Miitaala kwa ajili ya Msingi na Wakati wa Kushiriki
Somo la 15: Sabato ni Siku ya Kuabudu


Somo la 15

Sabato ni Siku ya Kuabudu

Madhumuni

Ni kumsaidia kila mtoto kuelewa kwamba Sabato ni siku ya kuabudu na kumpumzika.

Maandalizi

  1. Kwa maombi jifunze Mwanzo 2:1-3 na Kutoka 16:11–31. Ona pia Kanuni za Injili (31110), .sura ya 24.

  2. Vifaa vinavyohitajika:

    1. Biblia.

    2. Picha 1-6, Jioni ya Familia Nyumbani (62521); picha 1-7, Familia Yenye Upendo; picha 1-8, Kupitisha Sakramenti (62021); picha 1-9 Sala ya Asubuhi (62310); picha 1-10, Sala ya Familia (62275); picha 1-35, Kukusanya Mana; picha 1-36, Watoto na Mzazi Wakisoma Hadithi ya Maandiko.

  3. Fanya maandalizi yanayohitajika kwa Shughuli zo zote za Kuboresha unazotaka kutumia.

Shughuli za Kujifunza

Mwalike mtoto atoe maombi ya kufungua.

Shughuli ya Usikivu

Wasaidie watoto kuigiza kila siku ya Uumbaji huku ukiwakumbusha juu ya kile kilichoumbwa kila siku (ona Mwanzo 1):

Siku ya kwanza

Jifanye umelala na kisha uamke, kuashiria usiku na mchana.

Siku ya pili

Simama, tazama juu, na unyoshe na kufungua mikono yako kuashiria anga.

Siku ya tatu

Inama na utwae ua na kisha ulinuse lile ua.

Siku ya nne

Fanya duara kubwa kwa mikono yako kuashiria jua na duara ndogo kuashiria mwezi, kisha chezesha vidole vyako huku vidole vyako vikitembea tembea kuashiria nyota zikimetameta.

Siku ya 5

Jifanye kuwa ndege anayeruka chumbani au samaki anayeogelea baharini.

Siku ya 6

Jifanye kuwa mnyama. Tetembea chumbani mara kadhaa ukiigiza mnyama huyo. Kisha simameni katika mstari na kila mmoja aseme, “Jina langu ni (jina la mtoto). Mimi ni mtoto wa Mungu.”

Acha watoto waketi chini kimya kimya.

Waambie watoto kwamba katika siku ya saba, Baba wa Mbinguni na Yesu walipumzika. Waliita siku hiyo ya kupumzika Sabato.

Acha watoto waseme neno Sabato mara kadha.

Sabato ni siku takatifu

Soma kwa sauti Mwanzo 2:1–2 na mstari Mwanzo 2:3 mpaka neno siku. Elezea kwamba wakati Baba wa Mbinguni na Yesu walipomaliza kuiumba dunia na kila kitu kilichopo ndani yake, waliibariki siku ya saba. Ilitakiwa kuwa siku takatifu, tofauti na zile siku zingine za wiki. Sabato ni siku yetu ya kupumzika kutokana na kazi zetu na, kumwambudu Baba wa Mbinguni na Yesu.

  • Sabato ni siku gani ya wiki?

  • Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walifanya nini siku ya Sabato? (Ona Mwanzo 2:2.)

Shughuli

Acha watoto wanyoshe juu vidole saba. Hesabu mpaka saba pamoja nao, ukunje kila kidole kinapohesabiwa. Elezea kwamba siku sita (chezesha vidole sita), tunafanya kazi. Siku ya saba (chezesha kidole cha saba peke yake), tunapumzika kutokana na kazi zetu kwa sababu ni siku ya Sabato.

Hadithi

Onyesha picha 1-35, Kukusanya Mana, na usimulie hadithi ya Waisraeli na mana, kama inavyopatikana katika Kutoka 4:11–31.

Wasaidie watoto kuelewa muujiza wa mana. Elezea kwamba kila siku Waisraeli wakikusanya mana ya kutosha kwa siku hiyo, lakini siku ya sita walikusanya mana ya kutosha siku mbili. Kama Waisraeli wangekusanya mana zaidi siku yo yote ila siku ya sita, ingeharibika. Katika siku ya saba, ambayo ilikuwa Sabato, kulikuwa hakuna mana ya kukusanya. Siku hiyo Waisraeli walikula mana ya ziada iliyokusanywa siku ya sita.

