Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Somo la 33: Naweza Kuwa Rafiki


Somo la 33

Naweza Kuwa Rafiki

Madhumuni

Ni kumsaidia kila mtoto atamani kuwa rafiki mwema.

Maandalizi

  1. Kwa maombi jifunze Yohana 6:1–13 na 11:1–7, 17–44.

  2. Vifaa vinavyohitajika:

    1. Biblia.

    2. Picha 1-3, Yesu Kristo (Picha za Sanaa za Injili 240; 62572).

  3. Fanya maandalizi yanayohitajika kwa Shughuli zozote za Kuboresha unazotaka kutumia.

Shughuli za Kujifunza

Mwaalike mtoto atoe maombi ya kufungua.

Shughuli ya Usikivu

Jinyoshee mwenyewe kidole na ujiulize, “Mimi ni nani? Watoto wanaweza kujibu kwa kutaja jina lako au neno mwalimu. Elezea kwamba wewe pia ni rafiki yao na wao ni marafiki zako. Elezea kwamba marafiki ni watu ambao wanapendana.

Kusanyika pamoja na watoto katika duara. Ukimtazama kila mtoto kwa zamu, sema “(Jina la mtoto) ni rafiki yangu.” Acha kila mtoto apate zamu ya kufanya hivyo, ukihakikisha kwamba kila mtoto anatajwa kwa zamu.

Sisi tuna marafiki wengi

  • Marafiki zako ni kina nani?

Waache watoto waseme kuhusu marafiki zao. Sema kwamba marafiki wanaweza kuwa wa umri wo wote. Wana familia wanaweza kuwa baadhi ya marafiki zako wa dhati. Sisitiza kwamba kila mtu katika darasa ni rafiki.

Onyesha picha 1-3, Yesu Kristo. Elezea kwamba mtu aliyeko katika picha ni rafiki mwema sana kwa kila mtu darasani.

  • Ni nani aliye rafiki yetu katika picha hii?

  • Unajuaje kuwa Yesu Kristo ni rafiki yako?

Wimbo

Imbeni au semeni maneno ya “Jesus Is Our Loving Friend” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 58).

Yesu Kristo ni rafiki yetu mwenye upendo.

Yeye daima yu karibu.

Yeye atatuongoza tunaposali.

Kila mtoto ni mpendwa.

Hadithi

Simulia hadithi ya Yesu akimfufua Lazaro kutoka kwa wafu, kama inavyopatikana katika Yohana 11:1–17, 17–44. Sisitiza kwamba Lazaro na dada zake walikuwa marafiki wa Yesu. Wakati Yesu alipokuwa Bethania, aliishi katika nyumba yao na kula chakula pamoja nao.

  • Yesu alijisikia vipi juu ya Lazaro? (Ona Yohana 11:3, 35–36.)

  • Yesu alimfanyia nini Lazaro? (Ona Yohana 11:43–44.)

  • Unafikiri Lazaro, Mariamu, na Matha walijisikia vipi juu ya Yesu?

Tunaweza kuwa marafiki wema

  • Tunapaswa kuwatendea vipi marafiki zetu?

Elezea kwamba tunapokuwa marafiki wema, tunawasaidia wengine kuwa, na kufanya matendo mema. Tunawajali marafiki zetu na tunataka wao wawe na furaha. Jadili umuhimu wa kuwatendea wengine kwa njia ambayo sisi tungependa kutendewa. Waulize watoto jinsi wanavyoweza kuwa marafiki wema katika hali hizi zote:

  • Wewe na rafiki yao mnacheza pamoja, na mtoto mwingine anakuja na anataka kucheza pamoja nanyi.

  • Mtoto mpya anakuja darasani kwa mara ya kwanza na anaona haya au anaogopa.

  • Mtoto amekejeliwa na anajisikia vibaya.

Wimbo

Imbeni au semeni maneno ya “Kindness Begins with Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 145).

Nilitaka niwe mkarimu kwa kila mtu,

Kwani hivyo ni vyema, unaona.

Kwa hivyo najisemea, “Kumbuka hili:

Ukarimu unaanza na mimi.

  • Unajisikia vipi wakati marafiki zako wanapokuwa wakarimu kwako?

