Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Kufundisha Ukitumia Kitabu Hiki cha Kiada


Kufundisha Ukitumia Kitabu Hiki cha Kiada

Kitabu cha kiada hiki kina masomo kwa ajili ya kufundishia watoto wenye umri wa miaka mitatu ifikapo Januari 1. Walimu wanaweza kutohoa kitabu hiki cha kiada kwa matumizi ya watoto wa miezi kumi na minane hadi miaka mitatu. Kama watoto wa chini ya miaka mitatu wanahudhuria masomo ya watoto wa darasa la Msingi, wanapaswa kutengwa na kuwekwa katika darasa la chekechea tofauti na watoto wa miaka mitatu isipokuwa kama kata au tawi hilo ni dogo sana. Ikiwa kuna watoto zaidi ya nane au kumi wa rika moja katika kata au tawi, darasa linaweza kugawanywa.

Walimu wa watoto wa chekechea wanapaswa kutazama “Kutohoa Kitabu hiki cha Kiada kwa Matumizi ya Chekechea,” kuanzia ukurasa wa x, kama nyongeza kwa sehemu hii.

Viongozi na walimu wanapaswa kwa maombi kuamua jinsi bora ya kupanga madarasa na kutumia masomo na shughuli katika kitabu hiki cha kiada ili kukidhi mahitaji ya watoto katika kata au tawi.

Darasa la Umri wa Miaka Mitatu

Watoto ambao wana umri wa miaka mitatu ifikapo Januari 1 wanakuwa katika darasa la umri wa miaka mitatu.

Madhumuni

Madhumuni ya darasa la umri wa miaka mitatu ni kuwasaidia watoto kukuza uelewa na upendo kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, kujihusisha na uzoefu chanya katika darasa la Msingi, na kukua katika hisia za kujithamini.

Maombi

Kila kipindi cha darasa kinapaswa kufunguliwa na kufungwa kwa maombi yanayotolewa na mtoto. Kwa kawaida maombi ya kufungua yatakuwa mwanzoni mwa muda wa somo, na maombi ya kufunga yatakuwa mwishoni mwa somo. Wafundishe watoto kutoa maombi mafupi na rahisi. Wasaidie kama inahitajika.

Ratiba ya Muda

Darasa hili hutoa muda wa mabadiliko ya pole pole kutoka darasa la chekechea hadi lile la Msingi rasmi. Wakati wa sehemu ya kwanza ya mwaka, inaweza kuwa vyema kwa watoto wa miaka mitatu kuwa na muda wa kushiriki na wa shughuli katika chumba chao wenyewe. Wakati wa sehemu inayobakia ya mwaka, wanaweza kwenda katika muda wa kushiriki pamoja na watoto wengine wa darasa la Msingi. Kupevuka kwa watoto wa darasa kutaamua wakati hasa wa darasa kufanya mabadiliko haya. Angalia watoto ili kuona wakati gani watakuwa tayari, na shauriana na urais wa darasa la Msingi kuamua ni lini mabadiliko yafanyike. Wenye umri wa miaka mitatu wanaweza kwenda kwenye zoezi la kufungua au kufunga pamoja na watoto wengine wa darasa la Msingi mwaka mzima.

Masomo kwa watoto wa darasa la Msingi kwa kawaida huchukua saa moja na dakika arobaini. Mazoezi ya kufungua au kufunga huchukua dakika ishirini, kukiwa na dakika tano za kwenda kwenye madarasa yao. Ikiwa wenye umri wa miaka mitatu wana muda wa kushiriki katika darasa lao wenyewe, muda wa darasa utakuwa dakika sabini na tano. Ratiba pendekezwa ifuatayo inaweza kuguezwa kulingana na mahitaji ya eneo.

Muda wa Salamu:

Dakika 10–15

Muda wa Somo

Dakika 25–35

Muda wa Kushirikiana na Muda wa Shughuli:

Dakika 20–25

Muda wa Kufunga

Dakika 10–15

Wakati wenye umri wa miaka mitatu wanapohudhuria muda wa kushiriki pamoja na wengine wa Msingi, muda wa darasa hutachukua dakika arobaini na kutakuwa na muda wa somo na muda mfupi wa salamu na muda wa kufunga

Muda wa Kusalimiana: Madhumuni ya muda wa kusalimiana ni kuwapatia watoto nafasi ya kuzungumza na wa kufahamiana na mwalimu na wengine katika mazingira yasiyo rasmi. Watoto watajiona wako salama na chanya zaidi kuhusu kuwa katika darasa la Msingi kama watakuwa huru kutembea tembea wakati huu.

