Utangulizi wa1 Nefi
Kwa nini ujifunze Kitabu Hiki?
Unapojifunza 1 Nefi, utagundua kwamba “huruma nyororo ya Bwana iko juu ya wale ambao amewachagua, kwa sababu ya imani yao, kuwatia nguvu” (1 Nefi 1:20). Kwa mfano, utaona jinsi Mungu alivyomsaidia Nefi kupata mabamba ya shaba ili familia yake ipate kuwa na maandiko, jinsi Mungu alivyomwokoa Nefi kutokana na vitisho dhidi ya maisha yake, jinsi Mungu alivyomwokoa Lehi na watu wake kutokana na baa la njaa huko nyikani na maangamizo huko baharini, kuwapeleka salama kwenye nchi ya ahadi.
Lehi na watu wake walipata uzoefu wa huruma na usaidizi wa Mungu walipofuata amri. Lehi na Nefi walitafuta mwongozo kutoka kwa Mungu na kuupokea kupitia maandiko, ndoto, maono, na Liahona. Nefi alipokea na kuandika ono la historia ya ulimwengu ambalo lilimwonyesha uwezo wote wa maarifa ya Mungu. Kupitia maono, Nefi aliona ubatizo wa siku zijazo, huduma, na kusulubishwa kwa Yesu Kristo.
Unapojifunza uzoefu wa Nefi na Lehi katika kitabu hiki, unaweza kujifundisha jinsi ya kutafuta na kupokea baraka za mbinguni katika maisha yako.
Nani Aliandika Kitabu Hiki?
Nefi mwana wa Lehi aliandika kitabu hiki kama jibu la amri ya Bwana kwamba yeye aweke kumbukumbu ya watu wake. Nefi kuna uwezekano alizaliwa Yerusalemu au karibu na hapo. Aliishi huko wakati wa huduma ya nabii Yeremia na enzi ya Mfalme Zedekia.
Nefi alitafuta ushuhuda wake mwenyewe kuhusu maneno ya baba yake kuhusu maangamizo ya Yerusalemu na haja ya familia yao ya kuondoka. Alipoendelea kutafuta na kufuata ushauri wa Bwana, Nefi alikuwa chombo katika mikono ya Mungu. Yeye kwa utiifu alirudi Yerusalemu na ndugu zake mara mbili—kwanza kutafuta mabamba ya shaba na baadaye kushawishi familia ya Ishmaili ijiunge na familia ya Lehi huko nyikani. Kwa usaidizi wa Bwana, Nefi alijenga merikebu ambayo ilibeba familia yake na wengine kuvuka bahari hadi nchi ya ahadi. Lehi alipokufa, Bwana alimchagua Nefi kuwa kiongozi wa watu wake.
Kiliandikwa lini na wapi?
Nefi aliandika taarifa ambayo ilikuja kuwa 1 Nefi karibu mwaka wa 570Kabla Kristo Kuzaliwa—miaka 30 baada ya yeye na familia kuondoka Yerusalemu (ona 2 Nefi 5: 28–31). Alikiandika alipokuwa katika nchi ya Nefi.