  • Je, unafikiri wao wanajisikia vipi wakati unapokuwa mkarimu kwao?

Wasaidie watoto kuelewa kwamba kama wanataka kuwa na marafiki, lazima wao wenyewe wawe marafiki wema.

Marafiki hushirikiana

  • Kama unacheza na (taja jina la wamasesere au kitu fulani mahususi), na rafiki anakuja kucheza na wewe unapaswa kufanya nini?

Elezea kwamba wakati tunapomruhusu mwingine kucheza na sisi, au wakati tunapotoa baadhi ya vile tulivyonavyo kwa mtu mwingine, sisi tunashirikiana. Wakati mwingine hatuwezi kugawa kile tulichonacho, kwa hivyo tunakitumia kwa zamu. Hiyo pia ni kushirikiana

  • Kama mmoja wa marafiki zako ana njaa na wewe una chakula, unapaswa kufanya nini?

Hadithi

Onyesha Biblia na usimulie hadithi ya Yesu akiwalisha watu elfu tano, kama inavyopatikana katika Yohana 6:1–13. Sisitiza kwamba kwa sababu mvulana mdogo alitoa chakula alichokuwa nacho, Yesu aliweza kutumia nguvu zake za kutengeneza chakula cha kuwalisha watu wote.

Wakumbushe watoto hadithi ya Eliya na mjane wa Sarepta (iliyosimuliwa katika somo la 32). Mjane alibarikiwa kwa sababu alitoa chakula chake hata ingawa hakuwa na cha kutosha.

  • Tunaweza kutoa nini kwa marafiki zetu?

  • Tunaweza kushirikiana nini na familia zetu?

Wimbo

Acha watoto wasimame na kuimba “Fun to Do” (Kitabu cha Nyimbo cha Wtoto, uk. 253), wakitumia sentensi “Kushirikiana (wanasesere wangu, kitabu, au cho chote kile wanachopendekeza watoto) ambacho ni furaha kufanya.” Acha watoto wabuni matendo yanayoendana na maneno hayo.

Kutoa wanasesere wangu ni furaha kufanya,

Yafurahisha kutenda, kutenda, kutenda!

Kutoa wanasesere wangu ni furaha kufanya,

Yafurahisha kutenda, kutenda, kutenda!

(© 1963 by D. C. Heath and Company. Imechapishwa tena kwa Idhini.)

Wakumbushe watoto kwamba marafiki husaidiana, na kutiana moyo ili kusaidia kusafisha darasa kama inavyohitajika.

Ushuhuda

Toa ushuhuda wako wa umuhimu wa kuwa rafiki mwema. Unaweza kuelezea uzoefu wako binafsi kuhusu rafiki yako. Wakumbushe watoto kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu ni marafiki zetu na wanatupenda sisi. Wahimize watoto wawe wakarimu kwa marafiki zao wiki hii.

Shughuli za Kuboresha

Chagua baadhi ya shughuli hizi ili uzitumie katika somo.

  1. Imbeni au semeni maneno “‘Give,’ Said the Little Stream” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 236, au “Jesus Said Love Everyone” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 61, au ). “Friends Are Fun” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk. 262).

  2. Imbeni au semeni maneno ya “We Are Different” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk. 263). Wasaidie watoto kuelewa kwamba tunapaswa kuwa marafiki na wale wanaoonekana kuwa tofauti nasi pamoja na wale pia walio kama sisi.

  3. Acha watoto wasimame na kufanya mstari kitendo “Rafiki Mdogo Mpendwa”:

    Nina rafiki mdogo mpendwa (jikumbatie mweyewe);

    Mimi humwona yeye kila siku.

    Mimi nampenda rafiki yangu mdogo mzuri.

    Hivi ndivyo tunavyocheza:

    Tunacheza na wanasesere (jifanya unamliwaza mwanasesere mikononi);

    Tunatupa mipira yetu (jifanye unatupa mpira);

    Tunatembea kama (tembea kwa utulivu).

    Tunacheza na bembea (jifanye unabembea);

    Tunaweza kuongea na kuimba;

    Kama vile marafiki wote wema tunapaswa kufanya (kunja mikono na uinamishe kichwa).