Msaidie kila mtoto kujisikia kukaribishwa na kuona faraja kuwa katika darasa. Onyesha upendo, ukarimu na heshima kwa maneno na matendo yako. Jadili mahitaji ya watoto na mambo wanayopendelea. Mada sahihi za majadiliano zinaweza kuwa—

  • Matukio ya hivi karibuni katika maisha ya watoto, kama vile mtoto mpya nyumbani au matembezi ya familia.

  • Sikukuu Maalum.

  • Hali ya hewa.

  • Kuangalia mambo ya asili.

  • Ujuzi wa kijamii kama vile kusikiliza, kushiriki, au kutumia tabia njema.

  • Vitendo vya ukarimu.

Michezo ya vidole, mazoezi ya kuinama na kunyoosha, nyimbo pia zinaweza kutumika wakati huu ili kuwasaidia watoto kushinda ukosefu wa utulivu.

Muda wa Somo: Fuata mwongozo wa kawaida wa kila somo, ukitohoa kama inavyohitajika kwa darasa lako. Zingatia uelewa na upendeleo wa watoto. Chagua hadithi na shuguli ambazo zitafundisha vyema wana darasa lako kanuni muhimu za somo. Chagua kutoka kwenye sehemu ya “Shughuli za Kuboresha” sehemu ya shughuli yoyote unayoona itafanya kazi vyema kwa watoto wa darasa lako. Tumia shughuli hizi unapotaka wakati wa somo hili. Watoto hujifunza vyema kwa kurudiarudia, kwa hiyo ukitaka unaweza kutumia shughuli ile ile, nyimbo, hadithi, au maandiko zaidi ya mara moja wakati wa somo au katika masomo yanayofuata.

Fundisha masomo kwa mpangilio, isipokuwa somo la 45 na 46 (Pasaka na Krismasi).

Muda wa Kushirikiana na Muda wa Shughuli: Wakati watoto wanapokuwa na muda wa kushiriki darasa badala ya kuwa na watoto wengine wa darasa la Msingi, tumia shughuli hizo katika masomo na katika sehemu ya “Shughuli za Kuboresha” kwa muda wa kushirikiana. Ukitaka unaweza kurudia shughuli zinazopendwa na watoto kutoka kwenye masomo yaliyopita. Jumuisha muda wa kuimba nyimbo za watoto wa darasa la Msingi (tazama “Muziki Darasani,” uk. vii). Wahimize watoto kujumuika na kutoa mawazo yao kwa wengine.

Baada ya wenye umri wa miaka mitatu kuanza kuhudhuria muda wa kushirikiana pamoja na watoto wengine wa darasa la Msingi, wanaweza mara kwa mara kuombwa kufanya maonyesho katika muda wa kushiriki. Panga maonyesho rahisi ambayo yatawajumuisha watoto katika darasa lako. Unaweza—

  • Kuwasaidie watoto kuigiza hadithi au hali fulani kutoka kwenye mojawapo ya masomo.

  • Acha watoto watumie picha ili kuwasaidia kusimulia hadithi kutoka kwenye mojawapo ya masomo.

  • Acha kila mtoto aelezee maandiko au wazo kuhusu kanuni ya injili.

  • Waache watoto waimbe wimbo juu ya kanuni inayofundishwa.

Muda wa Kufunga: Rejea na ufanye muhtasari wa mawazo muhimu ya somo. Hasa taja kishazi kimoja au viwili vifupi vya maandiko kutoka kwenye somo, na usisitize mawazo muhimu ili kwamba watoto waweze kuyasimulia nyumbani. Mwalike mtoto atoe maombi ya kufunga.

Kuandaa Masomo

Kitu muhimu katika kufundisha watoto wadogo kwa ufanisi ni kuwajua na kuwapenda. Wajue na utumie majina ya washiriki wa darasa lako unapoongea nao. Fahamiana binafsi na wao na ujifunze kuhusu maisha yao. Tafuta njia ambazo zitawajumuisha katika masomo na kuyafanya masomo kuwagusa wao binafsi. Onyesha upendo ufaao na upendeleo kwa watoto wote katika darasa lako.

Kitu cha pili ni kujiandaa. Anza kuandaa kila somo angalau wiki moja kabla. Soma somo lote, kisha kwa maombi jifunze na uamue njia bora ya kufundisha kanuni kwa watoto katika darasa lako. Chagua Shughuli za Kuboresha za kujaliza shughuli katika somo na kuwafanya watoto wavutiwe na wajihusishe. Panga aina kadhaa za shughuli, na kisha uwe mwepesi kubadilika katika kuzitumia ili kukidhi mahitaji ya watoto. Lijue vyema vya kutosha somo lako kiasi kwamba hauhitaji kusoma kutoka kwenye kitabu cha kiada, na dumisha kuwasiliana kwa macho na watoto kadiri iwezekanavyo. Omba kila mara unapoandaa kila somo, na mtafute Roho hili akuongoze unapojiandaa na wakati wa kufundisha.