  • Waisraeli walipataje chakula chao?

  • Kwa nini hawakukusanya mana siku ya Sabato?

Soma Kutoka 16:26 kwa sauti. Elezea kwamba Waisraeli walifundishwa kuwa wasifanye kazi siku ya Sabato. Siku ya Sabato, Baba wa Mbinguni na Yesu wanataka tufikirie juu yao badala juu ya kazi yetu. Sabato ni siku takatifu sana kwa Baba wa Mbinguni na Yesu.

Sisitiza kwamba Sabato sio siku ya kufanya kazi na mambo ya kawaida bali ni siku ya kumwabudu Baba wa Mbinguni na Yesu. Kuabudu humaanisha kufikiria kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu na kufanya mambo ambayo yanaonyesha jinsi tunavyowapenda wao.

Sabato ni siku ya kuabudu

Wasaidie watoto kuelewa kwamba Sabato ni siku ya furaha kwa sababu tunaweza kuwaabudu Baba wa Mbinguni na Yesu katika njia tofauti.

  • Umefanya nini leo kuwaonyesha Baba wa Mbinguni na Yesu kuwa unawapenda?

Elezea kwamba njia moja muhimu tunayoweza kuwaabudu, Baba wa Mbinguni na Yesu au kuwaonyesha kwamba tunawapenda, ni kuja kanisani na kupokea Sakramenti. Onyesha picha 1-8, Kupitisha Sakramenti. Baba wa Mbinguni na Yesu hufurahia tunapoimba na tunapokuwa watulivu na kuwa na tabia njema ili tuweze kuwasikiliza walimu wetu na kuhisi upendo wa Baba wa Mbinguni na Yesu kwetu.

Shughuli

Wasaidie watoto kufanya mchezo ufuatao wa vidole:

Mimi Nafurahi Nimekuja Kanisani Leo

Mimi nafurahi kuwa nimekuja kanisani leo (piga makofi na ujenge mnara wa kanisa kwa kuweka vidole vya mbele pamoja).

Mimi najifunza kusikiliza (kunja kiganja sikioni).

Na kusali (kunja mikono na uinamishe kichwa).

Najifunza kuhusu Yesu aliye juu (onyesha juu);

Ninafikiria juu ya Kristo na upendo wake (jikumbatie mweyewe).

Pia tunamwonyesha Baba wa Mbinguni na Yesu kwamba tunawapenda kwa kuwa nadhifu na safi tunapokuja kanisani. Tunapaswa kunawa nyuso zetu na kuchana nywele na kuvaa nguo nzuri.

Shughuli

Acha watoto wafanye igizo la kujiandaa kwenda kanisani.

  • Tunafanya nini ili kumwabudu Baba wa Mbinguni na Yesu tunapokuwa kanisani?

  • Tunafanya nini ili kumwabudu Baba wa Mbinguni na Yesu tunapokuwa nyumbani?

Wasaidie watoto kuelewa kwamba hatupaswi kutumia hela au kununua vitu siku ya Sabato. Hatupaswi kwenda kwenye shughuli za michezo au burudani siku ya Sabato. Hatupaswi kufanya kazi za bustani au shambani au kwenda kuvua samaki au kuwinda siku ya Sabato.

Elezea kwamba kuna vitu vingi vya kufanya nyumbani ili kuitukuza siku ya Sabato. Onyesha picha kutoka kwenye sehemu ya “Maandalizi” wakati ufaao katika mazungumzo haya. Tunaweza kucheza michezo ya utulivu pamoja na wana familia, kusomewa hadithi za maandiko, kutengeneza albamu ya picha za familia, kutembelea jamaa au wale ambao ni wagonjwa, kuchora picha za vitu ambavyo tunashukuru kwa kuwa navyo, kutembea pamoja na mwana familia, kusali, kuimba nyimbo, na kusikiliza muziki mzuri.

Shughuli

Waache watoto wachukue zamu kuigiza mambo ambayo wanafurahia kufanya nyumbani ili kuitukuza siku ya Sabato.

Ushuhuda

Waambie watoto kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu hufurahia tunapokwenda kanisani siku ya Sabato na tunapoimba, kusali, na kuwasikiliza walimu wetu. Wao pia hufurahia tunapotenda ifaavyo nyumbani siku ya Sabato. Zungumza kuhusu mambo ya staha unayopenda kufanya siku ya Sabato, na uelezee jinsi unavyosikia furaha siku ya Sabato. Wahimize watoto kuwaelezea familia zao kile ambacho wamejifunza katika somo hili.