  4. Leta vitafunwa kidogo kwa ajili ya darasa (zungumza na wazazi wa watoto ili kuhakikisha hakuna mtoto yo yote anayeweza kudhurika na vitafunwa). Weka vitafunwa kwenye meza au kiti ambapo wanafunzi wataweza kuviona. Sema jinsi vinavyoonekana vizuri na uwaulize watoto kama wangetaka kuvila. Waulize watoto jinsi ambavyo wangejisikia kama ungeshiriki vitafunwa hivyo na baadhi yao tu. Jadili jinsi ambavyo wengine wangejisikia wasipojumuishwa. Shiriki vitafunwa hivyo na watoto.

  5. Acha mtoto achore picha yake mwenyewe akishirikiana na rafiki. Andika kila picha Naweza kushiriki na rafiki yangu.

  6. Simulia hadithi ifuatayo kwa maneno yako mwenyewe:

    Viatu vya Ncha ya Shaba

    Wakati watangulizi walipokuja kuishi Utah, wengi wao walikuwa maskini. Walikuwa wametumia hela zao zote kununua vitu kwa ajili ile safari ndefu na walinunua vifaa ambavyo wangehitaji kujengea nyumba na kulima mashamba. Kwa sababu watu hawakuwa na hela nyingi, watoto wengi walikuwa na jozi moja tu ya viatu, ambavyo walivivaa Jumapili. Kila mara walitembea pekupeku siku zingine za wiki.

    Msichana mmoja mtangulizi aliyeitwa Melinda alikuwa na viatu vizito, vyenye sura mbaya, vyenye ncha ya shaba ambavyo alivaa majira ya baridi. Katika majira ya joto familia yake ilimnunulia viatu vizuri sana, vinavyofaa Jumapili, na alikuwa avivae kwenye maonyesho.

    Rafiki wa dhati wa Melinda, Amanda, hakuwa na viatu kamwe. Melinda alimsikitikia Amanda na akamwomba mama ruhusa amwazime Amanda jozi ya viatu ili avae kwenye maonyesho. Wakati Melinda akitwaa, viatu vyake vya zamani vyenye ncha ya shaba na kumpelekea rafiki yake, mama yake alisema, “Kama utamwazima, unapaswa kutoa kile ambacho wewe mwenyewe ungependa kupokea.”

    Melinda akawaza sana kwa dakika chache. Akifikiria kuhusu kile ambacho Yesu angekifanya. Akifikiria kuhusu ni viatu gani ambavyo angevaa, na kisha akaamua. Akatwaa viatu vyake vipya vya Jumapili kwa rafiki yake ili avalie, na akaenda kwenye maonyesho kama amevaa viatu vya zamani vyenye sura mbaya vyenye ncha za shaba. Lakini Melinda alijisikia mwenye furaha sana! Alijua kuwa alikuwa anatoa kama vile Yesu angependa yeye afanye.

Shughuli za Ziada Kwa Watoto Wadogo

  1. Weka wanasesere kadhaa kwa ajili ya watoto kucheza nao. Jadili umuhimu wa kusema “tafadhali” na “asante.” Wahimize watoto kushirikiana wanasesere wanapocheza pamoja na wengine na kuweka wanasesere pembeni wanapomaliza kucheza.

  2. Unaposema mstari ufuatao, waongoze watoto katika vitendo. Rudia kama watoto wanapendelea.

    Fanya kuwa na siku za furaha

    Macho mawili yanaona mambo mazuri ya kufanya (ota macho),

    Midomo miwili ya kutabasamu siku nzima (tabasamu tabasamu pana).

    Masikio mawili ya kusikia kile wengine wanachosema (kunja kiganja sikioni).

    Mikono miwili ya kuweka wanasesere pembeni (jifanye kuokota wanasesere na kuwaweka pembeni).

    Ulimi wa kusema maneno ya ukarimu kila siku (ota mdomo),

    Moyo wa upendo wa kufanya kazi na kucheza (weka mkono juu ya moyo),

    Miguu midogo ambayo hukimbia kwa furaha (ota miguu)—

    Fanya kuwa na siku za furaha kwa kila mmoja.

  3. Imbeni au semeni maneno ya “I Have Two Little Hands” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto uk, 272).