa na watu, muziki mwingine umetengenezwa na vitu vilivyo katika ulimwengu unaotuzunguka. Taja vitu kadhaa vya asili vinavyotoa sauti ambayo ni kama muziki, kama vile upepo, mvua, ndege, na radi. Acha watoto waigizie kila sauti.