Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Somo la 44: Sote Tunaweza Kusaidia Kanisani


Somo la 44

Sote Tunaweza Kusaidia Kanisani

Madhumuni

Ni kumsaidia kila mtoto kuelewa kwamba kila muumini wa kata au tawi anaweza kusaidia kanisani.

Maandalizi

  1. Jifunze kwa maombi 1 Nefi 17:7–15; 18:1–4.

  2. Tengeneza kadi ya kawaida ya shukrani kwa kila mtoto ili apake rangi na kumpa rais wa Msingi au mtu yeyote ambaye huwasadia watoto kanisani. Unaweza kuchora ua ukipenda upande wa mbele wa karatasi iliyokunjwa na uyaandike maneno Asante sana upande wa ndani

  3. Vifaa vinavyohitajika:

    1. Kitabu cha Mormoni

    2. Ufito wa kuvulia samaki na samaki kutoka somo la 11. Kwenye kila samaki weka kidokezo kuhusu askofu au rais wa tawi, kama vile “Yeye hukaa mbele jukwaani kanisani,” “Yeye husaidia watu wa kata [au tawi],” au “Sisi tunaweza kumpa yeye zaka zetu.”

    3. Chombo chenye krayoni au penseli.

    4. Picha 1-8, Kupitisha Sakramenti (62021); picha 1-67, Darasa lenye Staha; picha 1-71, Kujenga Mashua.

  4. Fanya maandalizi yanayohitajika kwa Shughuli zo zote za Kuboresha unazotaka kutumia.

Shughuli za Kujifunza

Mwaalike mtoto atoe maombi ya kufungua.

Shughuli ya Usikivu

Weka kiti katikati ya darasa na ujaribu kukiinua kwa kuinua mguu mmoja kati ya miguu yake. Elezea kwamba kuna mambo mengi ambayo sisi hatuwezi kuyafanya isipokuwa tu kwa kuyafanya kwa pamoja. Waalike watoto watatu kila mmoja atwae mguu mmoja wa kitu na wakusaidie wewe kukiinua kiti hicho inchi chache kutoka sakafuni. Elezea kwamba endapo kila mmoja anafanya kazi kwa pamoja, tunaweza kufanya mambo mengi ambayo hatuwezi kuyafanya tukiwa peke yetu.

Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wanatutaka tufanye kazi pamoja

Hadithi

Onyesha picha 1-71, Kujenga Mashua, na kwa ufupi simulia hadithi ya Nefi na familia yake wakijenga mashua, kama ilivyo katika 1 Nefi 17:7–15 na 1 Nefi 18:1–4. Sisitiza kwamba Nefi alihitaji msaada wa Bwana (Yesu) na wa familia yake katika kujenga mashua.

  • Kwa nini Nefi hakuweza kujenga mashua bila msaada?

  • Ni kwa namna gani Bwana alimsaidia Nefi ? (Ona 1 Nefi 17:8–10,; 1 Nefi 18:1.)

  • Ni kwa namna gani familia yake ilimsaidia Nefi ? (Ona 1 Nefi 18:1.)

  • Ni nini kilitokea wakati kila mtu alipofanya kazi kwa pamoja? (Ona 1 Nefi 18:4.)

Waruhusu watoto waongee kuhusu uzoefu wo wote waliopata walipokuwa wanafanya pamoja na wengine.

Shughuli

Elezea kwamba sisi pia tunafanya kazi pamoja kanisani. Kila mtu katika kata au (tawi) huwasaidia wengine. Jifanye, kwa maneno au vitendo, kama mtu anayewasaidia washiriki wa darasa lako kanisani kila wiki, kama vile kiongozi wa kuimba, mpiga kinanda, mwalimu, au rais wa Msingi. Acha watoto wabahatishe kwa kutaja kile wewe unajifanya kuwa. Baada ya watoto kubahatisha wewe ni nani, elezea majukumu ya wito wa mtu huyo. Rudia mara nyingi kama upendavyo.

Onyesha picha 1-8, Kupitisha Sakramenti

  • Huyu shemasi anafanya nini?

  • Je, unamjua mtu yeyote anayepitisha sakramenti?

Elezea kwamba wavulana wenye Ukuhani wa Haruni hutayarisha, kubariki, na kupitisha sakramenti. Hizi ni njia ambazo wavulana wanaweza kusaidia kanisani.

Shughuli

Elezea kwamba kuna mtu fulani katika kata yako au tawi lako ambaye humsaidia kila mtu kanisani. Baba wa Mbinguni amempa mtu huyu kazi muhimu ya kufanya. Acha watoto wachukue zamu kuvua vidokezo kwenye samaki wa karatasi. Soma kila kidokezo kwa sauti. Endelea mpaka vidokezo vyote vimesomwa, kisha acha watoto wabahatishe mtu huyu ni nani.

  • Jina la askofu wetu au (rais wa tawi letu) ni nani?

  • Ni mambo gani muhimu ambayo yeye hufanya katika kutusaidia sisi?

Jadili kazi zilizofanywa na watu wengine katika kata yako au tawi lako, kama vile walimu wa nyumbani na walimu watembeleaji. Ukitaka waweza kuzungumza kuhusu miito ambayo wanafamilia za watoto wa darasa lako wanayo.