Kufundisha Masomo

Unapowafundisha watoto kanuni za injili, unapaswa kuhimiza watoto kupenda injili. Mapendekezo yafuatayo yanaweza kukusaidia kufanya darasa la watoto wa Msingi kuwa la kufurahisha kwa watoto katika darasa lako.

  • Wape watoto nafasi nyingi za kuzungumza na kushiriki.

  • Sikiliza wakati watoto wanasema, na ujaribu kujibu ukiwa chanya lakini ifaavyo.

  • Kuwa na shauku. Kama mwalimu anafurahia darasa la watoto wa Msingi, watoto watafurahia darasa la Msingi.

  • Sema kwa sauti ya upole.

  • Kuwa mvumilivu, mkarimu, na mwenye upendo, hasa wakati watoto wamechoka au wanapokosa utulivu.

  • Toa usikivu chanya kwa tabia nzuri na upuuze tabia hasi inapowezekana.

  • Andaa aina kadhaa za shughuli na uwe mwepesi kubadilika katika kuzitumia ili kukidhi mahitaji ya watoto. Watoto wadogo wana usikivu wa muda mfupi na wanahitaji kutembeatembea kila mara.

  • Jaribu kuwaelekeza tena watoto kuwa wasikivu wakati ubishi unapoibuka.

  • Kumbuka kwamba watoto hufurahia hadithi, vifaa vya picha, muziki na kutembeatembea. Wao hufurahia kurudirudia shughuli na nyimbo, hasa zile wanazozijua vyema.

Muziki Darasani

Kila somo katika kitabu hiki cha kiada hujumuisha nyimbo za kusaidia kuhimili mafundisho ya injili. Hauhitaji kuwa mwanamuziki mahiri ili kufanya kuimba darasani kuwa jambo la furaha na kuwa la maana. Watoto hawatajua kama unaimba vizuri au la; watajua tu kwamba wewe unapenda kuimba. Jifunze kila wimbo vizuri, ufanye mazoezi kama sehemu ya maandalizi ya somo lako. Kama kinapatikana Kitabu cha Nyimbo za Watoto kwenye kaseti za muziki (muziki tu, 52505; muziki na maneno, 52428) au diski (muziki tu 50505; muziki na maneno, 50428) zinaweza kukusaidia kujifunza nyimbo. Unaweza pia kutumia nyimbo hizi zilizorekodiwa mnapoimba darasani.

Nyimbo za kurudiarudia ni njia bora ya kuwafundisha watoto nyimbo. Ukitaka unaweza kutumia wimbo mmoja mara kadhaa katika somo hilo. Vitendo rahisi vinaweza kuwajumuisha watoto wadogo katika wimbo. Kama watoto wanajua wimbo vyema na wanafurahia kuuimba, uimbe kila mara katika muda wa somo au muda wa kushiriki na muda wa shughuli.

Kufundisha watoto wimbo au shughuli mpya—

  • Kariri wimbo au mstari wa shughuli kabla ya darasa.

  • Tanguliza wimbo mpya au shughuli kwa kuimba wimbo au kuusema kwa watoto. Fanya vitendo kwa kutia chumvi, kama kuna chochote.

  • Waalike watoto waimbe au waseme maneno pamoja nawe. Hawatajua maneno mara moja, lakini kama utarudiarudia wimbo au shughuli mara kadhaa, watajifunza maneno yake.

  • Nenda pole pole ili watoto waelewe maneno na vitendo.

  • Tumia vifaa vya picha mara kwa mara ili kuwasilisha wimbo au mstari wa shughuli. Watoto huwa makini na kujifunza vizuri wanapokuwa na kitu cha kutazama.

  • Fupisha wimbo au mstari wa shughuli kama watoto wanakosa utulivu. Kama wimbo au mstari wa shughuli ni mrefu, ukitaka unaweza kuwasaidia watoto kufanya vitendo huku ukiimba au kusema maneno pekee.

Watoto wadogo hawatataka kuimba pamoja nawe kila mara, lakini watafurahia kushiriki kwa kusikiliza uimbaji.

Vifaa vya Picha

Vifaa vya picha ni muhimu katika kufundisha watoto wadogo. Picha, mikato, vyombo, na vifaa vingine wa picha vinaweza kupata na kudumisha usikivu wa watoto, vikiwasaidia watoto kukumbuka kile ambacho wewe unafundisha.