Shughuli za Kuboresha

Chagua baadhi ya shughuli hizi ili uzitumie katika somo.

  1. Fanya shughuli ifuatayo, ukitengeneza mstari kwa kila mtoto katika darasa lako. Waalike watoto wafanye vitendo pamoja nawe.

    Kwa Sababu Leo ni Jumapili

    Onyesha kwa mtoto katika darasa lako na useme jina la mtoto huyu unaposema mstari huu na kufanya kitendo kinachoelezwa:

    (Jina la mtoto) alisikiliza maandiko leo (kunja kiganja sikioni).

    (Jina la mtoto) alisikiliza maandiko leo, kwa sababu leo ni Jumapili.

    Sema mstari kwa kila mtoto, ukitumia mawazo yafuatayo katika umbo lililo hapo juu:

    (Jina la mtoto) alisali katika darasa la Msingi leo (kuja mikono, inamisha kichwa, funga macho).

    (Jina la mtoto) alichora picha leo (jifanye unachora kwa mkono).

    (Jina la mtoto) alimtembelea mtu ambaye alikuwa mpweke leo (salimiana kwa mkono na mtoto aliyetajwa).

    (Jina la mtoto) alijifundisha kuhusu historia ya familia leo (jifanye kufungua kurasa na kutazama picha).

    (Jina la mtoto) aliwaandikia barua Babu na Bibi leo (fanya mkono kama vile unaandika).

    (Jina la mtoto) alisikiliza hadithi leo (kunja kiganja sikioni)

  2. Simulia hadithi ifuatayo kwa maneno yako mwenyewe:

    Watangulizi walisafiri maili nyingi kufika Bonde la Salt Lake ili kuishi hapo. Waliwasili siku chache kabla ya Sabato. Ingawa kulikuwa na nyumba za kujenga na mazao ya kupanda, waliamua wasifanye kazi siku ya Sabato. Walifanya kazi kwa bidii na upesi sana kulima na kuandaa kwa ajili ya kupanda. Ardhi lilkuwa ngumu sana, kwa hivyo ilibidi wainyunyizie maji ili majembe yaweze kupita. Kufikia Jumamosi usiku, shamba kubwa la mboga lilikuwa limepandwa. Jumapili asubuhi, walikutana kwa mikutano yao ya Sabato na wakamshukuru Baba wa Mbinguni kwa kuwaleta kwenye nchi mpya ya kuishi.

  3. Acha mtoto achore picha ya kwake mwenyewe akifanya shughuli ya Sabato. Waache watoto waambiane kuhusu picha zao. Andika kila picha jina na mtoto na shughuli, kama ilivyo katika mfano huu David huimba nyimbo za Msingi siku ya Sabato.

Shughuli za Ziada Kwa Watoto Wadogo

  1. Wasaidie watoto kufanya vitendo vya mstari wa shughuli huku ukisema maneno haya:

    Uumbaji

    Yesu alisema jua liangaze (fanya duara kubwa juu ya kichwa kwa mikono),

    Mvua inyeshe (teremsha mikono chini mbele ya mwili wako ukichezesha chezesha vidole),

    Maua na yakue (kunja mikono, viganja vikielekea juu).

    Yesu alisema ndege na waimbe (fungua na ufunge vidole mfano wa mdomo wa ndege),

    Na ikawa hivyo, ikawa hivyo (kunja mikono).

    (Jonhnie B. Wood, katika Sing, Look, Do, Action Songs for Children, ed. Dorothy M. Peterson [Cincinnati: Standard Publishing Co., 1965].)

    Elezea kwamba baada ya uumbaji wa dunia kukamilika, Baba wa Mbinguni na Yesu walipumzika. Sabato ni siku ambayo tunapumzika na kuwakumbuka Baba wa Mbinguni na Yesu.

  2. Wakumbushe watoto kwamba tunapofanya kazi yetu Jumamosi inafanya iwe rahisi kwetu kuwakumbuka Yesu na Baba wa Mbinguni siku ya Jumapili. Imbeni ”Saturday” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, uk.196), mkitumia vitendo vinavyopendekezwa na maneno.