Sisi tunaweza kusaidia kanisani

Shughuli

Tawanya chombo cha krayoni au penseli sakafuni. Muombe mmoja wa watoto aziokote, na pima muda atakaotumia kuziokota. Tawanya vifaa hivi tena. Acha darasa zima lifanye kazi pamoja, na upime itachukua muda gani. Elezea kwamba wakati kila mtu akifanya pamoja, tunaweza kufanya kazi vizuri zaidi.

  • Unaweza kufanya nini ili kusaidia kanisani?

Wasaidie watoto kufikiria juu ya njia wanazoweza kusaidia kanisani, ikijumuisha kusafisha jumba la mikutano, kuwa wakarimu kwa wengine, kuwasaidia watoto ambao wana huzuni au wanaogopa, na kuwa na staha wakati wa mikutano.

  • Tunawezaje kusaidia katika kuweka darasa letu na jumba la mikutano kuwa safi?

  • Tunawezaje kuwasaidia watu wengine kanisani?

Onyesha picha 1-67, Darasa lenye Staha.

  • Ni kwa namna gani watoto hawa husaidia kanisani?

  • Ni kwa namna gani huwasaidia wana darasa wenzetu sisi tunapokuwa na staha?

  • Ni kwa namna gani humsaidia mwalimu wakati kila mmoja anapokuwa na staha?

  • Tunajisikiaje kila mmoja anapokuwa na staha?

Shughuli

Elezea kwamba njia nyingine tunayoweza kusaidia kanisani ni kwa kusema “Asante sana” kwa watu ambao wanafanya mambo kwa ajili yetu. Acha watoto wachore kadi za kutoa shukrai mlizoandaa, na mzipeleke wakati wa darasa kama inawezekana.

Ushuhuda

Toa shukrani kwa watu wote ambao wanasaidia katika kata au tawi. Sema jinsi unavyojisikia kuhusu kufanya kazi ya Baba wa Mbinguni kwa kuwa mwalimu wa watoto wa darasa la Msingi.

Shughuli zenye Kuboresha

Chagua baadhi ya shughuli hizi ili uzitumie katika somo.

  1. Imbeni au semeni maneno ya “Our Bishop” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 135). Acha watoto wasalimiane kwa kupeana mikono wakati neno askofu linapotajwa.

  2. Kama inawezekana, nendeni kwa matembezi kanisani na uwaonyeshe watoto pale askofu (au rais wa tawi) hukaa wakati wa mkutano wa sakramenti. Acha watoto wachuke zamu kukaa kwenye viti. Kisha waonyeshe watoto pale ofisi ya askofu (au rais wa tawi) ilipo.

  3. Rusha au mpe mtoto chombo laini kama vile mpira au kijifuko cha maharagwe, na umuulize yeye amtaje mtu katika kata (au tawi) ambaye husaidia kanisani na aeleze jinsi mtu huyo anavyosaidia. Kisha acha huyo mtoto akurudishie chombo hicho. Endelea mpaka kila mtoto apate angalao zamu moja.

  4. Kwa idhini ya rais wako wa Msingi, mwalike mshiriki wa uaskofu au kiongozi mwingine wa kata atembelee darasa na kuwaambia watoto kile ambacho yeye hufanya katika kusaidia kanisani.

  5. Chora mchoro wa sura rahisi kwenye ubao au kwenye kipande cha karatasi duara kwa kila mtoto. Wape watoto krayoni au penseli, na uache kila mtoto aongeze rangi ya nywele zake mwenyewe. Waambie watoto kwamba kama wewe ukisema kitu kilicho sahihi kuhusu jinsi wanavyosaidia kanisani, wanapaswa kuinua juu sura zao za karatasi. Kama kauli si kweli, wanapaswa kuziacha mapajani mwao. Tumia kauli kama vile—

    • Ninapaswa kutupa karatasi chini ya kiti changu.

    • Ninapaswa kuwashukuru watu wanaonisadia kanisani.

    • Ninapaswa kukimbia kwenda darasani.

    • Ninapaswa kuwa na staha kanisani.

Shughuli za Ziada Kwa Watoto Wadogo

  1. Cheza “Fuata Kiongozi” pamoja na watoto. Acha watoto wasimame katika mstari. Mtoto wa kwanza katika mstari akimbie, aruke, aruke kamba, au afanye kitendo upande mwingine wa chumba. Watoto wengine wamwigize mtoto wa kwanza, kwa kufanya kile anachofanya. Kisha mtoto wa kwanza aende mwisho wa mstari, na mtoto anayefuata anakuwa kiongozi mpya. Endelea mpaka kila mtoto apate zamu ya kuwa kiongozi.

    Baada ya mchezo wakumbushe watoto kwamba askofu ndiye kiongozi wa kata. Yeye anataka sisi tufanye mambo ambayo yatatuongoza sisi kurudi kwa Baba wa Mbinguni.

  2. Imbeni wimbo ”Do As I’m Doing” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 276), mkitumia kitendo kinachopendekezwa na mmoja wa watoto wa darasa. Rudia wimbo vya kutosha ili kila mtoto awe amepata zamu ya kuchagua kitendo.