Picha na mikato iliyotajwa katika masomo imejumuishwa katika kitabu hiki cha kiada. Sehemu ya “Maandalizi” ya kila somo inaorodhesha picha zilizotumiwa katika somo hilo kwa kichwa na nambari. Nambari zilizo katika mabano hutambulisha kila picha (au kama hiyo) katika Sanaa ya Picha za Injili (34730 au 34735) na maktaba ya jumba la mikutano. Sehemu ya “Maandalizi” pia inaorodhesha mikato kwa nambari zake katika kitabu cha kiada na Mikato ya Vifaa vya Picha (33230–33250 au 08456) ambayo hujumuisha mikato kama hiyo.

Vitu uwa vifaa bora vya kuona kwa macho, hasa kama ni vitu vya kawaida ambavyo watoto wanaweza kuvigusa au kuvishika. Unaposimulia hadithi ya maandiko, tumia maandiko yako mwenyewe au maandiko kutoka kwenye maktaba ya jumba la mikutano kama vifaa vya picha.

Miongozo Maalum kwa ajili ya kuwajumuisha Watoto wenye Ulemavu

Mwokozi alionyesha mfano kwetu kwa kuona huruma kwa wale watu waliokuwa na ulemavu. Alipowatembea Wanefi baada ufufuko wake, alisema:

“Mnao wowote ambao ni wagonjwa miongoni mwenu? Waleteni hapa. Mnao wowote ambao ni viwete, au vipofu, au wa kupooza, au vilema, au ukoma, au walionyauka au ni viziwi, au ambao wanateseka kwa njia yoyote? Waleteni hapa na nitawaponya, kwani nina huruma juu yenu” (3 Nefi 17:7).

Kama mwalimu wa darasa la Msingi una nafasi nzuri ya kuonyesha huruma. Ingawa haujafunzwa kutoa msaada wa kitaalamu, kama mwalimu unaweza kuwaelewa na kuwatunza watoto walio na ulemavu. Kujali, kuelewa na hamu ya kumjumuisha kila mwana darasa katika shughuli za kujifunza huitajika.

Watoto walio na ulemavu wanaweza kuguswa na Roho bila kujali kiwango chao cha uelewa. Ingawa baadhi ya watoto yawezekana wasiweze kuhudhuria kwa muda wote wa darasa la Msingi, wanahitaji kuwa na nafasi ya kuhudhuria kwa muda mfupi ili kumhisi Roho Mtakatifu. Inaweza kulazimu kuwa na mwenzi ambaye ana usikivu wa mahitaji ya mtoto huyo awe pamoja na mtoto wakati wa kipindi cha darasa la watoto wa Msingi endapo mtoto anahitaji kuwa mbali na kundi lote.

Baadhi ya washiriki wa darasa wanaweza kuwa na changamoto katika kujifunza, kama vile kuona, kusikia, mtindio wa ubongo, lugha au matatizo ya kusema, shida za tabia na shida za kijamii, ugonjwa wa akili, shida ya kutembea, au matatizo sugu ya kiafya. Baadhi wanaweza kuona lugha au taratibu za kiutamaduni kuwa ngeni na ngumu. Bila kujali hali za watu binafsi, kila mtoto ana mahitaji sawa sawa ya kupendwa na kukubaliwa, kujifunza injili, kumhisi Roho Mtakatifu, na kushiriki kikamilifu, na kuwahudumia wengine.

Miongozo hii inaweza kukusadia wewe kumfundisha mtoto mwenye ulemavu.

  • Tazama zaidi ya ulemavu na mjue huyo mtoto. Kuwa wa kawaida, rafiki, na mkunjufu.

  • Jifunze kuhusu uwezo maalumu wa mtoto na changamoto zake.

  • Fanya kila juhudi kufundisha na kukumbusha washiriki wa darasa juu ya jukumu lao la kumheshimu kila mwana darasa. Kumsaidia mwana darasa aliye na ulemavu linaweza kuwa tukio la kujifunza kuwa kama Kristo kwa darasa lote.

  • Tafuta mbinu bora za kumfundisha mtoto kwa kushauriana na wazazi, na wana familia wengine, na kwa wakati ufaao, na mtoto mwenyewe.

  • Kabla ya kumwita mtoto aliye na ulemavu kutoa maombi au kushiriki kwa namna nyingine, muulize jinsi anavyojisikia kuhusu kushiriki darasani. Sisitiza uwezo na vipaji vya kila mtoto na utafute njia ambazo kila mmoja anaweza kushiriki kwa faraja na kwa ufanisi.

  • Tohoa vifaa vya somo na mazingira asili ili kukidhi mahitaji ya watoto walio na ulemavu.

Vifaa vya ziada vya kufundisha watoto walio na ulemavu vinapatikana kutoka vituo vya usambazaji vya Kanisa (tazama “Materials for Those with Disabilities” katika katalogi ya Kituo cha Usambazji cha Salt Lake).